Ni vita Ngoma, Mwanjali Oktoba mosi

Ni vita Ngoma, Mwanjali Oktoba mosi

1310
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA

ZIKIWA zimebaki siku chache ili tuweze kuona pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga, homa ya pambano hilo inazidi kupanda kila kukicha.

Ni mechi ambayo inavuta hisia za mashabiki na watu wengine kwa ujumla ambapo kwa mwaka huu kila timu inaonekana kujipanga kisawasawa kwa ajili ya kuibuka kidedea kwenye mchezo huo.

Kuelekea mchezo huo utakaochezwa Oktoba mosi pale Taifa, kuna vita mbalimbali ambayo mashabiki wataishuhudia uwanjani siku hiyo na leo tunaiangalia vita baina ya mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma na beki wa Simba, Method Mwanjali.

Ngoma na Mwanjali ambao wote wanatoka nchini Zimbabwe, wanajuana vilivyo hasa baada ya kukutana kwenye vikosi vya timu ya Taifa mara kadhaa.

Ngoma ambaye ni mshambuliaji wa muda mrefu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, mwenye kasi, nguvu na uwezo wa kucheza soka la aina yoyote ile, atapata upinzani kutoka kwa beki huyo kisiki wa Simba kwa sasa.

Ngoma ni mchezaji msumbufu asiyeogopa mabeki, ni mrefu na anaweza kumiliki mpira na hata kucheza mipira ya juu atalazimika kuonyesha uwezo wake wa hali ya juu kwenye mchezo huo na pengine kuifungia timu yake bao kama alivyofanya katika mchezo wa msimu uliopita.

Ikumbukwe kuwa huyu ndiye kinara wa pasi nyingi za magoli huku akifanikiwa kufumania nyavu mara moja msimu huu kwenye michezo mitano waliyocheza mpaka sasa.

Ngoma ambaye anaunda safu ya ushambuliaji Yanga akisaidiana na Amissi Tambwe, wanaonekana kuelewana zaidi na ubora wao umekuwa shida zaidi kwa mabeki wa timu pinzani.

Lakini Simba wana Mwanjali ambaye kiumri kama mtu mzima makeke uwanjani, anacheza soka la kiufundi na anajua kuziba njia za washambuliaji.

Mwanjali anacheza kwa kujituma na ni beki mwenye nguvu na akili hana makosa ya kizembe ambapo amekuwa kaicheza pamoja na Novalty Lufunga.

Wametengeneza mseto mzuri kwenye timu hiyo ambapo Mwanjali ni beki ambaye amekuwa na nidhamu katika ukabaji wake na kufanya safu za ushambuliaji za timu pinzani kushindwa kufurukuta kabisa.

Kwenye mchezo dhidi ya Yanga beki huyo atakuwa na kazi ya kutembea na Ngoma ambaye ni mviziaji mahiri. Staili ya uchezaji wake inafahamika lakini ukizubaa kidogo tu anakuliza.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU