BONGO MOVIE MNAMSUBIRI NANI AJE KUWAAMSHA?

BONGO MOVIE MNAMSUBIRI NANI AJE KUWAAMSHA?

608
0
KUSHIRIKI

NA ABDUL KHALID, TSJ

TAKRIBANI miaka minne imepita sasa tangu kutokea kwa kifo cha aliyekuwa staa wa filamu Bongo, Steven Kanumba, ambapo tumeweza kushuhudia mambo mbali mbali yakitokea katika tasnia hiyo.

Tangu Kanumba aondoke duniani, tasnia ya filamu imedorora kwa kiasi kikubwa na tumeona dhahiri wasanii wengi wakishindwa kuvaa viatu vilivyoachwa na mkongwe huyo.

‘Bongo Movie’ imepoteza ule mvuto wake uliokuwa nao awali kwa mashabiki wake na hiyo ni kutokana na wasanii wengi kutotoa kazi zenye viwango ambazo hazikidhi kiu za wafuatiliaji wa kazi zao.

Baadhi ya wasanii wamekuwa wakikiri kwamba soko la filamu limeshuka na hiyo ni kutokana na kifo cha staa huyo, kwani ndiye aliyekuwa chachu na changamoto kubwa iliyokuwa inawafanya wasanii wengine kufanya kazi kwa bidii.

Leo tutapata kuitazama kiundani tasnia ya filamu hapa nchini kwetu ‘Bongo Movie’ pamoja na changamoto zinazowakumba na kusababisha soko lao kuporomoka.

Zipo sababu nyingi zinazofanya kazi za hawa ndugu zetu kukosa mvuto, lakini tutaziangalia chache ambazo ni muhimu na zitakazowasaidia kama zikitafutiwa ufumbuzi.

USIMAMIZI

Hili ni mojawapo kati ya mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kudidimia kwa tasnia hii na sitashangaa kuona wakiishia hapa hapa walipo ama wakiendelea kudidimia zaidi ya hapa kama wasipoweza kulichukulia hatua za mapema jambo hili.

Siku zote ili msanii aweze kufanikiwa ni lazima awe na usimamizi ulio bora na wenye kuweza kutatua changamoto zake bila kusahau kutengeneza mazingira chanya yatakayotoa fursa na uhuru kwa mteja wake kufanya vizuri.

Wasanii wengi wa filamu hapa nchini wanaukosa usimamizi ambao nimejaribu kuuelezea kwa kiasi fulani hapo juu na hiyo itaendelea kuiadhibu kwa kiasi kikubwa sana tasnia yetu ya filamu kama hatua zisipoweza kuchukuliwa.

MIGOGORO

Ni muda mrefu sasa tasnia hii imekuwa ikiandamwa na migogoro ya hapa na pale kati ya wasanii na viongozi, huku muda mwingine ikiwa ni kati ya wasanii wenyewe kwa wenyewe.

Kutokana na kuwapo kwa migogoro hiyo ya mara kwa mara, imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma kazi zao ambapo wengi wao wamekuwa wakitumia muda mwingi huko na kushindwa kufanya kazi.

Muda mwingine migogoro hii imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa wasanii kutoa kazi zisizokuwa na viwango, ambazo zinazidi kuwapunguzia sifa sokoni na hata kwa mashabiki zao waliozoea kuona kazi nzuri kutoka kwao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU