Yanga tulizeni akili Medeama si wakubezwa

Yanga tulizeni akili Medeama si wakubezwa

522
0
KUSHIRIKI

NA EZEKIEL TENDWA

Sirtendwa@gmail.com

0789291209

JUNI 28 mwaka huu, wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Yanga  walijikuta wakipata matokeo mabaya, baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),  uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kilikuwa ni kipigo cha pili mfululizo katika michuano hiyo, kwani Juni 19 mwaka huu walifungwa bao 1-0 na Mo Bejaia ya Algeria  mchezo ulichezwa ugenini.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuburuza mkia katika kundi  A wakiwa hawana pointi wala bao walilofunga  huku TP Mazembe wakiongoza kwa  pointi sita baada ya kuifunga mabao 3-1, Medeama ya Ghana katika mchezo wa kwanza uliochezwa Juni 19 mwaka kwenye Uwanja wa Stade du TP Mazembe, Lubumbashi, kisha Yanga.

Baada ya kucheza na TP Mazembe, sasa Yanga wanajiandaa kucheza na Medeama katika mchezo utakaochezwa Julai 16 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, ambao kwenye kundi lao wanashika nafasi ya tatu.

Medeama ambao wanaonekana si timu ya kutisha katika kundi lao, wamefungwa mchezo mmoja, lakini wakitoka suhuhu na Mo Bejaia uliochezwa Julai 29 mwaka huu nchini Ghana.

Pamoja na Yanga kupoteza mechi mbili, lakini wana nafasi ya kupenya hatua inayofuata iwapo watapata matokeo mazuri kwa mechi zilizosalia huku wapinzani wao wengine kwenye kundi hilo wakipoteza.

Yanga wanatakiwa kushinda dhidi ya Medeama ili kujiweka katika mazingira mazuri, ambayo itaweza kutuliza presha ya mashabiki wao wanaoonekana kuumizwa na vipigo viwili mfululizo.

Ni muhimu Yanga kushinda mechi hiyo ambayo itafunga mzunguko wa kwanza kwenye kundi lao ili waweze kutoka mkiani na kushika nafasi ya tatu kwa kuwashusha Waghana hao.

Mechi hiyo itaonyesha mwelekeo wa Yanga, kwani wakishinda watakuwa wametengeneza mazingira mazuri ya kusogea hatua moja mbele lakini wakipoteza watakuwa wanajitengenezea mlima mrefu ambao huenda wakashindwa kuuvuka.

Ninachoweza kuwashauri kuelekea mchezo huo ni kwamba, wanakutana na timu ambayo nayo inatafuta matokeo mazuri ili ipate nafasi ya kusonga mbele hivyo kama Yanga watajidanganya kuwa wanakutana na timu nyepesi jambo hilo linaweza kuwagharimu.

Ni kweli kwamba kabla ya mechi yao ya kwanza dhidi ya TP Mazembe, tulisikia  kupitia vyombo vya habari nchini Ghana vikisema Medeama wanatishia kutosafiri kwenda Congo kutokana na ukata unaowakabili, lakini baadaye walikwenda kucheza na kupokea kipigo cha mabao 3-1.

Zinaweza pia zikaja taarifa kwamba Waghana hao hawatakuja kwa madai yaleyale ya ukata,  lakini hilo lisije likawafanya Yanga kulala.

Lisije likawafanya Yanga kupiga usingizi wa pono kwani siku hizi ujanja ujanja mwingi sana hasa katika soka letu la Afrika.

Ni kweli kwamba, Medeama ni timu ndogo ambayo haina mafanikio sana katika michuano hii ya Afrika kwani rekodi yao inaonyesha klabu hiyo imeanzishwa Aprili 18, 2002, tofauti na klabu ya Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935, lakini hiyo si tija na wala si silaha ya kuwafanya wawakilishi wetu hawa wawabeze.

Jambo la kufurahisha hapa ni kwamba, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Van de Pluijm, anao uzoefu mkubwa na soka la Ghana kwani huko ni kama nyumbani kwao ndiyo maana hata likizo huwezi kusikia anakwenda kokote zaidi ya nchini humo.

Angalizo lingine ambalo Yanga wanatakiwa kuna nalo macho ni kuachana na zile tabia za kuamini kuwa wanahujumiwa hasa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama walivyotunisha msuli wakati wanakabiliwa na mchezo dhidi ya TP Mazembe.

Yanga walitumia nguvu nyingi kwenye vyombo vya habari kutangaza kwamba wanaonewa na kama nguvu ile waliyoitumia wangeitumia kuhamasisha mashabiki wao kuipa sapoti timu yao nadhani ingewasaidia sana.

Naamini Yanga ni timu nzuri kwa sasa hasa kutokana na utulivu wao walionao, umoja na mshikamano, ikichagizwa na usajili mzuri walioufanya hivyo kama watatulia nafasi yao ya kusonga mbele katika michuano hii ya Afrika ipo wazi.

Ni ukweli ulio wazi kuwa Medeama si timu ya kubeza kwani mpaka wamefika hatua hii wamepishana na mishale mingi,  hivyo Yanga wasije wakadharau kwani Waswahili tuna msemo wetu usemao ‘mdharau mwiba mguu huota tende’.

Nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara kwamba pasi nyingi zisizo na mabao haziwezi kuisaidia timu na ndicho hicho kinachotokea kila mara kwa Yanga.

Imejitokeza mara nyingi kuisifu Yanga kwamba wanacheza kandanda la kuvutia,  lakini mwisho wa siku wapinzani wao ndio wanaotoka na pointi tatu ndiyo maana huwa najiuliza nani mwenye faida kati ya anayecheza pasi nyingi na yule anayetoka uwanjani na pointi tatu?

Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Etoile du Saleh, Yanga walicheza mpira mwingi sana, lakini wakatolewa na kutupwa huku chini kwenye Kombe la Shirikisho.

Wote tulibaki kuwasifu kwamba waliwashika Waarabu hao tukasahau ni nani aliyepata faida.

Mechi yao dhidi ya Mo Bejaia Yanga walicheza mpira mwingi ugenini tukawasifu sana, lakini mwisho wa dakika 90 wapinzani wao wakaondoka na ushindi wa bao 1-0 sisi tukabakia na pasi zetu zenyewe wakaondoka na pointi tatu.

Walipokutana na TP Mazembe wakafungwa bao 1-0 tukaendelea kujisifu kwamba Mazembe wamekwisha,  kwani Yanga waliwashika sana. Bado tukabakia na sifa zetu za kampa kampa tena wenzetu wakaondoka na pointi tatu. Yanga sasa tafuteni pointi tatu.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU