Gabo anavyobadilisha mwelekeo wa filamu Bongo

Gabo anavyobadilisha mwelekeo wa filamu Bongo

835
0
KUSHIRIKI

NA CHRISTOPHER MSEKENA,

SI jambo rahisi kupata mafanikio, ni lazima utakutana na changamoto lukuki ambazo ukishindwa kuzikabili basi utaendelea kubaki pale pale na kushuhudia wenzako wakipiga hatua ndefu za mafanikio kwenye nyanja mbalimbali.

Huku kwenye sanaa nako si mchezo. Watu wanakutana na vikwazo ambavyo kama una roho nyepesi huwezi kuvuka na kufanikiwa kuwa maarufu kupitia muziki, filamu au sanaa nyingine ukitaka ujue ukweli huu tafuta historia za mastaa mbalimbali wanaofanya vyema wakati huu kuna kitu utajifunza.

BINGWA limebisha hodi mpaka Magomeni Mkumi jijini Dar es Salaam ndani ya ofisi ya mshindi wa tuzo ya ZIFF katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume kupitia filamu ya Safari ya Gwalu, Salim Ahmed maarufu kama Gabo Zigamba. Karibu ufuatilie mazungumzo yetu.

BINGWA: Gabo Zigamba ni nani ndani ya filamu za Tanzania?

Gabo: Nilianza kuigiza muda mrefu tangu mwaka 2006 kwenye vikundi mbalimbali huku nikiwa na hamu ya kuwa maarufu na kutimiza lengo langu la kupaza sauti ya wanyonge. Filamu yangu ya kwanza iliitwa Olopong chini ya Al Riyamy na hapo ndiyo nikaanza kufahamika.

BINGWA: Ilikuwaje mkafahamiana na marehemu Sajuki?

Gabo: Baada ya kufanya filamu inayoitwa 007 Boys na The Pain ndiyo nikapata shavu la kujiunga na Sajuki kupitia kampuni yake ya Wajey Film na kucheza filamu kama Mchanga na Keni, The Killer na 007 Days.

BINGWA: Jina lako halisi ni Salim Ahmed, ilikuwaje ukaitwa Gabo Zigamba, jina linalolifunika jina lako halisi?

Gabo: Gabo Zigamba ni muunganiko wa jina la nchi ya wanyonge na ndogo ya Gabon na ng’ombe anayepiga kazi katika kabila la Kisukuma anayeitwa Zigamba kwa hiyo nikaunganisha nikapata hilo jina.

BINGWA: Umekuwa mstari wa mbele katika kuipigania lugha ya Kiswahili, nini asili ya kuitamka lugha hii kiufasaha?

Gabo: Mimi nadhani ni kipawa tu cha Mungu na nimeishi ukanda huu wa Pwani kwa muda mrefu, kilichonifanya niifahamu lugha ya Kiswahili. Si kutamka tu mimi pia huwa nashiriki katika kusaidia watunzi wa mashairi.

BINGWA: Umekuwa ukiendesha na kutangaza kipindi cha Bondeni, wazo la kuanzisha kipindi kile lilikuwa ni nini?

Gabo: Ni ngumu kuwafikia wadau wakubwa wa kazi zetu za filamu kama umekaa tu nchini kwako. Bondeni ni kipindi ambacho kinanikutanisha na wadau ana kwa ana kwa kuwa kinawahusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi kama vile Afrika Kusini, Kenya, Uganda na nchi nyingine duniani kwa hiyo kwangu mimi ni wigo mpana wa kujitangaza.

BINGWA: Ushindi wa tuzo ya ZIFF una maana gani kwako?

Gabo: Ni heshima kubwa mno kwangu na huu ndio muda mwafaka wa mimi kuwaonyesha mashabiki wangu kuwa ushindi nilioupata nilikuwa na stahili na sina njia nyingine ya kuwaonyesha zaidi ya kufanya kazi nzuri.

Gabo: Kuna kazi ipi mpya ambayo inaweza kuizidi ile filamu ya Safari ya Gwalu?

BINGWA: Tanzania ina matatizo mengi yanayowakumba wanyonge na hawana sehemu ya kusemea. Hivi sasa nasubiri muda ufike niachie filamu inayoitwa Siyabonga. Humo watu watamuona Gabo mwingine kabisa na filamu hiyo inahusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji inayoendelea nchini.

BINGWA: Toka umeanza kuzalisha filamu zako umekuwa ukitoa sinema zenye mlengo mwingine kabisa tofauti na za zile za mapenzi zilizooeleka, kwanini unafanya hivyo?

Gabo: Ukitaka kufanya mapinduzi ni lazima uangalie adui yako anafanya nini na wewe ufanye yako. Ukiangalia Safari ya Gwalu hata hii mpya itakayotoka utagundua mimi nafanya harakati zaidi, nataka niipeleke tasnia ya filamu sehemu nyingine kabisa ili niwe na utambulisho wangu utakaonitofautisha na wasanii wengine.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU