Ureno ilivyochukua ubingwa kwa ‘style’ ya Ugiriki

Ureno ilivyochukua ubingwa kwa ‘style’ ya Ugiriki

381
0
KUSHIRIKI

PARIS, Ufaransa

HISTORIA imejirudia! Kile kilichoitokea Ureno kwenye fainali za Mataifa ya Ulaya za mwaka 2004, ndicho kilichojirudia kwa Ufaransa mwaka huu.

Kabla ya kuanza kwa michuano hiyo iliyofanyika nchini Ureno, hakuna aliyetarajia kuwaona Ugiriki wakifika fainali na kunyakua taji hilo.

Kinyume na matarajio ya wengi, kikosi hicho kilinyakua taji hilo baada ya kuwanyuka wenyeji Ureno bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa mjini Lisbon.

Katika michuano hiyo, Ugiriki ilianza kwa mwendo wa kusuasua kama ilivyokuwa Ureno mwaka huu nchini Ufaransa.

Wababe hao walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ufaransa na kisha kuibuka na ushindi kama huo katika michezo miwili iliyofuata dhidi ya Jamhuri ya Czech na Ureno.

Rekodi ya Kocha Otto Rehhagal ambaye ndiye aliyekuwa akikiongoza kikosi hicho kwenye fainali hizo, itaendelea kukumbukwa katika historia ya michuano hiyo kutokana na mfumo wake wa kupaki basi.

Akiwa na umri wa miaka 65, Rehhagal ndiye aliyekuwa kocha mwenye umri mkubwa kuliko wote kwenye mashindano hayo.

Mfumo huo wakupaki basi huku wakitegemea mashambulizi ya kushtukiza ndio uliowaliza Wareno wakiwa kwenye ardhi ya nyumbani.

Wakiwa na mkongwe, Traianos Dellas, katika safu ya ulinzi, walifanikisha hilo huku staili yao hiyo iliyowafanya kuibuka na ushindi mwembamba ikibaki gumzo.

Katika mchezo wa fainali, Ugiriki iliwaacha kinywa wazi Wareno kwa bao la mwanzoni mwa kipindi cha pili lililopachikwa na Angelos Charisteas.

Takwimu zinaonyesha kuwa licha ya Ugiriki kushinda mchezo huo, ilimiliki mpira kwa asilimia 42 pekee huku Ureno wakikaa na mpira kwa asilimia 58.

“Wameshinda, huwezi kuwanyima sifa hiyo, lakini kama utaniuliza kama (mchezo wa fainali) ulikuwa mzuri nitakwambia hapana,” alisema staa Luis Figo alipokuwa akiizungumzia Ugiriki.

“Watu wengi watakwambia hivyo. Sidhani kama ni timu nzuri lakini walijipanga na wameshinda.”

Kama ilivyokuwa mwaka 2004, katika fainali za mwaka huu Ureno haikuonekana kuwa na uhakika wa kuchukua taji zaidi ya kuzisindikiza Ujerumani, Hispania na Italia.

Cristiano Ronaldo ndiye mchezaji pekee aliyebaki kwenye kikosi cha sasa cha Ureno baada ya kupotea kwa kizazi cha dhahabu kilichokuwa na akina Luis Figo, Nuno Gomes na Rui Costa.

Mpaka inafika fainali, licha ya kucheza mechi sita, Ureno ilikuwa imeshinda mchezo mmoja pekee katika dakika 90.

Katika hatua ya makundi, ilitoa sare michezo mitatu dhidi ya Iceland, Austria na Hungary na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye Kundi E.

Katika mchezo uliofuata, ikaibuka na ushindi wa dakika za majeruhi wa bao 1-0 dhidi ya Croatia kabla ya kushinda kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Poland na kisha kuibukia na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wales.

Kocha Fernando Santos amekuwa akimtumia Ronaldo kama straika huku Nani akimtumia zaidi katika mashambulizi ya pembeni.

Kabla ya kurejea Ureno miaka miwili iliyopita, Santos alikuwa akifundisha soka nchini Ugiriki na wakati ‘mabaharia’ hao walipochukua ubingwa mwaka 2004, alikuwa akikinoa kikosi cha AEK Athens.

Hivyo, wachambuzi wa soka wanaamini kuwa Santos ana aina ya uchezaji inayofanana na ile ya  Ugiriki.

Mwaka 2004, wachambuzi wasoka waliamini kuwa Ureno ilistahili kuifunga Ugiriki katika mchezo wa fainali na katika michuano ya mwaka huu Ufaransa ilikuwa bora mbele ya Ureno.

Kwa mchezaji mmoja mmoja, wachambuzi wamedai kuwa Ufaransa iliwazidi Ureno katika kila idara. Antoine Griezmann ambaye alifunga jumla ya mabao sita katika michuano hiyo, Dmitri Payet na Paul Pogba katika safu ya kiungo, kwa pamoja walitosha kuimaliza Ureno.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU