Jux, Chege, Shilole, Lord Eye kuiteka Mbeya Tigo Fiesta leo

Jux, Chege, Shilole, Lord Eye kuiteka Mbeya Tigo Fiesta leo

1159
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU

BAADA ya kutimua vumbi katika mikoa takribani 12, hatimaye Tamasha la Tigo Fiesta 2016, leo litatimua vumbi jijini Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine ambapo wasanii Jux na Chege, wanatarajiwa kuwaongoza wenzao kufanya yao kuendeleza shangwe za tukio hilo kubwa kabisa nchini la burudani.

Tamasha hilo linapiga hodi Mbeya, ikiwa ni baada ya kupagawisha wakazi wa Mkoa wa Mtwara mwishoni mwa wiki iliyopita kabla ya jana wasanii waliopo katika msafara wa tukio hilo kuwarusha vilivyo watu wa Sumbawanga.

Kilele cha tamasha hilo kinatarajiwa kuwa jijini Dar es Salaam Oktoba 29, mwaka huu ambapo kunatarajiwa kuwa na ‘surprise’ ya msanii kutoka nje ya nchi ambaye hadi sasa hajatangazwa.

Katika tamasha la mwaka huu, wapenzi wa muziki wamejikuta wakipata burudani safi kutoka kwa wasanii mbalimbali ambao wamefanikiwa kutoa shoo ya aina yake.

Wasanii ambao wamekuwa wakipanda jukwaani katika mikoa yote tamasha hilo lilikofanyika, wameacha gumzo kutokana na burudani ya nguvu waliyoitoa, kuanzia katika uimbaji hadi uchezaji.

Lakini pia kwa mwaka huu wasanii wameonesha uwezo mkubwa wa kuimba muziki wa moja kwa moja wakiwa kwenye majukwaa tofauti na ilivyokuwa misimu kadhaa iliyopita.

Burudani hiyo kwa mwaka huu imekwenda sambamba na ugawaji wa madawati kutoka kampuni ya Tigo kwa kila mkoa ambao tamasha hilo limefanyika.

Katika tamasha la leo, mbali ya Jux na Chege, wasanii wengine watakaopanda jukwaani kwa mujibu wa orodha iliyotolewa na waratibu, Prime Times Promotions, ni Darassa, Mr. Blue na Billnass.

Wengine ni Shilole, Ben Pol, Man Fongo, Roma, Weusi, Msami, Lord Eyes, Quick Racka, Baraka Da Prince, Maua, Nandy, Chege, Stamina, Hamadai.

Kati yao, Chege, Jux na Shilole wanatarajiwa kuwa kivutio zaidi kwani walikosekana katika matamasha ya Mtwara na Sumbawanga hivyo kuwapo jukwaani leo ni wazi watafanya mambo ambayo yatawaacha hoi wapenzi wa burudani wa Mbeya.

Waandaaji wa Tamasha la Fiesta, Kampuni ya Prime Times Promotion chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake, Joseph Kusaga, wameahidi tamasha la mwaka huu kuwa la aina yake katika kila mkoa watakaofika na kwamba wapenzi wa burudani watarajie kupata shoo za nguvu kutoka kwa wasanii wao.

Kusaga, anasema: “Tutaendelea na harakati zetu za kuendeleza vipaji kutoka kwa wasanii wapya na wanaoibukia katika kizazi kipya wakati wa tamasha la Fiesta 2016 kama ambavyo tulifanya awali wakati wa tamasha la Dance la Fiesta, Fiesta Super Star na Bonanza la Soka la Fiesta.

“Ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 15 ya Tamasha la Fiesta nchini, mwaka huu tutaendesha kampeni maalum inayojulikana kama ‘kipepeo’ kwa ajili ya kuwatambua na kuwasaidia wasichana walio na mahitaji maalumu katika mikoa 15 ambako tamasha  hili litafanyika.”

Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Tigo, Savkat Berdiev, anasema wapenzi wa muziki watarajie burudani ya nguvu kutoka kwa wasanii wa muziki wa ndani na nje ya nchi.

“Ikiwa ni kampuni iliyojikita katika kukuza sekta ya muziki wa ndani, tunayo furaha kuwa wadhamini wakuu wa tamasha hili kubwa la muziki nchini Tanzania. Lengo letu kila mara limekuwa ni kunyanyua wasanii wa ndani kupitia majukwaa ambayo  yatawawezesha kuonesha vipaji vyao, kuwaunganisha na  mashabiki ili kuzipaisha  kazi zao na kufanikiwa kupata kiasi kikubwa cha fedha,” anasema.

Akielezea zaidi jinsi mashabiki wa muziki nchini na wateja wao wanavyonufaika na tamasha la mwaka huu, Meneja Chapa wa Tigo, William Mpinga, anasema wanawapatia vifurushi vinavyowawezesha kuchagua kati ya data za GB 1 au visivyo na ukomo vinavyojumuisha dakika 490 Tigo kwenda Tigo.

“Tamasha la Fiesta linawakaribisha Watanzania wote na pia tukio hili linatoa shuguli za kijamii tukiwa na kauli mbiu yetu Fiesta 2016 kwa Kishindo cha Tigo Imoooo,” anasema Mpinga.

Wapenzi wa muziki na burudani kwa ujumla wa Jiji la Mbeya, wanaweza kupata tiketi za kuingia kwenye tamasha hilo leo kwa njia ya Tigopesa na kwa kufanya hivyo, wanapata punguzo la asilimia 10 kwa kuwa watanunua kwa Sh 9,000, wakati wakikata tiketi mlangoni ni Sh 10,000.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU