Yanga wawageuka mashabiki wao

Yanga wawageuka mashabiki wao

2019
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU

MASHABIKI wa Yanga ni kama wamegeukwa na viongozi wao kutokana na mwenendo wa timu yao katika Ligi Kuu Tanzania Bara unaowafanya wapoteze matumaini ya kutetea ubingwa wao wa ligi hiyo.

Kabla ya kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu Bara, mashabiki wa Yanga walikuwa na matumaini makubwa ya kutetea ubingwa wao kutokana na imani yao kwa kikosi chao kinachoundwa na wachezaji mahiri hapa nchini na wengine kutoka nje ya Tanzania.

Lakini kadiri siku zinavyokwenda, Yanga inaonekana kupoteza mwelekeo, huku watani wao wa jadi, Simba, wakiwa katika kasi ya aina yake ambapoo hadi sasa wapo kileleni mwa ligi hiyo wakiwa na pointi nane zaidi ya Wanajangwani hao.

Pamoja na hali hiyo, hakuna jitihada zozote za makusudi zinazoonekana kufanywa na uongozi wa timu hiyo, zaidi ikiwa ni wajumbe wa kamati ya mashindano ambao wamekuwa mbali na timu wakiwaachia wachezaji na benchi la ufundi kupambana kivyao vyao.

Hali hiyo imeelezewa kuchangia kwa kikosi cha Yanga kujikuta kikishindwa kukabiliana na ‘figisu figisu’ za timu pinzani, hasa katika mechi za ugenini tofauti na ilivyo kwa wapinzani wao wa jadi, Simba.

Yanga ambayo hadi sasa imecheza mechi 13, imeshapoteza mbili, huku ikipata sare mara tatu na hivyo kuwa na pointi 27, wakati Simba wana pointi 35.

Yanga imepoteza mechi zake na Stand United kwa kipigo cha bao 1-0 kabla ya kulala mabao 2-1 kutoka kwa Mbeya City katikati ya wiki hii, huku wakipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba na suluhu walipocheza na Azam pamoja na Ndanda FC.

Mmoja wa viongozi wa Yanga, ameliambia BINGWA akisema: “Kiukweli msimu huu ubingwa wetu umeshaonekana kuingia dosari na hii inatokana na wapinzani wetu kutuzidi ujanja nje ya uwanja kwa kucheza mechi zetu.

“Wenzetu kwenye kamati ya mashindano wanaonekana kuwa vizuri licha ya uchache wao tofauti na sisi, kamati inazaidi ya watu 10, lakini anaonekana mjumbe mmoja tu kila timu inapocheza.”

Alisema kulingana na ligi ilivyo, wasipoanza kuwa makini, ni wazi kuwa msimu huu ubingwa watanyanganywa na Simba ambao wameonyesha wamejipanga katika kila idara.

“Wapinzani wetu wameonekana kujipanga vizuri nje na ndani lakini pia hata michezo yetu tunayocheza bado pia noa wanatia mkono wao, hii inaweza kutugharimu mwisho wa msimu ni wakati wa kuzinduka na ku fuata nyayo zao ili turejee kwenye kiwango cha ushindani,” alisema.

Ikumbukwe kuwa Yanga ipo katika mchakato wa kubadilisha benchi la ufundi baada ya kudaiwa kumalizana na kocha wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina anayetarajiwa kutua nchini muda wowote kuanzia sasa kuanza kazi kubeba mikoba ya Mholanzi, Hans van der Pluijm.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU