UPENDO KUSHINDA UFAHAMU

UPENDO KUSHINDA UFAHAMU

457
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia Jumanne

Kwa furaha kubwa na machozi, Roika alimkumbatia Dk. Sufian, akaelekea kitandani alikolala Shazayi akamshika kichwani na kumbusu. Alijawa na furaha isiyoelezeka kwa urahisi.

SASA ENDELEA

FURAHA ilikuwa kubwa ndani ya Hospitali ya Mohamed Words, si Roika tu aliyefurahia kupona kwa Shazayi, bali hata Dk. Sufian na wafanyakazi wake wote wa hospitali hiyo walizipokea taarifa hizo kama muujiza kwao. Ile hofu ya kupelekwa mahakamani haikuwapo tena, japokuwa bado Serikali ya Pakistani ilikuwa ikiendelea kumtafuta mtoto wa Rais kila kona ya nchi.

Roika alilia kilio cha furaha kisicho kuwa na mfano, kwani alimwona Shazayi kwake ni kama malaika. Ndani na nafsi yake alishamfanya Shazayi kuwa mkewe, hakutaka kujua kuwa ni vikwazo gani atakumbana navyo pindi atakapokuwa kwenye hatua za kumuoa binti huyo wa Kiarabu tena mtoto wa Rais. Alichojua yeye Shazayi ni mke wake tena mke wake wa maisha. Kwa wakati huo hakumfikiria kabisa mrembo wa dunia, Ramona Fika, aliyekuwa akimpenda kuliko mwanamke mwingine yeyote hapa duniani. Alimtafakari Mungu na kumwona ni wa ajabu. Kwani alikuwa amempa mke ambaye yeye hakumtarajia. Siku zote yeye aliamini kuwa mke wake ni lazima aje kuwa Ramona na si mwanamke mwingine na hata kama atakuwa si Ramona, basi atakuwa ni mwanamke mwingine atakayetoka bara lake la Afrika na nchi yake ya Tanzania.

Alikumbuka kwa mara ya kwanza alipokutana na mtoto huyo wa Rais, katika hospitali hiyo hiyo pindi wote walipokuja kuwajulia hali watoto waliokumbwa na shambulio la bomu.

Ilimaanisha kuwa Mungu aliwakutanisha watu wenye tabia moja na wenye mienendo sawa ya kifikra. Kwani Roika alikuwa ni mtu anayewapenda sana watoto na ni mtu aliyependa kuwasaidia masikini na watu wanaoishi katika mazingira ya magonjwa na vita. Ndivyo na tabia Shazayi ilivyokuwa. Mtoto huyo wa Rais, aliwapenda sana watoto na wanawake wanaoishi katika mazingira magumu. Kama Roika ambavyo alikuwa na vituo vya kulelea watoto na wazee, mtu aliyejenga hospitali ya wanawake, Shazayi naye alikuwa na hospitali kubwa nchini Haiti, iliyokuwa maalumu kwa watoto, wanawake na wazee. Mwanamke huyo alitumia pesa yake na pesa anayopewa na baba yake kuwasaidia watu wote wasiojiweza.

Asubuhi hiyo, macho ya Roika hayakuchoka kumtazama Shazayi, alijikuta anazidi kumpenda sana kupita ufahamu wake wa kawaida. Uso wa Shazayi ambao mwanzo ulikuwa unaelekea kuwa uso wa maiti, kwa muda huo ulianza kurudi  na kuonekana wenye kung’aa kama ya jua. Macho yake mazuri, yenye kope za kupendeza, midomo yake ya rangi ya zambarau ilizidi kumpendezesha Shazayi aliyekuwa kwenye usingizi mzito, akiota ndoto za ndoa, ndoa yake na Roika.

Dk Sufiani alikaa kwenye meza na kuongea na Roika. Yeye pia alikuwa na furaha kubwa kwani hakuwa na hofu tena  ya kunyongwa. Alimuona Roika ni mkombozi wake.

“Mr Roika unastahili pongezi, hakika umeleta ukombozi unaofanana na nguvu ya jua. Mimi sitakuwa na mengi ya kusema ila maneno yangu makuu ambayo yataendelea kuishi siku zote ni  kwamba, huyu ndio ubavu wako wa kushoto, roho yako na mama wa watoto wako,” aliongea Dk Sufian akiwa amemshika Roika bega.

“Hakika Dk Sufian, pia nakushukuru na wewe kwa kuweza kuokoa maisha yake. Mungu akubariki naamini Mungu alisimama katikati yetu.”

“Usijali Mr Roika ni kazi yangu. Ila nachotaka kusema ni kwamba, Shazayi ataendelea kuwa hapa, kwa siku zingine mbili. Ingawa tuko kwenye hatari kubwa. Kwani  serikali inamtafuta  binti huyu  kila kona.”

“Kwa kiasi fulani niachie mimi. Wewe endelea na ratiba zako zingine za hospitali. Nitakaa pembeni yake muda wote. Na hata kama nitatoka nitarudi mara moja, nataka akifungua macho anione mimi.”

Baada ya kuongea hayo Dk Sufiani alitoka chumba cha ICU na kurudi ofisini kwake ambako huko aliendelea na ratiba zake  zingine za kihospitali. Alimuacha Roika karibu na kitanda cha Shazayi.

Taarifa za kupotea kwa mtoto wa Rais, zilizidi kutangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari, ndani ya nchi na nje ya nchi. Shirika la utangazaji la BBC, lilikuwa la kwanza kuripoti habari hiyo kwa upande wa vyombo vya habari vya nje ya Pakistani.

Kikundi cha kigaidi cha Swaba kilitoa mkanda wa video, kikisema kuwa kinamshikilia mtoto wa Rais, Shazayi binti Galim. Jambo ambalo lilikuwa si la kweli. Mkanda huyo ulisema uongo mtupu. Swaba waliamua kutoa uzushi huo kwa masilahi yao binafsi, ikiwemo kuitishia Serikali ya Rais Galim na kuitaka itoe kiasi kikubwa cha pesa na kukipa eneo la Ramadan Kash lenye visima viwili vya mafuta, eneo lililokuwa linashikiliwa na jeshi la nchi hiyo.

Nini kitafuatia? Usikose kesho.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU