Yanga wasipomwelewa Chirwa, nani atamwelewa?

Yanga wasipomwelewa Chirwa, nani atamwelewa?

1872
0
KUSHIRIKI

OBREY Chirwa haeleweki. Anatembea na sura zake mbili tofauti zilizobeba maswali mengi kuliko majibu. Nani wakuzielezea?

Yanga wamelamba dume au Yanga wameliwa? Mpaka sasa kila mtu amechagua kuelewa cha kwake.

Wanaosema ni bonge la straika, wanaomba apewe muda zaidi, wanaosema ni changa la macho, wamebaki na kilio cha milioni 200 za usajili. Lakini nani mwenye majibu kuhusu Chirwa?

Ni viongozi na benchi la ufundi la Yanga pekee wanaoweza kujibu maswali haya na kumaliza utata huu wa Obrey Chirwa. Kivipi?

Tuanze na hoja hizi, ni kweli Chirwa ni straika wa thamani ya Sh milioni 200? Kama ndio, ni nini kinachomweka mbali na nyavu za wapinzani mpaka leo hii?

Ndio, kwa sasa hakuna cha zaidi mashabiki watakachokihitaji kwa Chirwa zaidi ya mabao. Na hawafanyi hivi kwa makusudi, hiki ndicho walichoambiwa wakati klabu yao ilipotumia kiasi kikubwa cha fedha kumleta Chirwa Tanzania.

‘Tumesajili straika wa nguvu’ kama ndivyo, yuko wapi huyo straika? Ni Chirwa au kuna mwingine?

Ni dhambi kwao kusifia mbio zake, pasi zake na nguvu zake, hizo ni kazi za Mahadhi Juma na Simon Msuva, Chirwa anatakiwa afunge. Yako wapi mabao miguuni mwake?

Majibu ya swali hili yamefichwa nyuma ya majibu ya swali hili, linatakiwa kujibiwa na benchi la ufundi la Yanga.

Walimsajili Chirwa kwenye nafasi gani? Aje acheze kama straika wa kati au kiungo mshambuliaji? Likijibiwa hili kwa ufasaha bila shaka mzigo mzito ulio mabegani mwa Chirwa utaondoka.

Je, Yanga walimsajili Chirwa kama straika wa kati? Kama ndio, basi wamefeli.

Chirwa hana jicho la goli. Si ‘finisher’ wa thamani ya milioni 200, kwenye nafasi 5 alizokosa dhidi ya Mo Bejaia, Malimi Busungu angefunga mbili. Ukweli uko hivyo!

Chirwa hana ‘taiming’ nzuri ya umaliziaji na ni mzito wa kuamua pindi anapotakiwa kufanya maamuzi, sehemu ya kichwa atapiga na mguu, sehemu ya kufunga anatoa pasi.

Washambuliaji halisi wamezaliwa na uchu wa mabao ndani yao, wanapenda kufunga muda wote katika mazingira yoyote, Chirwa hana sifa hii.

Aina yake ya uchezaji haifanani na kile kilichosemwa wakati akisajiliwa, labda kama tulidanganywa au uongozi ulificha baadhi ya vitu vya kiufundi!

Chirwa si mshambuliaji, ila ana sifa zote za kuwa kiungo mshambuliaji. Ni mzuri akicheza kama namba 7, 11, 10 lakini si namba 9.

Sikushangaa alivyokuwa akitumia muda mwingi kumwekea mipira Kamusoko anapokuwa ndani ya boksi. Chirwa hajui kufunga ila anajua kutengeneza nafasi watu wafunge.

Ana kasi, nguvu na mwepesi wa kukokota mpira, ni kama alivyo Simon Msuva anapokuwa kwenye ubora wake, wamepishana kitu kimoja tu, Chirwa anajiamini sana anapokuwa na mpira miguuni mwake.

Kwenye mchezo dhidi ya Mo Bejaia, alitakiwa kucheza nyuma ya Amissi Tambwe na si mbele yake, lilikuwa kosa la kiufundi lililowanyima faida ya kupata mabao mengi kwenye uwanja wa nyumbani.

Nilimsikia kocha wa Mo Bejaia akimsifia Chirwa, amemtaja kama mtu aliyeisumbua sana safu yake ya ulinzi. Hakuna wakupinga hili, Chirwa alisumbua sana.

Lakini ukweli ambao kocha wa Mo Bejaia hakuusema ni namna Chirwa alivyokosa umakini kwenye umaliziaji, natamani angemuona Donald Ngoma katika nafasi zile.

Mwisho wa siku wenye kuujua ukweli ni Yanga wenyewe, kama walikwenda sokoni kumsajili kiungo mshambuliaji mwingine kwenye timu yao, basi pale kwa Chirwa wamelamba dume.

Ila kama waliweka mezani Sh milioni 200 kwa ajili ya kusaka mtu wa kuja kumpa changamoto, Amissi Tambwe, hapa walifeli na ni vyema wakaanza mawasiliano na Walter Musona kokote alipo.

Chirwa ana uzuri wake na ubaya wake, inategemea tu Yanga watakavyoamua kumtumia.

Hawa wanaosema apewe muda zaidi, hawaamini kama atakuja kufunga mabao 15 msimu ujao, wanachojua atasumbua sana beki za Bongo.

Na ni kweli, kama Chirwa akicheza kutoka pembeni au nyuma ya straika mmoja wa kati, lazima thamani yake ionekane. Ila kwa kumpa jukumu la namba 9 ni kuendelea kumjengea lawama na wale wazee wa Kariakoo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU