TBBF WAGEUKIA VYUO VIKUU

TBBF WAGEUKIA VYUO VIKUU

691
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

PENGINE kama kuna mchezo ambao nao uliwahi kupendwa katika miaka ya 1990, ni ule wa kutunisha misuli kwani ulitajwa kila kona kiasi cha kupata wadhamini lukuki.

Katika kipindi hicho, vilifunguliwa vituo vingi vya mazoezi ya viungo (gym) na kuanzishwa pia mashindano katika wilaya, mkoa na taifa.

Kwa miaka ya hivi karibuni, hali imekuwa tofauti kwani licha ya wadhamini kupungua pia hata wanamichezo wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na hali hiyo, shirikisho la mchezo huo Tanzania (TBBF), halijakata tamaa kwani kila mwaka limekuwa likiandaa shindano la kitaifa linalojulikana kwa jina la ‘Mr Handsome’.

Mwakani mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika yakiwa na kauli mbiu ya ‘Taifa lenye afya, wananchi wenye afya’.

Mbali na kuandaa shindano hilo kwa mwaka huu, lakini pia TBBF limejipanga kustawisha mchezo huo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ili  waweze kujiunga na kushiriki shindano la kumsaka Mr. Tanzania kwa mwakani inayofahamika kwa www.tztbbf.org ambayo itatumika kujiunga katika mashindano  mbalimbali yanayoandaliwa na chama hicho.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili, Mratibu wa Mashindano wa TBBF, Fike Wilson, anafafanua kuwa lengo la kutengeneza mtandao huo ni kutoa urahisi kwa wanamichezo wanaotaka kushiriki mashindano hayo mwakani kuweza kutuma maombi yao kwa urahisi kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

“Kumekuwa na usumbufu mkubwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni pindi wanachama wetu na wanamichezo wanapotaka kujiunga na mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na chama, kwani wengine wanalazimika hata kutumia kiasi kikubwa cha fedha ili kuthibitisha ushiriki wao, hivyo tumeona si vibaya tukatafuta njia ya kutatua tatizo hilo nayo si nyingine ila ni kuingia kwenye utandawazi,” anasema.

Anaongeza: “Mwanamichezo mtunisha misuli anapotaka kuwa mshiriki wa mashindano yanayoandaliwa na chama ni lazima awe na kifaa kitakachoweza kumpatia intaneti, ambapo ataingia www.tztbbf.org, kisha kuandika jina kamili, anuani na namba yake ya simu si vibaya akiweka na barua pepe kama anayo ili iwe rahisi kuwasiliana naye.”

Naye Katibu Mkuu wa TBBF, Francis  Mapungilo, anasema usajili wa mashindano hayo kwa mwakani umefunguliwa tangu Desemba 8, mwaka huu, huku ukitarajiwa kufungwa Januari 15, mwakani hivyo ni muda mzuri kwa yeyote anayetaka kushiriki kujisajili.

Anasema kwa mara ya kwanza tangu kuazishwa kwa mashindano hayo, wajenga mwili watatakiwa kuwa wanachama katika gym na klabu za mazoezi ya viungo tu, lengo likiwa ni kukuza na kuwezezesha utamaduni wa kufanya mazoezi ya gym kwa watu wengi.

Naye mmoja wa watakoshiriki katika michuano hiyo, Omari Abdalah, anasema kuwa mchezo wa kutunisha misuli ni mzuri hasa kwa vijana wa kiume kwani mara kwa mara wanalazimika kufanya mazoezi ya kuinua vitu vizito.

“Kitendo cha kuingia gym mara kwa mara kufanya mazoezi kunasababisha miili yetu kujengeka katika mwonekano mzuri kiasi hata cha kuwavutia wanawake ingawa hatushauriwi kutumia miili yetu katika anasa.

“Kwa kiasi kikubwa mazoezi yanamfanya kijana kuondoa mawazo ya anasa kama ataamua kufuata masharti yake, kwani progamu zake husababisha kijana kutokuwa na muda mwingi wa kufikiria vitendo viovu binafsi nawashauri vijana wengi wajitokeze katika mchezo huu,” anasema.

 Vigezo vya ushiriki

Mwenyekiti wa TBBF, Albert Chiwala, anavitaja vigezo vya ushiriki wa Mr. Tanzania kuwa ni sawa na vile vinavyotumika kwa Mr Africa, Mr World na Mr. Universe ambapo washiriki wote wanatakiwa kufuata misingi saba muhimu ya utunishaji misuli.

“Mbali na misingi hiyo ambayo inatambulika kisheria katika mchezo huo, lakini pia unapotaka kuthibitisha ushiriki wako lazima uambatanishe  walau si chini ya picha nne na zisizidi saba,” anasema.

 Zawadi

Kwa upande wa zawadi za washindi, Mr Photogenic na Mr Handsome wanatajwa kuwa watapata zawadi ya fedha taslimu kiasi cha Sh 5000,000 na mkataba wa kuchezeshwa filamu na tamthilia kutoka pilipili entertainment co. ltd.

Mshindi wa kwanza wa Mr Tanzania atazawadiwa 10,000,000 (milioni kumi) na gari, wa pili atapewa 5000,000 (milioni tano) huku wa tatu atajinyakulia kitita cha 2,500,000 (milioni mbili na nusu).

“Katika kilele cha fainali za mashindano haya itakayofanyika siku ya June 30 mwakani jijini Dar es Salaam, mshindi wa shindano la Mr. Tanzania atapata nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya Mr Africa, Mr Universe na Mr World  yaliopangwa kufanyika Novemba mwakani,” alisema Chiwala.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU