ROMA, DULLY SYKES, RUBBY WALIVYOWASHIKA MASHABIKI HANANASIFU

ROMA, DULLY SYKES, RUBBY WALIVYOWASHIKA MASHABIKI HANANASIFU

605
0
KUSHIRIKI

NA KYALAA SEHEYE


JUZI mashabiki wa muziki kutoka maeneo mbalimbali ya Kinondoni  hususan Hananasifu, walipata uhondo baada ya kupagawishwa na wasanii wanaopiga muziki wa aina tofauti katika tamasha lililoandaliwa na Kituo cha Redio Efm.

Katika tamasha hilo ambalo lilihudhuriwa na mamia ya mashabiki,  wa kwanza kuwapa uhondo huo alikuwa ni mkali  wa muziki wa hip hop mwenye vina vya kuchana maneno makali hasa   kwa wale wanaopenda kuwakandamiza wenzao kwa madaraka yao, Ibrahimu Mussa ‘Roma Mkatoliki’, baada ya kuachia kibao chake chenye maneno ya kutatanisha  yenye mistari ya kuuliza kitu kitamu kinakaa wapi na mashabiki kulipuka kwa shangwe.

Roma alipanda jukwaani baada ya kukaribishwa katika kipindi cha Uhondo kutoka Redio Efm kilichokuwa kikirushwa live kutoka katika viwanja hivyo.

Pia Roma aliweza kuwagawa mashabiki kwa kutaka kujua shangwe ziko wapi huku akiwaambia wakae mafungu matatu akiamini kulia Roma kushoto Darasa na katikati watakaa waumini na wanafunzi na hapo hakitaharibika kitu.

“Usicheze wewe kulia linakaa kanisa, bila shaka kushoto linakaa darasa  katikati nawapata waumini na wanafunzi hapo lazima kiwake na kinuke”, alisema Roma na kushangiliwa na mashabiki waliohudhuria shoo hiyo.

Shoo hiyo iliyombatana na kikosi cha askari polisi waliokuwa na mbwa kiliratibiwa na Kituo cha Redio cha Efm  ambacho kimeamua kufanya vipindi vyake ‘live’ mitaani ili kuwafikia wasikilizaji wake, wakiamini kuwa kwa kufanya hivyo watawapa fursa  kuwafahamu watangazaji wao kuliko kukaa studio bila wao kuwajua vilivyo.

Naye msanii Hellen Geogre ‘Ruby’  naye aliwakonga mashabiki  waliohudhuria  tamasha hilo pale alipoporomosha vibao  vyake  viwili alivyovipa majina ya Shetani ana sura mbili pamoja na Kwiki ambavyo vipo katika mtindo wa Singeli.

Akizungumza kabla ya  kuporomosha vibao hivyo, staa huyo alisema kuwa kwa sasa   ameamua kufanya singeli kwa kuwa yeye ni msanii na anapaswa kuimba chochote kile ambacho kipo na kinachokwenda na wakati.

“Nataka kuendana na wakati ndio maana nimeamua kuimba Singeli kwa sasa huu ndio muziki wa mjini na Kwikwi iko kisingeli na dawa ya Kwikwi maji, nataka kuwaonyesha hiyo kwikwi niliyowapa maji ninayo mimi,” alisema Ruby.

Baada ya kuongea hayo staa huyo ambaye amewahi kutamba na vibao kadhaa vilivyo katika miondoko ya R&B,  alianza kuimba na kucheza sawasawa  huku akishangiliwa  kwa nguvu  jambo ambalo lilimfanya aamini amefunga mwaka kwa ushindi.

Kwa upande wake mkongwe wa Bongo Flave anayetamba na wimbo wa Inde, Abdul Sykes maarufu Dully Sykes, naye hakuwa nyuma kwani alionyesha mbwembwe zake za kufunga mwaka, kama ilivyo kawaida yake alisababisha vurugu kwa mashabiki wake pamoja na wasikilizaji wake baada ya kushuka jukwaani  na kwenda kukata nao viuno vya ‘Inde’ hadi kusababisha polisi waliotumia mbwa kuwatawanya na kumrudisha tena stejini.

Mbali na hilo, Dully alitamba kuwa mwaka huu mashabiki wake wajiandae  akidaia kuwa yeye ni msanii asiyeshuka kiwango na huku akiwatishia nyau wapinzani wake kwamba anakuja kuwapoteza.

“Toka nimeanza sijawahi kupotea kwenye fani hii inaonyesha sikukurupuka ni kipaji na hilo halina mpinzani, sasa wajipange waliovamia fani kwani ninakuja kushika nafasi yangu lazima mtanielewa mimi ndio mkali wao,” alisema Dully.

Naye Meneja wa vipindi wa Efm, Dickson Ponela, alisema kuwa hii ndio itakuwa staili yao na wana imani kabisa kwa kufanya hivyo watazidi kujiweka karibu na mashabiki wao kwa kuwa kipindi si kusikiliza tu redioni.

“Kipindi si kusikiliza redioni watu watakuwa hawawajui watangazaji, tukifanya live mtaani tunatoa fursa kwa watangazaji wetu kujulikana na wasanii wanaotutembelea kuwa karibu na mashabiki wao, pia kuongea na mashabiki na kusikiliza matatizo yao.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU