LWANDAMINA AIBUA UOZO YANGA

LWANDAMINA AIBUA UOZO YANGA

3764
0
KUSHIRIKI

NA WINFRIDA MTOI

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, amekutana na kitu cha kushangaza kidogo katika mazoezi ya timu yake hiyo mpya, hali inayoonyesha kuwa ana kazi kubwa ya kufanya wakati huu timu hiyo ikijiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

Lwandamina, ambaye ni kocha wa zamani wa Zesco ya Zambia, aliposikia kuwa Yanga ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, alitarajia kukuta idadi kubwa ya wachezaji wanajua mambo mengi, lakini akakutana na kioja.

Cha ajabu alichokutana nacho kocha huyo ni baadhi ya wachezaji kutokuwa na uwezo wa kumiliki mpira, hali iliyomfanya kuanza upya kufundisha, kitu ambacho kiliwashangaza baadhi ya mashabiki.

Katika mazoezi hayo ambayo yalifanyika Gymkhana juzi, Lwandamina alionekana kuwafundisha baadhi ya wachezaji jinsi ya kupokea mpira na namna ya kuumiliki, hali iliyowafanya baadhi ya mashabiki kushikwa na mshangao.

Baadhi ya mashabiki hao walivunja ukimya na kutamka wazi kuwa kama hali itakuwa hivyo, basi kocha wao huyo itabidi akaze sana msuli kuelekeza, vinginevyo anaweza akaonekana mbaya timu itakapofanya vibaya, kosa ambalo si lake.

“Dah! Jamani hii hali mbaya sana, hivi kumbe kwenye timu yetu kuna wachezaji ambao hata kumiliki mpira hawawezi kabisa! Kwa hali hii kocha atakuwa na kazi kubwa ya kuanza kuelekeza na mpaka wamuelewe itawachukua muda.

“Kweli saa nyingine makocha wanafukuzwa kwa makosa ambayo si yao kabisa, hivi mchezaji anasubiri kufundishwa namna ya kumiliki mpira halafu mashabiki tutarajie nini hapo?” Alihoji shabiki mmoja aliyekuwa akishuhudia mazoezi hayo.

Mwingine alidakia na kusema: “Ni kweli makocha saa nyingine wanabebeshwa mizigo ambayo si yao, kwa mfano Lwandamina alitakiwa afundishe tu mbinu za kukabiliana na timu pinzani, lakini angalia anaanza kufundisha namna ya kumiliki mpira, du! Wengine nadhani hata kupiga danadana kwao ni tatizo.”

Katika mazoezi hayo, Lwandamina ameonekana kuanza kupitia njia za kocha wa zamani wa timu hiyo, Mbrazil Marcio Maximo, kwa kumpika Juma Said Makapu ambaye ni zao za kocha huyo aliyetimuliwa kwa madai ya kushindwa kwendana na kasi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.

Makapu ni mmoja wa wachezaji walioanza kuonekana katika kipindi cha Maximo ambapo kinachofanywa na Lwandamina kwa kuanza kumpika upya ni wazi kitendo hicho kinaonyesha kuwa Mzambia huyo anahusudu kiwango chake na anataka kumpika ili baadaye awe tegemeo lake.

Mbali na Makapu, pia kocha huyo alitumia muda mwingi kumuelekeza kiungo mshambuliaji Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, hii ikionyesha kuwa kuna kitu cha ziada anataka kiungo huyo akionyeshe.

Ni wazi kuwa uamuzi wake huo umetokana na viwango vya wachezaji hao alivyoviona kupitia video za mechi walizocheza wakiwa na kikosi cha wana- Jangwani hao.

Wakati Niyonzima akiwa ni mchezeshaji na mpishi mzuri wa washambuliaji, Makapu, iwapo ataaminiwa na kupewa mechi zaidi, anaweza kutibu tatizo sugu ambalo limekuwa likiikabili Yanga la kiungo mkabaji mwenye uwezo wa hali ya juu kuilinda safu ya ulinzi na kuiunganisha na ile ya ushambuliaji.

Uzuri wa Makapu, ni mrefu mwenye uwezo wa kucheza mipira ya juu na chini, lakini pia nguvu za kupambana na viungo na washambuliaji wa timu pinzani.

Kabla ya kuanza kibarua chake hicho, kocha huyo alipitia mikanda mbalimbali na kushuhudia uwezo wa wachezaji wake na sasa anajua uwezo wa kila mmoja.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU