NIYONZIMA: AKIINGIA ZULU NDIYO MTAISOMA YANGA

NIYONZIMA: AKIINGIA ZULU NDIYO MTAISOMA YANGA

2518
0
KUSHIRIKI

ZAINAB IDDY NA WINFRIDA MTOI

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima, amewasikia mashabiki wanaobeza kiwango cha soka cha kiungo wa chini wa timu hiyo, Justine Zulu, lakini yeye amesema neno moja tu kuwa jamaa huyo anajua.

Niyonzima ambaye amefanya mazoezi kwa muda mfupi na Zulu, baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea klabu ya Zesco ya Zambia, amesema Zulu ana vitu vingi mguuni mwake tofauti na watu wanavyodhani.

Zulu aliyesajiliwa katika dirisha dogo la Ligi Kuu Tanzania Bara, amebezwa na baadhi ya mashabiki wa Yanga na hata wale wa upande wa Simba ambao wamedai kiungo huyo si lolote baada ya kucheza dakika 45 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Yanga kufungwa mabao 2-0.

Lakini Niyonzima ameibuka na kusema kiungo huyo aliyeletwa na kocha mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina, ni mchezaji mzuri na ataisaidia Yanga katika harakati zao za kutetea ubingwa.

Niyonzima alisema kwa kipindi walichofanya mazoezi pamoja amebaini ni mchezaji ambaye ana vitu vingi mguuni na kinachotakiwa ni kupewa muda ili aweze kuzoea mazingira.

“Zulu anajua lakini huwezi kumzungumzia mchezaji kwa kucheza  mechi moja au mbili, lakini nilivyomwona kwenye mazoezi kwa kweli ni mchezaji mzuri, sasa watu wasubiri tucheze pamoja mimi yeye na Kamusoko ndiyo waone utamu wa Yanga,” alisema Niyonzima.

Kuhusu kikosi chao kwa ujumla, alisema kiko vizuri licha ya changamoto zilizopo katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo.

Niyonzima alisema ligi ni ngumu  kutokana na timu nyingi kujipanga ili ziweze kupata matokeo mazuri na baadaye wachukue ubingwa.

“Mpira ni kazi yetu, lazima tukubaliane na hali na mwalimu ni mpya, kuna baadhi ya mambo amebadilisha kidogo kama wachezaji tunatakiwa kumsikiliza na kufanyia kazi kile anachotuelekeza,” alisema.

Katika hatua nyingine, Niyonzima ameanika siri zilizowafanya wapate ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wao dhidi ya JKT Ruvu uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Niyonzima alisema siku zote wanahitaji ushindi wa mabao mawili, hivyo lazima wacheze kwa umoja na kuzingatia maelekezo ya benchi la ufundi.

Yanga wanatarajia kucheza na African Lyon katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU