Payet akata mzizi wa fitina West Ham

Payet akata mzizi wa fitina West Ham

377
0
KUSHIRIKI
Dimitri Payet

LONDON, England

STAA wa klabu ya West Ham, Dimitri Payet, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kusema kwamba ataendelea kukipiga msimu ujao na ana furaha atakuwa mmoja wa wachezaji watakaozindua uwanja mpya wa Olimpiki.

Payet anafukuziwa na miamba ya soka baada ya kuonesha kiwango cha hali ya juu msimu uliopita wa Ligi Kuu England pamoja na timu ya taifa ya Ufaransa, ambapo wamiliki wa West Ham, David Gold na David Sullivan, waliweka wazi kuwa mchezaji wao huyo hawezi kutoka bila kitita cha pauni milioni 50 hadi 100.

Lakini Payet (29), amempa ahueni kocha wake, Slaven Bilic pamoja na mashabiki kwa ujumla baada ya kuweka wazi kuwa ana furaha kucheza katika klabu hiyo ya Ligi Kuu England na hana mpango wa kutimka.

“Nimezisikia klabu zote zinazonihitaji na ninafarijika,” alisema Payet.

“Lakini ninaipenda West Ham. Tulikuwa na msimu mzuri na nina hamu ya kukipiga kwenye dimba la Olimpiki.

“Ninabaki West Ham, kuna asilimia 100 za jambo hilo kutokea, ninaipenda hii klabu. Hilo ndilo ninaloweza kuwaambia mashabiki wetu.”

Payet alijiunga na West Ham msimu uliopita akitokea Marseille na ameifungia klabu hiyo jumla ya mabao tisa katika michezo 30 ya ligi na alijizolea umaarufu miongoni mwa mashabiki wa wagonga nyundo hao waliocheza kwa mara ya mwisho katika uwanja wao wa Upton Park msimu uliopita.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU