Mayanja mfalme wa ‘sub’

Mayanja mfalme wa ‘sub’

400
0
KUSHIRIKI

mayanja-akiwa-kazini-simba_1836bf5vzqefk17bhy3wmcr520NA MSHAMU NGOJWIKE

ACHANA na rekodi ambazo amekuwa akivunja kila siku, Kocha wa Simba Mganda, Jackson Mayanja, amezidi kuwa mjanja kulinganisha na makocha kadhaa waliopita kwa Wekundu hao wa Msimbazi katika siku za karibuni kutokana na kuwa bora sana kwenye kufanya mabadiliko ambayo yamekuwa yakitoa faida kwenye kikosi chake msimu huu.

Mayanja amekuwa akifanya mabadiliko ambayo yamemsaidia kumpa matokeo mazuri tofauti na makocha waliopita kama Dylan Kerr, Milovan Cirkovick, Patrick Liewig, Goran Kopunovic na Zdravko Logarusic, huku akikonga mioyo ya mashabiki kwa ‘teknik’ yake ya kufanya ‘sub’.

Mara nyingi toka achukue mikoba ya kukinoa kikosi cha Simba kutokea mikononi mwa Mwingereza, Dylan Kerr, Mayanja amekuwa akiwatupa benchi baadhi ya wachezaji kama, Daniel Lyanga, Said Ndemla, Awadhi Juma na mara nyingine, Hassani Ramadhani ‘Kessy’.

Katika mabadiliko aliyofanya Mayanja kwenye mechi sita zilizopita dhidi ya Yanga, Singida United, Mbeya City, Ndanda FC, Tanzania Prisons na Coastal Union, yalikuwa na tija kiasi cha kupelekea kupata matokeo wakati timu ilipokuwa imepotea ama kulinda mabao yao.

 

SIMBA VS YANGA

Licha ya Simba kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga, lakini mabadiliko ambayo aliyafanya Mayanja ya kumuingiza Novaty Lufunga baada ya Abdi Banda kupata kadi nyekundu yalishusha presha na ukuta wa Simba kuimarika.

Baada ya kutolewa kwa Banda katika mchezo huo, Simba ilikuwa imeelemewa kwenye safu ya ulinzi lakini alipomuingiza Lufunga alipunguza presha za washambualiaji wa Yanga, Donald Ngoma na Amissi Tambwe.

Katika mechi hiyo ya kusisimua, washambuliaji wa Yanga walionekana kuwa na uchu wa kufunga kiasi cha mashabiki wengi kufahamu yale mabao 5-0 ya msimu wa 2010/11 ndio yanaweza kurudi lakini Lufunga na Jjuuko Murshid waliweza kuwa imara kwenye safu ya ulinzi hata kama Banda alitoka.

 

SIMBA VS SINGIDA UNITED

Lakini, Mayanja alizidi kuonekana kuwa ni mtamu zaidi katika ‘sub’ baada ya kufanya mabadiliko kwenye mechi ya FA dhidi ya Stand United ambayo Simba ilishinda mabao 5-1.

Katika mchezo huo, Mayanja aliwaingiza Mussa Hassani ‘Mgosi’, Said Ndemla pamoja na Peter Mwalyanzi ambao walikuja kuonyesha mabadiliko makubwa na kuifanya Simba waibuke na ushindi huo.

Simba ilionekana haina maelewano mazuri katika mchezo huo, kiasi cha kupoteza nafasi nyingi za mabao ya kufunga ndipo Mayanja akafanya mabadiliko ambayo yalileta uhai na kuibuka na ushindi.

 

SIMBA VS MBEYA CITY

Mayanja aliwaacha midomo wazi mshabiki wa soka alipofanya mabadiliko yenye tija katika mechi dhidi ya Mbeya City ambayo Simba ilishinda mabao 2-0.

Katika mchezo huo, Mayanja aliwaingiza Hassan Ramadhani ‘Kessy’ pamoja na Daniel Lyanga ambao walibadili upepo wa mechi hiyo kipindi cha pili na Simba kupata ushindi.

Kuingia kwa Lyanga kuliifanya Simba kupata bao la kuongoza dakika ya 75, kabla ya beki wa Mbeya City, Hassan Mwakipasile, kujifunga dakika za mwisho kutokana na kazi nzuri ya Ibrahim Ajib.

 

SIMBA VS NDANDA FC

Katika mchezo wa Simba dhidi ya Ndanda ambao Simba ilichomoza na ushindi wa mabao 3-0, Mayanja alifanya ‘sub’ ya maana kumuingiza Lyanga ambaye alikuja kubadili sura ya mchezo huo.

Simba ilionekana hajaelewana sana katika safu ya ushambuliaji lakini kuingia kwa Lyanga kulifanya mchezo kuchangamka na kupata mabao ya haraka.

Mayanja amekuwa akimtumia sana Lyanga katika ‘sub’ nyingi kuja kubadili upepo wa mchezo na mara nyingi alifanikiwa toka atue akichukua mikoba ya Dylan Kerr aliyefukuzwa mwanzoni mwa Januari.

SIMBA VS TANZANIA PRISONS

Kiungo, Awadhi Juma, alikuja kubadili upepo wa mchezo kati ya Simba dhidi ya Tanzania Prisons ambao wekundu hao wa Msimbazi walishinda bao 1-0.

Bao hilo, Awadh alifunga dakika ya 86 kwa shuti la mita 19 na ushee akimalizia pasi ya kiungo, Jonas Mkude dakika chache kuingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya kiungo Mzimbabwe, Justice Majabvi.

Katika mchezo huo, Simba ilikamatwa kila idara lakini Mayanja alifanya ‘sub’ ambayo ilileta matunda kwa kupata pointi tatu muhimu kwenye mechi hiyo.

 

SIMBA NA COASTAL UNION

Licha ya Simba kufungwa na kuondoshwa katika Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Coastal Union kwa mabao 2-1 lakini Mayanja alifanya ‘sub’ ya maana ambayo iliwarejesha vijana hao kwenye ‘game’.

Katika mchezo huo ambao ulipigwa Jumatatu iliyopita, Mayanja alifany ‘sub’ kwa kumuingiza Hamisi Kiiza ‘Diego’ ambaye alichukua nafasi ya Justice Majabvi na kusawazisha bao la Simba dakika ya 47 baada ya Coastal kupata bao dakika ya 19 likifungwa na Mcameroon, Youssouf Sabo.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU