KWA MOURINHO MBONA AKINA RASHFORD WATACHEZA TU

KWA MOURINHO MBONA AKINA RASHFORD WATACHEZA TU

221
0
KUSHIRIKI

MAREGES NYAMAKA NA MITANDAO

AWALI kulikuwa na wasiwasi mkubwa kuhofia kufika mwisho wa falsafa ya Manchester United, baada tu ya ujio wa kocha mpya, Jose Mourinho.

Lilikuwa ni gumzo kubwa kona mbalimbali ya dunia, wengi wakihoji ni jinsi gani Mourinho ataendana na falsafa ya United, ikiwemo uendelezaji wa vipaji vya wachezaji vijana kama akina Marcus Rashford na Jesse Lingard.

Pia kuwapandisha wachezaji makinda kutoka  academy kucheza timu ya wakubwa na kuwatengeneza  kuwa wachezaji mahiri na tegemeo baadaye katika timu.

Lakini hivi sasa hiyo hofu huenda ikawa imetoweka  baada ya Mourinho mwenyewe  kuulizwa suala hilo na waandishi wa habari kwenye mkutano wake wa kwanza.

Ni vipi ataweza kuendana na falsafa ya timu hiyo huku yeye akisifika zaidi kutumia asilimia 95 ya wachezaji wenye majina kama historia inavyoonyesha.

Akijibu swali hilo alisema ‘mwongo akilirudia mara kadhaa hilo neno najua ukweli wa jambo utabaki ukweli daima, mkitaka majina  ya wachezaji niliofanya nao kazi katika klabu zote nilizofundisha  nitawapa.”

Baada ya kusema hivyo, Mreno huyo  alitoa karatasi mfukoni na kuwaonyesha waandishi wa habari idadi ya wachezaji 49 aliowaibua. Hawa ni baadhi ya nyota makinda waliopita mikononi mwa Mourinho.

Benfica

  1. Diogo Luis (2000)

Mshambuliaji  huyo raia wa Ureno alikua kwenye orodha ya wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Jose Mourinho  katika klabu ya Benifica kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 20. Hivi sasa Luis ni mshauri wa  fedha katika  moja ya benki kubwa.

Geraldo Alves (2000)

Baada ya kupewa nafasi  kucheza mechi yake ya kwanza  siku chache baadaye alianza kung’ara kwenye michuano  mikubwa Ulaya ikiwemo Europa. Uwezo wake ukamwezesha kusajiliwa na baadhi ya klabu kama vile AEK Athens, Steaua Bucuresi na Petrolul ya Romania.

Porto

Ricardo Costa (2002)

Ricardo alitolewa timu B na kupandishwa timu ya wakubwa moja kwa moja  ambapo aliendeleza makali kwa kucheza  soka la kuvutia. Klabu nyingine alizozichezea Wolfsburg na Valancia, kwa sasa anakipiga  katika timu ya Granada ya Hispania.

Joca (2002)

Kiungo mkabaji ambaye hakudumu sana kikosi cha kwanza, ndani ya miaka 12 amechezea klabu 13.

Hugo Luz (2003)

Huyu ni nyota mwingine wa Porto aliyefanikiwa kuicheza klabu hiyo akiwa na umri mdogo, vile vile  aliweza kukipiga klabu ndogo zaidi ya tano kabla ya kutundika daruga mwaka jana.

Elias (2003)

Kiungo wa Brazil aliyeichezea Porto mchezo mmoja pekee na kisha kupata uhamisho wa kuchezea klabu mbalimbali za hapo Ureno kabla ya kitimkia Bulgaria

Bruno Moraes (2003)

Aliwasili mahali hapo akitokea kwao  Brazil kakita klabu ya Santos  na kufanikiwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza na akishuka dimbani mara 17 kabla ya kutolewa kwa mkopo Vitoria Setubal.

Hugo Almeida (2003)

Hugo alipata bahati ya kuingia kikosi cha kwanza cha Jose Mourinho 2003, inaelezwa Almeida alikuwa kati ya washambuliaji wenye nguvu  kupambana, tangu hapo alipata mafanikio kiasi flani ikiwemo kufanya vizuri kwenye timu ya taifa ya Ureno, katika michezo 57 alizocheza aliingia wavuni mara 19.

Anthony Grant (2005)

Jicho la Mourinho pia lilimuona Grant ana uwezo wa kuisaidia timu na kumpa nafasi kwenye kikosi chake, kilichofuatia kwa Grant ni kucheza kwa mkopo mfululizo klabu mbalimbali kwa nyakati tofauti tofauti.

Inter Milan

Davide Santon (2008)

Santon alikuwa ni moja ya vijana wa mwanzo kabisa kupewa kipaumbele na Mourinho, ingawa baadaye majeraha ya mara kwa mara yamemfanya kukosekana uwanjani  kuonyesha kiwango chake hata alipohamia Newcastle United hali ilikuwa hiyo hiyo.

Rene Krhin (2009)

Winga raia wa Slovenian, pia ni moja ya makinda waliopata kucheza kwenye kikosi chini ya Mourinho viunga vya San Siro 2009 na mwaka uliofuata alisajiliwa na Bologna, hivi sasa anakipiga  Granada ya Hispania.

Alen Stevanovic (2010)

Mserbia huyu alidumu kwa msimu mmoja Inter Milan pekee na baadaye akatimkia Torino  alipocheza miaka mitano, kabla ya kupata uhamisho wa kwenda klabu ya Partizan.

Real Madrid

Juan Carlos (2010)

Akiingia uwanjani kutokea benchi kuchukua  nafasi  ya Angel Di Maria, mchezo wa La Liga dhidi ya  Deportivo la Coruna  ndiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza Bernabeu. Aliichezea pia Braga kwa mkopo.

Pablo Sarabia (2010)

Muda mwingi alikuwa akionekana benchi  hata michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya  ilikuwa hivyo, kiungo huyo mshambuliaji  baadaye akajiunga na Getafe akidumu kwa misimu mitano, kwa sasa yupo Sevilaa.

Alvaro Morata (2010)

Moja ya washambuliaji anayeng’ara  barani  Ulaya akibebwa zaidi kwa kutupia mabao  ya kutosha wavuni  akiwa na  timu yake ya  Juventus akitokea  Raal Madrid ambao wamepambana  kumrejasha  klabuni hapo.

Jese (2011)

Alikomaa kwenye academy ya Real Madrid kwa muda wa miaka mitano hadi alipopandishwa timu ya wakubwa na  Mourinho 2011, mpaka sasa anaendelea kutesa  chini ya kocha Zinedine Zidane.

Jose Rodriguez (2012)

Rodriguez inaelezwa kama moja ya viungo shupavu na wenye nguvu hasa, ingawa muda mwingi alicheza timu B, Mhisipania huyo alibahatika kupandishwa timu A 2014-15 lakini msimu huo huo akatolewa kwa mkopo Deportivo La Coruna. Kwa sasa anawasha moto katika klabu ya Mainz.

Casemiro (2013)

Amekuwa  miongoni  mwa nyota chaguo la kwanza kwa kocha wa sasa wa Real Madrid, Zinedine Zidane, mara kadhaa amekuwa akianza kikosi cha kwanza ikiwemo mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Mei mwaka  huu dhidi ya Atletico Madrid  na Real kuibuka bingwa.

Fabinho (2013)

Ni beki wa kushoto aliyepitia  Bernabeu kwa mkopo  kabla ya kwenda Monaco inayocheza Ligi Kuu ya Ufaransa  maarufu kama League 1. Mwaka jana pia alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kilichoshiriki michuano ya Copa America iliyofanyika nchini Chile.

Diego Llorente (2013)

Llorente (22) anayecheza beki ya kati  kutokana na upana wa  kikosi cha Real Madrid uhakika wa kupata namba  ulikuwa finyu kwake, Real Madrid wakaamua  kumpeleka Rayo Vallecano kwa mkopo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU