BARAZANI ENTERTAINMENT KUIKOMBOA TASNIA YA FILAMU

BARAZANI ENTERTAINMENT KUIKOMBOA TASNIA YA FILAMU

513
0
KUSHIRIKI

NA BEATRICE KAIZA


TASNIA ya uigizaji ni moja kati ya fani ambazo zimekuwa zikiwavutia watu wengi kutokana na maudhui yaliyomo ndani yake.

Kutokana na kuwavutia wengi, wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza ili kuhakikisha fani hiyo inafika mbali kama ilivyo katika nchi zilizoendelea.

Tyeoo Barazani Entertainment ni miongoni mwa wadau ambao wamejipanga kufanya mabadiliko kwenye tasnia ya filamu na kutoa ajira kwa vijana mwaka huu.

BINGWA lilikutana na Mkurugenzi Mtendaji, John Kallaghe na kuzungumza naye  kuhusu mikakati yao mwaka huu kwenye tasnia hiyo.

Kallaghe anasema kuwa mwaka huu ni mwaka wa kuleta maendeleo kwenye tasnia ya filamu ili kufika mbali katika ngazi za kimataifa na kutoa ajira kwa vijana.

“Mradi wa Tyeeo Barazani ni miongoni mwa miradi kadhaa ambayo imeanzishwa na taasisi yetu ulioasisiwa tangu mwaka 2013 na unakadiriwa kutoa fursa ya ajira za uhakika kwa vijana takribani 6,000  katika kada zote za filamu mwaka huu,” anasema mkurugenzi huyo.

“Pia kazi itakuwa ikiwafikia mashabiki na wapenzi wa filamu majumbani kwao na kuweza kununua kazi kwa kupitia njia ya simu kwa namba *149*97# ukituma ujumbe mfupi kwa namba hiyo unaweza kununua filamu na kufikishiwa hadi nyumbani kwako kwa wakati,” anaongeza.

Anasema tasnia ya filamu wanaweza kufanya vyema kutokana na kuwa wamejipanga  mwaka huu na ni zamu yao kuifanya tasnia  hiyo  kukaa kwenye mstari.

Kwa upande wa Jacob Stephen maarufu kwa jina la ‘JB’ ambaye ni msanii na mtayarishaji wa filamu hapa nchini, anasema Tyeeo Barazani Entertainment imekuja kuleta mabadiliko ili wasanii  waweze kufanya kazi kwa kujiamini na kuacha kutegemea  kuwashirikisha wasanii wa nje ili kazi zao ziweze kwenda kimataifa.

Anasema hakuna haja ya kuwashirikisha wasanii kutoka nje ili kusaidia kazi zao zifike mbali kwani na wao wanaweza kuzifikisha  na zikawazalishia fedha nyingi zaidi kupitia Tyeeo Barazani Entertainment.

“Kingine niwaase wasanii wenzangu ni kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kutimiza malengo yetu kwa kushirikiana na Tyeeo Barazani Entertainment,’’ anasema JB.

Naye msanii maarufu wa filamu, Single Mtambalike ‘Richie’, anasema kuwa vijana wanatakiwa kujitolea kufanya kazi kwa kushirikiana na Tyeeo Barazani Enteinment ambayo imejitokea kuikomboa tasnia ya filamu kwani ni zamu ya wasanii wa filamu kufanya vema mwaka 2017.

Anasema wameamua kuileta barazani ili kuleta mapinduzi katika usambazaji, kwani sasa hivi kuna wanyonyaji ambao wanajinufaisha wao wenyewe.

“Tumechoshwa na unyonyaji wa wasambazaji waliopo kwani Barazani iko wazi kopi inayouzwa hata ukiwa nyumbani inaonesha kwa kuwa inatumia mfumo wa kisasa wa BVR ambao popote ulipo utajua na utaona fedha zako ni shilingi ngapi kutokana na kopi, mambo ya kupanga foleni dirisha la muhindi yameisha na kukadiriwa kopi”, anasema Richie.

Richie anasema Barazani watafuta mirahaba yote kwani hawatahitaji waonaokodisha na vibanda umiza kuonyesha kazi zinazosambazwa na kampuni hiyo, hiyo yote ili kukwepa uwapo wa kazi kiholela isiyomwingizia msanii au mwandaaji kipato.

Hata hivyo, Richie anasema yale mambo ya filamu ya fulani kwa sababu ni mtu wao ndani ya Barazani hayatakuwapo, wanachoangalia wao ni ubora wa picha na stori.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU