Uchunguzi upangaji wa matokeo Katavi ufanyike haraka

Uchunguzi upangaji wa matokeo Katavi ufanyike haraka

263
0
KUSHIRIKI

JUZI Shirikisho la soka Tanzania (TFF)  lilikiagiza Chama cha soka Mkoa wa  Katavi (KRFA), kufanya uchunguzi wa  kina kuhusiana na upangaji wa matokeo katika mchezo wa mwisho wa Ligi ya mkoa huo.

Mchezo huo ulikuwa ni kati ya Stand FC dhidi ya Kazima, ambapo Stand iliifunga Kazima mabao 16-0 hali iliyopelekea shaka kwa TFF na kutoa maagizo kwa  KRFA isitangaze bingwa wa mkoa huo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

TFF ilikiagiza chama hicho cha mkoa kuziagiza kamati zake kufanya uchunguzi ili ikibainika kama ni kweli ulikuwepo upangaji wa matokeo wachukuliwe hatua kutokana na kanuni ilizowekwa na shirikisho hilo.

Kabla ya mchezo huo timu ya Nyundo ilikuwa ikiongoza ligi hiyo ikiwa tayari na pointi 21, mabao 24 ya kufunga wakati Stand ilikuwa ikihitaji ushindi wa mabao 13 ili iweze kuwa bingwa wa Mkoa wa Katavi.

BINGWA tunasema hongera TFF kwa uamuzi huo wa kuagiza chama cha soka kifanya uchunguzi wa kina kuhusiana na shaka ya upangaji wa matokeo hayo, ambapo ilipelekea Stand kuwa bingwa wa mkoa huo.

TFF hadi kufikia kutoka uwamuzi huo tayari ilikuwa na wasiwasi kuhusiana na matokeo ya mchezo huo, haingii akilini kuona timu inashinda mabao 16 wakati haijawahi kufanya hivyo toka ilipoanzishwa miaka kadhaa iliyopita.

BINGWA tunaomba uchunguzi huo ufanywe haraka ili adhabu itolewe kwa wahusika wote kabla ya muda kupita, sidhani kama suala hili linaweza kuchukua muda mwingi, tuna imani  kwamba KRFA itatoa ushirikiano wa kutosha juu ya hilo.

Tuna imani kwamba endapo suala hili likitolewa maamuzi mapema hata wale wengine waliokuwa na mpango wa kupanga matokeo kama wapo wataogopa, kitendo cha upangaji wa matokeo kinatakiwa kupigwa vita na kila mpenda soka hapa nchini.

Upangaji wa matokeo umekuwa ukidhoofisha soka letu, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wadau kukata tamaa na kusaidia sekta hii muhimu hapa nchini, hivyo basi nia yetu ni kuona suala hili linadhibitiwa kwa kutoa adhabu kali kwa wahusika.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU