NGAO YA JAMII………..Yanga vs Azam FC ni zaidi ya mechi

NGAO YA JAMII………..Yanga vs Azam FC ni zaidi ya mechi

1589
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

BAADA ya kusubiriwa kwa shauku kubwa, kesho pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/17 litafunguliwa kwa kupigwa pambano la Ngao ya Jamii baina ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga dhidi ya Azam FC.

Kipute hicho kinatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na maandalizi ya uhakika yaliyofanywa na kila timu.

Yanga itaingia uwanjani ikiwa bado ya moto kwani tangu ligi ilipomalizika wachezaji wake hawakuwahi kupumzika, hatua hiyo ilisababishwa na ushiriki wake katika michuano ya Kombe la Shirikisho ambapo wikiendi iliyopita iliichapa Mo Bejaia bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam kwa upande mwingine kikosi chake kimekuwa kikijifua kwa nguvu kama maandalizi yale ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.

MABENCHI YA UFUNDI

Kuelekea mchezo huo, Yanga itaingia uwanjani kesho ikiwa haina mabadiliko kwenye benchi lake.

Mdachi Hans Van Der Pluijm, atakuwa Kocha Mkuu wa Yanga, huku msaidizi wake akiwa ni Juma Mwambusi.

Hans anapendelea soka la pasi fupi fupi na kushambulia kwa haraka kwa kutumia mawinga.

Mdachi huyo ni muumini wa mfumo wa 4:4:2, wakati Azam wakiwa na mabadiliko kwenye benchi lao la ufundi litakalokuwa chini ya Kocha Mkuu Mhispania, Zeben Hernandez.

Mhispania huyo alichukua jukumu hilo baada ya mtangulizi wake Mwingereza, Stewart Hall, kuachia ngazi baada ya Ligi Kuu msimu uliopita kumalizika.

Azam ikiwa chini ya benchi jipya la ufundi itatumia mfumo wa 4:3:3 au 4:4:2.

Mfumo huo utaifanya Azam kujaza viungo wengi katika eneo la katikati, huku ikiwa na mastraika wachache ambao wanashambulia na kukaba.

NYOTA WA KUCHUNGWA

Kwa upande wa Yanga, straika Mzimbabwe, Donald Ngoma na mwenzake raia wa Burundi, Amissi Tambwe, watapewa jukumu na Pluijm la kuhakikisha Azam inaumia kwenye mchezo huo.

Tambwe ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita baada ya kukwamisha wavuni mabao 21 baada ya ushirikiano mzuri na Ngoma.

Pia kuna viungo; Deus Kaseke, Juma Mahadhi, Juma Abdul na  beki Vicent Bosou  hawa ni wachezaji mahiri kabisa katika kikosi cha Yanga.

Azam nayo itakuwa na fowadi wake matata, John Bocco, ingawa kuna wakali wengine kama  Daniel Amoah, Gadiel Michael, Ismail Gombo, Idi Shaaban na Abdalah Msoud ambao wana mchango mkubwa kwenye kikosi cha timu hiyo.

WAKALI WAPYA

Yanga imesajili wachezaji wanne wapya ambao ni Obrey Chirwa, Mahadhi, Vicente Andrew, Benno Kakolanya na Hassan Kessy.

Hata hivyo, hakuna uwezekano wa Kessy kucheza mechi hiyo kwakuwa klabu yake ya zamani ya Simba imeweka ngumu kutoa barua ya kumwidhinisha.

Azam kwa upande wake imesajili wachezaji wawili wa  kigeni na kuwapandisha wengine watatu kutoka katika academi yao.

Nyota wapya wa kigeni waliotua Azam ni pamoja na Bruce Kangwa kutoka Zimbabwe na  Daniel Amoah kutoka  Ghana, wakati wachezaji wazawa ni Ismail Gambo, Idi Shaaban na Abdalah Msoud.

Nyota hao wameonekana kuongeza kitu kipya katika kikosi cha Azam hivyo wanaweza kuifanya mechi ya kesho kuwa tamu zaidi.

HISTORIA YAO NGAO YA JAMII

Yanga na Azam zimeshakutana mara tatu katika mechi za Ngao ya Jamii.

Katika kukutana huko, Yanga ndiyo imekuwa na bahati nayo kwa kuibuka na ushindi katika mechi zote.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ilikuwa ni msimu wa 2015/16 ambapo  Yanga ilishinda kwa penalti 8-7 kufuatia matokeo ya suluhu ya ndani ya dakika 90.

MATOKEO NA WAFUNGAJI

2012/13-Yanga 1-0 (mfungaji Salum Telela)

2013/14-Yanga 3-0 Azam FC (wafungaji Genilson Santana ‘Jaja’ aliyetupia mawili na Simon Msuva)

2014/15-(Penalti Yanga 8-7 Azam) baada ya dk 90 kupata suluhu (wapigaji, Yanga ni Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Amissi Tambwe, Andrey Coutinho, Geofrey Mwashiuya, Thaban Kamusoko, Kelvin Yondani na Mbuyu Twite huku Azam FC zikitiwa nyavuni na Kipre Tchetche, John Bocco, Agrey Morris, Mugiraneza Jean Baptiste, Erasto Nyoni, Himid Mao na Shomari Kapombe).

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU