WAZEE SIMBA WAMKATAA MO

WAZEE SIMBA WAMKATAA MO

1755
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

WAKATI Baraza la Wazee la Klabu ya Yanga kupitia kwa katibu wake, Ibrahim Akilimali wakisema hawawezi kuikodisha timu kama masufuria ya msibani, wakipinga aina ya mabadiliko yanayotakiwa kufanywa ndani ya klabu hiyo, wajumbe wa Baraza la Wadhamini la Simba nao wameibuka kutoka mafichoni na kutoa dukuduku lao juu ya mchakato wa mabadiliko Msimbazi.

Mzee Akilimali alisema kwamba Yanga haiwezi kukodishwa kama masufuria ya msibani, akipinga timu kukodishwa kwa miaka 10 ambapo wakati wengi wakidhani Simba ni shwari, kumbe Baraza la Wadhamini lilikuwa linajipanga kuona linatokaje katika hilo.

Baraza hilo la Simba, limeibuka na kupinga vikali Mkutano Mkuu wa dharura uliotishwa na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Desemba 11, mwaka huu, lakini pia wakionekana kutokumuunga mkono Mohamed Dewji ‘Mo’.

Kamati hiyo ya Utendaji iliitisha Mkutano Mkuu wa dharua kwa ajili ya kujadili namna ya kubadili katiba ili kuendana na mabadiliko ya kimfumo wanayotaka kuyafanya waendeshe timu kwa mfumo wa hisa, jambo ambalo wazee hao wanalipinga.

Mbadiliko hayo yamekuja baada ya mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewij (MO), kutaka kununua hisa ya asilimia 51 ya uendeshaji wa klabu hiyo, huku 41% zikibaki kwa wanachama.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mzee Hamisi Kilomoni alisema tangu kuanza kwa mchakato wa kutaka Simba iingie kwenye mfumo mpya wa uendeshaji kumekuwa na mambo mengi yakiendeshwa kinyume cha katiba ya timu hiyo, ikiwemo suala la ushirikishwaji wa wanachama.

Alisema hivi sasa Simba imekuwa ni ya wanachama wachache, hususani wa Mkoa wa Dar es Salaam peke yake, jambo ambalo si zuri, kwani Klabu hiyo inao wanachama wengi mikoani.

Kilomoni alisema Baraza la Wadhamini limepokea barua kutoka kwa wanachama wa klabu hiyo wakilalamikia mkutano huo ambapo nakala za barua zimefika hadi kwa Rais John Magufuli, Baraza la Michezo (BMT) pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambapo kwa kuliangalia suala hilo kwa mapana yake wakagundua wana hoja ya kuipigania klabu yao.

“Hapa kuna barua nyingi kutoka kwa wanachama, wakiomba kusitisha mkutano huo, mpaka kufikia kupeleka barua kwa Rais wa nchi ujue hilo si suala dogo, sisi kama wenye klabu tumeamua kumuomba Mkuu wa Mkoa (Paul Makonda) kuusimamisha mkutano huo ili isije ikatokea balaa zaidi.

“Huyo Mo alishawahi kuja kutuona na kutueleza nia yake ya kumiliki asilimi 51 ya hisa ndani ya klabu, tukamwambia haiwezekani kwa kuwa Simba inahusisha zaidi ya mchezo wa soka pekee, lakini pia Simba ni timu ya gharama na thamani kubwa kuliko hiyo asiliami 51 anayoitaka yeye, kwa maana hiyo haiwezekani  kuona wanachama wachache tu wanaopenda soka ndio wamiliki wa klabu,” alisema Kilomoni.

Kuhusu kuondolewa kwa Baraza la Wadhamini wa Simba mara baada ya kuingia madarakani kwa Rais Evans Aveva kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama uliofanyika Agosti, mwaka 2014, Mzee Kilomoni alisema yeye bado yupo kwenye orodha ya wadhamini wanne wa klabu hiyo, baada ya kupinga kuenguliwa huko kupitia kwa msajili wa klabu  na RITA.

“Mimi bado ni mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, kwani ninayo barua ya kutoka RITA iliyotolewa Agosti 12 mwaka huu ikiainisha majina ya wadhamini wa klabu ya Simba ambao ni Abdul Wahab Abas, Ally Sykes (marehemu), Ramesh Patel na mimi,” alisema nyota huyo  wa zamani wa Simba.

Hayo yanatokea wakati ambao MO akiwa ametumia fedha zake nyingi tu kusaidia mambo mbalimbali ndani ya Simba, ikiwamo mishahara ya wachezaji na za usajili.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU