NI AIBU Z’BAR KUWA WASINDIKIZAJI MAPINDUZI CUP

NI AIBU Z’BAR KUWA WASINDIKIZAJI MAPINDUZI CUP

908
0
KUSHIRIKI

MACHO na masikio ya mashabiki wengi wa soka hapa nchini yameelekezwa visiwani Zanzibar ambako kuna michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Michuano hiyo iliyoanza rasmi mwaka 2007, hakuna ubishi kuwa imekuwa msaada mkubwa kwa soka letu tangu kuanzishwa kwake.

Moja kati ya sababu ambayo imekuwa ikitajwa na wadau wengi wa soka juu ya kushuka kwa soka letu ni kuwapo kwa idadi ndogo ya mashindano.

Wadau hao walidai wachezaji wetu wamekuwa wakishiriki mashindano machache, hivyo wamekuwa wakipumzika kwa kipindi kirefu jambo linalosababisha kushindwa kufanya vizuri kimataifa.

Kombe la Mapinduzi limeongeza idadi ya michuano kwa timu zetu zinazotuwakilisha kwenye michuano ya kimataifa.

Mfano, Yanga na Azam zina nafasi nzuri ya kuviweka sawa vikosi vyao kabla ya kuingia kwenye michuano ya kimataifa ya mwaka huu.

Lakini pia, hata zile za Zanzibar hazikuwa na mashindano makini kama hayo ambayo yangewaandaa kukabiliana na michuano ya kimataifa.

BINGWA hatuna shaka kuwa timu vigogo kutoka Zanzibar na Tanzania Bara zinaweza kujipima kupitia mashindano hayo kabla ya kuzama kwenye mashindano ya kimataifa ikiwemo Kombe la Shirikisho na Klabu Bingwa Afrika ambayo inawakabili mwaka huu.

Kwa maana hiyo, sisi BINGWA tunaamini uwepo wa Kombe la Mapinduzi una msaada mkubwa katika kuzisaidia timu za Tanzania kujipima kabla ya kutia nanga kwenye michuano ya kimataifa.

Hata hivyo, bado BINGWA tunaamini kuwa timu za Zanzibar ambazo hushiriki michuano hiyo zilitakiwa kuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

Ni jambo la kusikitisha na kutia aibu kuona timu wenyeji zimeendelea kuwa wasindikizaji huku wageni wakiondoka na kombe mbele yao.

Kwa kipindi chote tangu kuanzishwa kwa Kombe la Mapinduzi, ni timu moja pekee ya visiwani humo iliyotwaa ubingwa. Ni aibu.

Ilikuwa mwaka 2009, ambapo Miembeni ilichukua ubingwa baada ya kuichabanga KMKM mabao 2-0 katika mtanange wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan. Baada ya hapo, timu shiriki za Zanzibar zimeendelea kuwa wasindikizaji wa Kombe la Mapinduzi.

Mbali na kuchukua ubingwa, huo ndio uliokuwa mwisho wa Zanzibar kuwa na mwakilishi kwenye mechi za fainali.

Hiyo inaamisha kwamba, tangu mwaka 2009, ambao Miembeni walikuwa mabingwa, hakuna timu ya Zanzibar iliyofanikiwa kutinga fainali.

Ni kweli timu za Zanzibar zilistahili kuchukua mara moja michuano hiyo inayoandaliwa visiwani humo?

BINGWA tuna shaka kuwa timu za Zanzibar zimekosa mipango madhubuti ya kuhakikisha kombe hilo linabaki nyumbani.

Lakini pia, BINGWA tunakiri kuwa kama Chama cha soka visiwani humo (ZFA), kinatakiwa kujitathmini na kuibuka na mikakati kabambe ya kuziwezesha timu shiriki kutoka visiwani humo. Kuziwezesha ni pamoja na kujipanga kuipa uhai Ligi Kuu Zanzibar ambayo imeonekana kuwa si ya kiushindani.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU