Wivu ni kipimo cha mapenzi?

Wivu ni kipimo cha mapenzi?

799
0
KUSHIRIKI

NA MICHAEL MAURUS

KARIBU ndugu msomaji katika safu hii ya mahusiano ambayo hukupa fursa ya kufahamu na kujadiliana mambo mbalimbali ya mahusiano ya kimapenzi.

Awali ya yote, nitoe shukrani zangu za dhati kwa wote ambao wamekuwa wakipiga simu au kutuma sms kupongeza au kuchangia juu ya mada mbalimbali katika safu hii.

Baada ya salamu hizo, tugeukie mada ya leo ambayo imetokana na matoleo ya wiki tatu zilizopita juu ya ni vipi unaweza kumfahamu mwenza mwenye mapenzi ya dhati.

Kwa kuwa wengi wameutaja wivu kama njia mojawapo ya kumpima mpenzi, nimeona tulijadili neno wivu na nafasi yake katika mahusiano ya kimapenzi.

Wapo wanaoamini kuwa wivu ni kama ‘suna’ katika mapenzi katika kuonyesha jinsi mtu anavyompenda mwenzake, huku wengine wakidai wivu ni ulimbukeni.

Kuna siku katika pitapita zangu huko mitaani, jijini Dar es Salaam, nilikutana na wasichana wanaoonekana kuwa wanafunzi wa chuo ambapo mmoja wao alikuwa akijibizana na mpenzi wake kupitia simu.

Katika mabishano hayo, ilielekea yule msichana hakuwa amemuaga mpenzi wake kuwa anaelekea wapi, hali iliyoonekana kumkera mwenzake huyo na kugombana kupitia simu.

“We nawe umezidi kuwa na wivu, mtu akitoka tu unafikiria amekwenda kwa mwanaume!…mbona wewe huwa huniagi safari zako, lakini mimi sikuulizi…mi si mtoto bwana, nina akili zangu…”

Hata kabla ya mpenzi wake kumaliza kuongea, msichana yule alikata simu na kuanza kumponda mwenza wake huyo akimshutumu kwa kuwa na wivu uliopitiliza kiasi cha kumkosesha raha.

Kati ya wasichana wale, ni mmoja tu aliyesapoti kuwa wivu ni kitu muhimu mno katika mahusiano ya kimapenzi kwani humtambulisha mhusika ni vipi anampenda mwenzake.

Waliobaki walikuwa wakimponda ‘shemeji’ yao wakisema amekuwa akimwonea wivu rafiki yao kwa kuwa yeye si msafi.

“Ukimwona mpenzi wako anakuonea sana wivu, ujue huyo hajatulia, anadhani anavyofanya yeye hata wewe unafanya hivyo hivyo, jipime shoga,” hayo yalikuwa ni maneno ya mmoja wa wasichana wale.

Majadiliano yale yalinivutia mno na ndiyo yaliyoniwezesha kupata mada hii kuhusiana na suala zima la wivu katika mapenzi.

Wakati baadhi ya watu wakiamini kuwa wivu ni ishara ya upendo wa dhati, wapo wanaopingana na hilo wakidai kuwa hali hiyo inatokana na ulimbukeni wa mapenzi.

Kwa wanaoamini kuwa wivu ni ishara ya mapenzi ya dhati kwa wahusika, wanadai kuwa asiyemwonea mwenzake wivu, huyo hana mapenzi hata kidogo kwa mwenzi wake huyo.

Kwamba hupenda kuwa naye mara kwa mara ikiwamo kufahamu wapi aliko mpenzi wake na akifanya nini.

Kwa wale wasio na wivu, hata mpenzi wake awe mbali naye kwa mwezi mzima, kwake ni poa tu wakiamini kumwonea mpenzi wako wivu ni ulimbukeni wa mapenzi.

Hebu niwaachie ‘homework’ wasomaji wa BINGWA kujadili hili juu ya suala zima la wivu ambapo maoni yenu nitayachapisha katika toleo la Jumanne ijayo.

Tuma maoni yako juu ya suala zima la wivu kupitia namba ya simu 0713 556022 au ukurasa wa facebook wangu wa Michael Maurus au anuani pepe, michietz@yahoo.com.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU