Majibu ya Mourinho kuhusu Man Utd

Majibu ya Mourinho kuhusu Man Utd

370
0
KUSHIRIKI

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

KWA mara ya kwanza, kocha Jose Mourinho ‘Special One’, alizungumza na waandishi wa habari juu ya kibarua chake kipya cha kuinoa klabu ya Manchester United.

Ikumbukwe kuwa kocha huyo raia wa Ureno alikabidhiwa mikoba hiyo mwezi uliopita lakini kwa kipindi chote hicho hakuwahi kufanya mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia suala hilo.

Je, ni maswali gani ambayo Mourinho alikumbana nayo kutoka kwa waandishi wa habari wa mjini Manchester? Tiririka nayo.

 

  1. Bado unajiita Special One, ‘Happy One’ au umekuja na jina jingine?

“Sijui, kweli. Ujio wangu wa sasa hapa England ni tofauti na ilivyokuwa miaka miwili iliyopita. Nilifukuzwa Chelsea na nilibaki hapa (England), mashindano ni yale yale na sura ni zile zile, hakuna kilichobadilika. Zaidi ni kuwa kwenye klabu ambayo ni ngumu kuielezea, hakuna maneno ambayo naweza kuyatumia kuzungumzia klabu hii,” alisema kocha huyo.

 

  1. Umekuja kushindana au kushinda?

“Inategemea jinsi ulivyojiandaa kukabiliana na ushindani utakaokutana nao. Sijawahi kutumia maneno kama kilevi kwa wapinzani wangu. Sijawahi kutumia falsafa kama silaha yangu. Sijawahi kujaribu kufanya hivyo.”

“Nataka kushinda kila mechi, nataka kucheza vizuri, nataka kuchezesha makinda, nataka kufunga mabao mengi, sitaki kuruhusu nyavu zangu kutingishwa.”

“Nataka mashabiki watuunge mkono mpaka dakika 10 za mwisho tutakazokuwa tunafukuzia matokeo au tutakapokuwa tunalinda goli. Nataka kila kitu. Huo ndio ukweli.”

 

  1. Utaendelea na mfumo wako wa ‘butua butua’?

“Nataka kuwa kama awali na nilijua wazi kuwa miongoni mwenu mngekuja na maswali juu ya mfumo huu na naamini kuwa unaweza kushinda mechi nyingi bila ya kucheza vizuri lakini huwezi kutwaa taji bila ya kucheza vizuri,” alisema.

“Kucheza vizuri maana yake nini? Kucheza vizuri ni kufunga mabao mengi kuliko mpinzani wako, kuruhusu mabao machache, ni kuwafanya mashabiki wako wafurahi.”

“Ni kuwafanya mashabiki wafurahi kwa sababu timu inashinda. Hivyo, tunataka kufanikisha vyote kwa muda mmoja. Kwangu, ni mfumo wa ‘kufosi’. Nataka kushinda kila kitu.”

 

  1. Nini ambacho ukikiangalia msimu uliopita kinakupa jeuri ya kutamba England?

“Kuna baadhi ya makocha ambao walichukua taji lao la mwisho miaka 10 iliyopita. Wengine wameshasahau siku waliyopata ubingwa huo. Kwa mara ya mwisho kuchukua ubingwa ilikuwa mwaka mmoja uliopita, si miaka 10 au 15 iliyopita, hivyo kuna mengi ya kuthibitisha ubora wangu,” alisema.

 

  1. Unajisikiaje kukutana tena na Pep Guardiola?

“Nachukia kumzungumzia kocha mmoja, klabu moja au adui mmoja, sidhani kama ni sahihi. Ni timu moja dhidi ya wapinzani wengi kama mbio za farasi, ni kama nilivyokuwa Hispania au Italia. Timu tatu zilikuwa zikiwania ubingwa, hapo aina ya falsafa inachangia,” alidai Mourinho.

 

  1. Hauna kawaida ya kukuza makinda. Ni sahihi kufanya hivyo?

“Sina muda wa kujibu hilo. Kujibu swali hilo itachukua dakika 10. Nilijua swali hilo lingefuata. Mnajua ni vijana wangapi nimewatoa ‘academy’ na kupelekwa vikosi vya kwanza? 49? Unataka kujua walipo sasa?

Naweza kukwambia kuhusu hilo. Niliibua vipaji 49. Kuna sababu zinazoweza kukufanya ugeukie vijana, kwanza ni kukosa wachezaji kutokana na majeruhi.

“Sababu ya pili ni pale unapocheza mechi ambazo si muhimu, hapo ni rahisi kuwapa nafasi,” alisema Mourinho.

“Baadhi ni mastaa wakubwa, wameshinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, wanapata namba kwenye vikosi vyao vya timuy za taifa, wachezaji 49 ni wengi.

“Hivyo, uongo ukizungumzwa sana huonekana ukweli, lakini ukweli utabaki pele pale kuwa nimeibua vipaji 49. Kama mnataka majina yao nitawatajia.”

 

  1. Kwanini uliamua kumpotezea Giggs?

“Kuhusu Ryan, acha nimalize. Huwa siingilii yasiyonihusu. Si jukumu langu juu ya Ryan (Giggs) kutokuwepo klabuni. Kazi ambayo aliitaka ndiyo niliyopewa mimi. Alitaka kuwa kocha mkuu wa Manchester United na uongozi ulinikabidhi mimi kazi hiyo.

“Ni kama  mwaka 2000, niliamua kuwa kocha. Wengi tulianza kama makocha wasaidizi, tena kwa miaka mingi. Hivyo, unapozungumzia kuhusu mimi kumpa kibarua, alitakiwa kuhitaji hilo. Klabu ilitaka kumbakisha hapa.

“Ni kama ilivyowahi kunitokea pale Barcelona mwaka 2000, nilikuwa na mkataba wa miaka miwili. Haikuwa rahisi kuendelea kubaki. Kwa Ryan (Giggs), si rahisi kutoka kuwa msaidizi hadi kocha mkuu, alitakiwa kuiacha Man United aliyodumu nayo kwa miaka 29.”

“Alikuwa shujaa, mpole, namtakia kila la kheri na akiwa atataka kurejea (Old Trafford) nikiwepo sitamkatalia na ikiwa atakabidhiwa benchi la ufundi, basi litakuwa ni jambo zuri kwa kile anachokitaka.”

 

  1. Ulipata ushauri wowote kutoka kwa Sir Alex Ferguson?

“Ndiyo. Ushauri wa kwanza ni pale  aliponiletea mwavuli mazoezini ambapo mvua ilikuwa inanyesha. Ushauri mwingine ni kuniletea chupa ya ‘Wine’. Kwa sasa, tutakuwa tukikutana sasa.”

 

  1. Unazungumziaje kuhusu nafasi ya Rooney kikosini?

“Katika mchezo wa soka kuna kazi nyingi. Kuna majukumu mengi ndani ya uwanja. Kazi nzito kuliko zote ni kumpata mpachikaji mabao.

“Labda si straika, si mpachikaji bora, kucheza mita 50 kutoka langoni. Unaweza kuniambia pasi zake ni hatari, lakini hata mimi nina uwezo wa kupiga pasi bila presha.

“Kufunga bao ni kazi ngumu. Kwangu, atacheza namba 9 au 10, lakini si nafasi ya kiungo.”

 

10.Una mpango wa kuiacha Man United?

“Nimefika nilipopataka, kuwa klabuni hapa na katika nchi hii. Nasikitika kutoshiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Sifichi, naifukuzia rekodi ya Mabingwa Ulaya.

“Man United ni klabu ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na tunatakiwa kuhakikisha kwamba Julai 2017, badala ya kucheza Ligi ya Europa kisha hatua ya makundi, tunafika pale timu hii inapotakiwa kuwa, yaani Ligi ya Mabingwa Ulaya.”

Nataka kuifikia rekodi ya mkongwe Sir Alex (Ferguson) ya kucheza takribani michezo 130 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.”

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU