UPENDO KUSHINDA UFAHAMU

UPENDO KUSHINDA UFAHAMU [72]

643
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia jana

Ramona aliposikia hivyo, alianza kulia tena, maana maneno hayo yalizidi kumuumiza yeye kama muuaji wa mmoja wa familia ile.”

 “Usilie mwanangu, tayari tumekwisha sameheana. Ninachotaka tu binti yangu asijue lililompata kaka yake.”

 “Mama najiona ni mwenye dhambi. Naumia pindi napowatazama wewe na huyu mwanao. Kwa kuwa mimi ni chanzo cha nyie kuishi bila Roika,” aliongea Ramona.

SASA ENDELEA

WAKIWA wanaendelea na maongezi, Dina alirudi sebuleni. Ilionyesha ana hamu sana ya kujua ni kipi hasa kilikuwa kimemleta mrembo huyo wa dunia nyumbani kwao. Na nini kilikuwa kikimliza.

“Tayari mama, nimekwishabandika ile sufuria kubwa.”

“Sawa mwanangu hongera kwa kufanya hivyo.”

Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, mama Roika alimwambia Ramona.

“Ramona mwanangu, huyu anaitwa Dina ni mtoto wangu wa pili baada ya Roika.”

Akamgeukia na Dina na kumwambia.

“Dina, huyu anaitwa Ramona ni rafiki yake na kaka yako.”

Ramona alimtazama Dina, wote wakatazamana. Lakini Dina alitabasamu. Kwa kuwa alijua kuwa kaka yake anaweza kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Ramona. Kwa kuwa siku zote Dina alikuwa ni shabiki namba moja wa mrembo huyo wa dunia, kuambiwa kuwa Ramona ni rafiki wa kaka yake, kulimfanya kuwa na furaha isiyopimika.

Lakini hakuwa akijua nyuma ya pazia, kulikuwa na nini. Baadaye alimsogelea Ramona na kumpa mkono. Ramona aliutoa mkono, huku akijikaza kisabuni maana bado moyo wake uliomkumbuka Roika ulizidi kuteseka, pindi alipozidi kuiona familia hiyo.

“Karibu nyumbani kwetu Ramona. Mimi ni shabiki wako nambari moja ninakupenda sana. Chumbani kwangu nimejaza picha zako. Kufika kwako naona ni muujiza, kumbe una urafiki na kaka yangu. Hongera sana kaka yangu ni mtu mzuri hakika umechagua rafiki bora,” aliongea Dina maneno yaliyozidi kuutupa moyo wa Ramona kwenye tanuru la moto.

Alimtazama mama Roika na kisha akamtazama Dina na kumjibu.

“Asante Dina nashukuru kuwa shabiki yangu nambari moja. Mimi na kaka yako ni marafiki sana.”

“Karibu sana Ramona karibu sana. Lakini naona hali yako si nzuri sana unaumwa?”

“Hapana Dina niko sawa tu.”

Dina hakujua lolote lililokuwa likiendelea, hakujua kuwa lengo la Ramona kuja  nyumbani kwao, lilikuwa ni kuwataarifu kuwa Roika alikwisha kufa.  Kifupi hakuja chochote. Aliyekuwa anazijua siri zote pale ni mama Roika. Ambaye alijua kuwa mwanaye alipona baada ya kupigwa risasi na Ramona. Alifahamu kuwa mtoto wa Rais wa Pakistani ndiye aliyemwokoa mwanaye.

Ramona hakuwa akijua kama Roika anaishi.

Usiku  uliingia Ramona akiwa bado yupo nyumbani kwa mama Roika. Aliamua kutoka nje na kuwaambia walinzi wake, walinzi waliokuwa nje ya nyumba wakimsubiri kuwa waende wakapumzike na waje kumchukua kesho, kwani alihitaji kulala pale pale kwa mama Roika.

Ramona aliamua kukaa pale nyumbani kwa mama Roika kwa usiku mmoja. Maana hakuwa na hamu ya kuondoka mapema. Mama Roika aliandaa chakula ambapo walikaa wote mezani na kula pamoja. Dina alikuwa ni mwenye furaha sana lakini Ramona alikuwa kwenye kifungo kikubwa cha mateso. Baadaye mama Roika aliwaaga na kwenda kulala. Ramona alibaki pale sebuleni pamoja na Dina wakiongea mengi.  Baadaye Dina alimuuliza Ramona swali ambalo, lilimfanya kuwa mnyonge wa hali ya juu. Moto mkali uliwaka ndani ya moyo wake, alihisi maumivu makali zaidi ya risasi.

“Ramona wewe ni wifi yangu?” aliuliza Dina.

Ramona alijifanya hajasikia aliamua kumuuliza.

“Umesemaje Dina?”

“Najua umesikia Ramona. Kama kweli wewe na kaka yangu ni mtu na mpenzi wake, nitafurahi sana.  Yaani nitatamani ndoa yenu ifungwe haraka sana. Ramona naomba usimuache kaka yangu mkiwa wawili mnapendeza sana.”

Hakika maneno hayo yalikuwa taji la miba kwenye moyo wa Ramona.  Pale pale alikumbuka jinsi alivyokuwa akifyatua risasi pindi alipokuwa akimuua Roika. Alitamani ampige Dina kofi lakini hakuweza. Alijikaza kisabuni kupita maelezo.  Alianza kuona kama mateso anayozidi kuyapata ni adhabu kutoka kwa marehemu Roika.

Baadaye alimuaga Dina na kuelekea kulala huko chumbani alilia kilio cha kusaga meno. Kesho ilipofika Ramona aliamua kuwaaga mama Roika pamoja na Dina. Aliwaambia kuwa atarudi wiki mbili zijazo kwani amefurahi kuwa pamoja nao.

Ramona alipanda ndege kurudi nchini Pakistani. Alipofika Pakistani alipokelewa na walinzi wake wengine. Moja kwa moja alielekea katika jumba lao la biashara. Akiwa anapanda ngazi mpiganaji mmoja wa kikundi cha Swaba alimuita na kumuomba waongee. Mpiganaji huyo ndiye yule aliyekuwa ametumwa akauchome moto mwili wa Roika.

Nini kitafuatia, usikose kesho.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU