Tunatofautiana nao kuthamini riadha

Tunatofautiana nao kuthamini riadha

353
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU

ITATUCHUKUA muda kupata wanariadha aina ya Filbert Bayi na Suleiman Nyambui ambao miaka ya 1980 waliipeperusha vyema bendera ya taifa kwenye mashindano ya Olimpiki ambayo ni makubwa duniani.

Agosti 5 hadi 21 mwaka huu katika Jiji la Rio de Janeiro nchini Brazil, mataifa mbalimbali duniani yatajumuika kushiriki michuano ya Olimpiki ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne. Swali linabaki, je, tutaenda kushindana au kuwa wasindikizaji? Je, bado tutaendelea kuitwa watalii?

Mwaka 1980 kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika jijini Moscow nchini Urusi, Bayi na Nyambui walilitoa taifa kimasomaso ambapo kati ya wanariadha 41 walioliwakilisha taifa, ni hao wawili tu waliorudi na medali.

Nyambui alitwaa medali ya fedha baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye mbio za mita 5,000 huku Bayi naye pia akishinda medali ya fedha baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi.

Historia inaonyesha hii ndiyo ilikua mara ya kwanza na mwisho kwa Tanzania kutwaa medali katika mashindano ya Olimpiki. Tumekuwa tukijaribu kila mara bila mafanikio kiasi cha wanariadha wetu kupachikwa jina la watalii.

Kushindwa kufanya vyema kwenye mashindano makubwa kama vile Olimpiki na kupelekea idadi ndogo ya washiriki imesababisha tuchague wanariadha wa mataifa mengine kuwashangilia kwa mfano Usain Bolt wa Jamaica anayekimbia mbio za mita 100 au Mwingereza mwenye asili ya Somalia, Mo Farah, anayekimbia mbio za mita 10,000 na 5,000 au hata pia bingwa wa dunia mita 800, David Rudisha wa Kenya.

Tanzania tumepanga kupeleka wanariadha wanne kwenye mashindano ya Olimpiki mwezi ujao ikiwa ni idadi ndogo ukilinganisha na majirani zetu Kenya ambao watapeleka wanariadha 48. Wanariadha wote wanne watashiriki mbio za kilomita 42 maarufu kama marathon.

Kati ya wanariadha hao wanne, moja ni wa kike ambaye kufuzu kwake hakukutambulika mara moja na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT). Taarifa za muda bora alioweka zilianza kuzagaa kwenye mitandao na hakuna hata kiongozi mmoja wa RT aliweza kuthibitisha hilo.

Mwanariadha huyo Sarah Ramadhani ambaye hivi karibuni alimaliza kutumikia kifungo baada ya kugundulika kutumia dawa za kuongeza nguvu michezoni, aliorodheshwa miongoni mwa wanariadha kutoka Tanzania waliofuzu kushiriki Olimpiki.

Wengine ambao waliweka muda bora katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ni Alphonce Felix, Fabian Joseph na Saidi Makula. Juhudi za RT kuona idadi hiyo kuongezeka ziligonga mwamba baada ya wanariadha Watanzania kushindwa kufanya vyema katika mashindano ya riadha Afrika yaliyofanyika hivi karibuni nchini Afrika Kusini.

Inasikitisha licha ya idadi ndogo ya wanariadha tunaowapeleka Brazil, baadhi yao wamekuwa wakinung’unika na hali ya kambi yao huku RT wakisisitiza wanapata huduma stahiki. Je, nani msema kweli? Anayeenda kushiriki au anayeandaa washiriki?

Tangu mafanikio waliyoleta Bayi na Nyambui, bado tumeshindwa kujifunza au kutafuta mbinu mbadala wanariadha wetu kuonekana ni washindani na si wasindikizaji. Hebu fikiria, sisi tunapeleka wanariadha wanne huku wenzetu Kenya wanapeleka 48!

Hata namna ya kupata wawakilishi wa timu ya taifa tunatofautiana. Kwanini tusiige mfano wa Kenya? Majirani zetu waliandaa mashindano ya siku mbili kwenye Uwanja wa Kipchoge Kieno mjini Eldoret kutafuta wanariadha watakaoliwakilisha taifa lao kwenye mashindano ya Olimpiki.

Kila mwanariadha mwenye jina kubwa alitua Eldoret, mji unaotambulika kama ‘Mji wa Mabingwa’, huku kilele cha mashindano hayo kikishuhudia Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, akiwa mgeni rasmi. Mashindano hayo ya mchujo ya siku mbili yalitafsiriwa na umati mkubwa uliojitokeza kama ‘Olimpiki ndogo’.

Makampuni makubwa nchini Kenya yalijitokeza kudhamini mashindano hayo na hii inatokana na imani kubwa waliyonayo katika riadha. Huku ndipo tunapaswa na sisi kuelekea. Riadha ina historia kubwa Tanzania na wanaoiongoza riadha nchini ni watu makini wanaoupenda mchezo huo.

RT, Serikali, makampuni na wadau wa riadha hawana budi kukaa meza moja na kuandaa mpango mkakati kuhakikisha Olimpiki ya mwaka 2020 itakayofanyika jijini Tokyo, Japan tunapeleka idadi kubwa ya wanariadha lakini kikubwa zaidi tunavuna medali nyingi.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU