Vibopa Simba wamaliza kazi

Vibopa Simba wamaliza kazi

2641
0
KUSHIRIKI
SONY DSC

NA ZAITUNI KIBWANA

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ni kama wamemaliza kazi baada ya vibopa wa klabu hiyo wanaounda Kamati ya Mashindano kujiimarisha kila kona kuhakikisha hawapotezi mchezo wowote kizembe kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Simba ambayo mpaka sasa imecheza michezo 13, inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 35, huku wakiwaacha mabingwa watetezi, Yanga, kwa pointi nane.

Wekundu wa Msimbazi hao hadi sasa ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo zaidi ya kukubali suluhu dhidi ya JKT Ruvu ya mkoani Pwani.

Licha ya kutoruhusu kufungwa, pia Wekundu wa Msimbazi hao wameonekana kuwa vizuri kwenye michezo yao ya mikoani ambayo yote wameibuka na ushindi, huku mahasimu wao Yanga na Azam, wakiboronga.

Siri kubwa inayotajwa kuibeba Simba ni usajili mzuri ambapo kikosi cha timu hiyo kimesheheni nyota mbalimbali, huku kikiwa na benchi la ufundi linaloundwa na makocha wataalam ambao ni Joseph Omog na msaidizi wake, Jackson Mayanja.

Jambo lingine linalotajwa kuisaidia Simba kufanya vema simu huu, ni kamati yao ya mashindano chini ya Mwenyekiti, Musley Al Ruwah, ambayo imeonekana kufanya kazi kubwa nje ya uwanja.

Kamati hiyo yeye watu sita inaonekana kuwa na nguvu kubwa kuliko ile ya Yanga yenye watu 16 ambao wanaonekana kuzidiwa mbinu na wenzao hao wa Msimbazi.

Mbali ya Al Ruwah, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hassan Hassanoo, naye anatajwa kuwa mtu muhimu mno katika mafanikio ya Simba kama ilivyo kwa wajumbe Mohamed Nassor, Cosmas Kapinga, Juma Pinto na Octavian Mushi.

Kwa upande wao, wanakamati wa Yanga wakiongozwa na Abdallah Bin Kleb, wameshindwa kabisa kufurukuta na matokeo yake kuishuhudia timu yao ikipoteza mwelekeo pole pole.

Mbali ya Bin Kleb, wajumbe wengine wa kamati hiyo ya Ynaga ni Moses Katabaro, Hussein Ndama ‘Ndama Mtoto wa Ng’ombe’, Yusuphedi Mhandeni, Mustafa Ulungo, Mahende Mugaya, Jackson Mahagi, Samuel Lukumay, Hussein Nyika, Athumani Kihamia,  Felix Felician, Beda Tindwa, Leonard Chinganga, Omar Chuma, Hamad Ali Islam, John Mogha, Roger Lemlembe na wengineo.

Tayari mashabiki wa Yanga wameanza kuopoteza matumaini ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara kutokana na mwenendo wa timu yao, lakini pia kasi ya Simba wanaoongoza ligi kwa kuwa na pointi 35, huku wao wakiwa na pointi 27.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU