UPENDO KUSHINDA UFAHAMU -50

UPENDO KUSHINDA UFAHAMU -50

749
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia jana

AKIWA ananyonga ufunguo, kwa mbali alimuona mtu mmoja akitoka ndani ya jengo lile. Mtu huyo alikuwa ameubeba mwili wa binadamu, mwili ambao aliutua na kuupakia kwenye gari. Macho yalimtoka Shazayi alibaki kumtazama mtu yule asilijue lengo lake.

SASA ENDELEA

Baada ya kuupakia ule mwili, mtu yule aliingia kwenye gari. Akalitoa kwenye eneo la maegesho, akanyonga usukani na kuelekea upande wa kushoto ambako kuna barabara kuu ya mtaa.

Kwa kuwa Shazayi aliona ameshindwa kujua Ramona alikuwa amekwenda mle ndani kufanya nini, aliona njia pekee ya kupata angalau jambo dogo ni kulifuata lile gari, gari lilokuwa limemshtua kutokana na kupakiwa kwa mwili wa binadamu. Kutokana na Ramona  kukawia sana kutoka nje ya jengo lile, alianza kuhisi kuwa huenda kuna jambo baya limemkuta mrembo huyo. Alijua endapo atamkosa Ramona, basi hawezi tena kujua mahali alipo Roika.

Aliwasha gari na kuanza kulifuatilia gari la yule mtu aliyebeba mwili wa binadamu. Kadiri alivyozidi kusogea mbele, ndivyo giza lilivyozidi kutanda, kwa kuwa huko hakukuwa na nyumba nyingi za watu. Aliamua kuzima taa ili yule anayemfuatilia asijue kuna gari nyuma yake.

Baada ya dakika tano, yule mtu alifika eneo moja lililokuwa na mawe. Shazayi naye alikanyaga breki na kulisimamisha gari. Akiwa kwa mbali kidogo, aliona mtu yule akiushusha ule mwili aliokuwa ameupakia.

Mtu huyo alikuwa ni mpiganaji wa kikundi cha Swaba. Aliyekuwa ametumwa kuja kuuchoma moto mwili wa Roika. Baada ya Roika kupigwa risasi, kiongozi wa kikundi hicho, alimwambia mpiganaji wake huyo, auchukue mwili wa Roika na kwenda nao kuuchoma moto.

Alipoushusha mwili wa Roika, uliokuwa kwenye shuka, alichukua dumu la mafuta. Kabla hajaumwagia, alijisachi mfukoni akitafuta kiberiti, ambapo hakukiona. Aliingia kwenye gari na kuanza kupekua akikitafuta. Kwa bahati mbaya aligundua kuwa alikuwa hajajanacho. Alianza kutafuta bastola au bunduki ndani ya gari ili aitumie kuwasha moto kwa kufyatua risasi. Ndani ya gari lake hakukuwa na silaha yoyote.

Kwa kuwa ni mwendo wa dakika sita hadi kwenye jengo lao, aliamua kuingia kwenye gari ili aende akakichukue kiberiti na baadaye arudi kuuchoma moto mwili wa Roika. Aliuacha pale pale mwili wa Roika pamoja na dumu la petroli, akaingia kwenye gari na kuondoka lile eneo kwa kasi.

Aliondoka pale akiwa hajafanikiwa kujua kama kuna mtu alikuwa akimfuatilia. Shazay alikuwa ameliegesha gari lake pembezoni kabisa mwa barabara.

Baada ya mpiganaji yule kuondoka, Shazayi aliingia kwenye gari lake, ambapo alichukua tochi na kuelekea pale ulipokuwa mwili. Alipofika, aliuona mwili wa mtu pamoja na dumu la mafuta. Moja kwa moja alijua mtu yule alikuwa amekusudia kuuchoma moto.

Shazayi alijikuta anaogopa kuufunua ule mwili, mwili aliokuwa amehisi kuwa huenda ulikuwa ni mwili wa mrembo Ramona. Baadaye kidogo nafsi yake ilimtuma kuufunua. Alipoumulika  sehemu za kichwani, hakuyaamini macho yake kabisa. Alianza kuhisi labda zile ndoto anazoota kila siku kuhusu Roika zinazidi kumuandama. Macho yake yalikuwa yameona kitu halisi na sahihi, lakini yeye kama yeye hakuamini moja kwa moja. Alijikuta ananza kuweweseka. Mwili wake ulianza kutetemeka, machozi aliyoshindwa kuyazuia, yalianza kumtoka. Baadaye aliamini ule mwili ulikuwa ni wa Roika, kijana wa Kiafrika mwanaume anayempenda kushinda ufahamu wake. Hakika alichanganyikiwa.  Alianza kulia hovyo, sauti yake ilikuwa kubwa, hakujali utulivu wa eneo hilo na giza lilokuwa linazidi kuwa jeusi, alilia sana mtoto huyo wa Rais, akijua tayari Roika wake alikuwa amekwisha kufa.

Akiwa analia, alianza kusikia sauti ya mtu akihema kwa tabu, aliacha kulia kwa muda, ambapo aligeuka nyuma ili kuona kama kulikuwa na mtu aliyekuwa lile eneo. Lakini hakuwa na mtu mwingine zaidi yake yeye na ule mwili wa Roika.

Baadaye alishtuka, macho yalimtoka, baada ya kugundua mtu aliyekuwa akihema kwa tabu, alikuwa ni Roika. Kama mtu aliyekuwa chizi alitoka pale mbio akalifuata gari lake na kulisogeza hadi pale ulipokuwa mwili wa Roika. Alijitahidi kumbeba Roika kwa nguvu ambazo yeye mwenyewe hakujua amezitoa wapi. Alimpakia kwenye gari na kuondoka naye lile eneo kwa kasi isiyo ya kawaida.

Licha ya kupigwa risasi mbili, Roika alikuwa bado anahema bado alikuwa ni mzima. Lakini hali yake ilikuwa mbaya sana, muda wowote angeweza kupoteza maisha. Damu nyingi zilizidi kumtoka sehemu za tumboni sehemu ambako alipigwa risasi. Wakati huo akili ya Shazayi ilikuwa mbele, ikiwa makini kwenye usukani. Machozi yalizidi kumtoka, mara chache alikuwa akigeuka nyuma kumtazama Roika. Alijua ana muda mchache sana wa kumuokoa mwanaume huyo anayemfanya kuwa kichaa wa mapenzi.

Wakati yeye anatoka kule alikokuwa amemchukua Roika, yule mpiganaji wa Swaba alikuwa anarudi, akitokea kwenye jengo lao, alikokuwa amekwenda kuchukua kiberiti, kwa ajili ya kuuchoma moto mwili wa Roika.

Nini kitafuatia usikose kesho

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU