UKIONA WAMEHAMA TIMU ZAO JANUARI USISHANGAE

UKIONA WAMEHAMA TIMU ZAO JANUARI USISHANGAE

932
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

HIVI sasa vichwa vya makocha wa timu mbalimbali havijatulia kabisa. Tayari presha ya dirisha dogo la usajili la Januari imeshaanza.

Mauricio Pochrettino amejinasibu kuwa hatafanya usajili lakini huenda akabadili mawazo yake kadiri siku zinavyokwenda.

Jose Mourinho naye ametangaza kuwa hataongeza straika mpya kwenye kikosi chake. Hata hivyo, naye Mourinho hatabiriki.

Lakini pia, tayari Arsenal wameshamkosa Julian Draxler ambaye ametua zake PSG, hivyo huenda wakali hao wa London wakasaka mbadala.

Hebu cheki timu vigogo hizi zitakavyoachana na mastaa wao ikiwa ni sehemu ya kuviboresha vikosi vyao.

Man City/Tottenham

Hatima ya Yaya Toure pale Etihad bado haijaeleweka licha ya uwezo mkubwa aliounyesha hivi karibuni. Kwa upande wa Tottenham, Kevin Wimmer hana nafasi ya kubaki klabuni hapo hasa baada ya kuzidiwa kete na Eric Dier. Huenda akatimkia Southampton ambayo inajiandaa kumpoteza Virgil van Dijk.

Liverpool

Ni wazi Mamadou Sakho yuko njiani kutimka Anfield. Beki huyo hajacheza hata mechi moja na aliwahi kufanya mazoezi na timu ya vijana kutokana na utovu wa nidhamu.

Kwa sasa haonekani kuwa kwenye akili ya kocha Jurgen Klopp na huenda akakubali ofa kutoka Juventus au Paris Saint-Germain ambazo zimekuwa zikimmezea mate.

Mwingine ni Tiago Ilori ambaye pia amekuwa benchi kwa msimu mzima.

Alikaribia kuondoka Agosti mwaka jana na iliposhindikana alitakiwa kufanya mazoezi na timu ya vijana.

Saini ya beki wa kati huyo inafukuziwa na Frankfurt, Freiburg, Valencia na Granada.

Everton

Nyota Oumar Niasse aliigharimu Everton kiasi cha pauni milioni 13.5, lakini amekuwa mzigo klabuni hapo.

Kilichofuata ni kushuka kiwango na kupelekwa kwenye kikosi cha vijana wenye umri wa chini ya miaka 23.

Kwa sasa ni majeruhi na hata hivyo haionekani kama ataweza kuhimili ushindani wa namba kwenye kikosi cha kocha Ronald Koeman. Moja ya klabu zinazotolewa udenda na saini ya Msenegal huyo ni Trabzonspor ya Uturuki.

 Mchezaji mwingine anayeweza kuondoka Januari pale Everton ni Darron Gibson, ambaye alipewa mkataba wa miaka miwili wakati wa majira ya kiangazi.

 Tangu hapo, hajaingia kwenye kikosi cha kwanza hata mara moja na sasa yuko nje kikosi cha vijana wa umri wa chini ya miaka 23.

Leicester

Wanaoweza kuondoka Jeffrey Schlupp, Leonardo Ulloa, Matty James na Bartosz Kapustka. Kwa upande wake, Schlupp anayecheza nafasi ya beki wa kushoto anawaniwa na West Brom.

Straika Ulloa anafukuziwa na Sunderland huku saini ya msugua benchi Matty James ikisakwa na Aston Villa.

Baada ya kununuliwa kwa pauni milioni 7.5, Kapustka ameshindwa kuthibitisha ubora wake kwani mpaka sasa hajacheza hata mchezo mmoja akiwa kwenye kikosi cha kwanza.

Miongoni mwa klabu zinazomtaka ni Preston, Barnsley na Bristol City.

Chelsea

Wengi wanamini kuwa Branislav Ivanovic ataondoka hasa baada ya beki huyo kukosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kocha Antonio Conte.

Imeelezwa kuwa Juventus wako mstari wa mbele katika kuifukuzia huduma ya Mserbia huyo.

Pia, John Obi Mikel ameshindwa kung’ara chini ya Conte na saini yake imekuwa ikiwindwa na Wachina, Inter Milan na Fenerbahce.

 Kwa upande mwingine, wachambuzi wa soka wanamtaka Ruben Loftus-Cheek kutimka Stamford Bridge. Kama ilivyo kwa Obi Mikel na Ivanovic, staa huyo ameshindwa kumshawishi mkufunzi Conte.

Manchester United

Ni wazi Memphis Depay, Morgan Schneiderlin na Bastian Schweinsteiger hawana jipya Old Trafford.

Depay hajaingia kwenye kikosi cha kwanza cha Jose Mourinho na tayari ameshapewa ruksa ya kuondoka.

Everton wanamtaka na Man United wako tayari kupokea hata nusu ya kiasi cha pauni milioni 25 waliyotumia kumsajili kutoka PSV Eindhoven.

Schneiderlin alinunuliwa na Louis van Gaal kwa pauni milioni 24 akitokea Southampton.

Ameshindwa kujihakikishia namba kwenye kikosi cha Jose Mourinho na amekuwa nyuma ya Marouane Fellaini.

Tayari West Brom wameshatangaza ofa yao ya pauni milioni 13 na Everton nao wanamsikilizia.

Schweinsteiger ameshindwa kuingia kwenye mipango ya Mourinho na kinachosubiriwa kwa hamu ni safari yake ya kwenda kumalizia soka nchini Marekani.

Arsenal

Inaelezewa kuwa Alex Oxlade-Chamberlain hana furaha pale Emirates. Taarifa zilizopo ni kwamba, huenda akaondoka zake.

Pia bado kumekuwa na mvutano kati ya Arsenal na mastaa wake Mesut Ozil na Alexis Sanchez. Nyota hao wamegoma kusaini mkataba mpya wakitaka kuongezewa mishahara.

Huenda ikatokea kwa Sanchez kuondoka kwani tayari kuna tetesi kuwa anatakiwa na moja ya klabu za China ambayo iko tayari kumpa mshahara mnono wa pauni 400,000 kwa wiki.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU