BUSHIR AFUATA NJIA ZA OMOG

BUSHIR AFUATA NJIA ZA OMOG

1003
0
KUSHIRIKI

NA MAREGES NYAMAKA

KOCHA mkuu mpya wa Mwadui, Ally Bushir, amekula sahani moja na kocha wa Simba, Joseph Omog, baada ya kushinda mechi tatu mfululizo za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Bushir aliyeanza kuifundisha timu hiyo mzunguko wa pili baada ya kocha mkuu aliyemtangulia Jamhuri Kihwelu ‘Julio’,  kuachia ngazi, ameonekana kuanza vizuri baada ya kuiwezesha kupata pointi tisa kutokana na mechi tatu sawa na Omog ambaye ameiwezesha Simba kushinda mfululizo.

Katika mechi tatu Bushir aliiongoza Mwadui kushinda mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar, kisha bao 1-0 na Toto Africans na baadaye bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.

Simba walianza mzunguko wa pili kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda, lakini waliibuka na ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu na baadaye ushindi wa bao 1-0 kwa Ruvu Shooting.

Katika hatua nyingine, kocha wa Ndanda, Hamimu Mawazo, amepumua baada ya kuwapo kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomwezesha kufanyia kazi upungufu wa kikosi chake.

Mawazo alisema ushiriki wa timu za Tanzania Bara, Azam, Simba na Yanga kwenye michuano hiyo imempa muda wa kufanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mechi tatu walizocheza za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Katika hizo, Ndanda walipoteza zote baada ya kufungwa na Simba, Mtibwa Sugar na Yanga kwenye mechi zao zilizochezwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Nangwanda Sijaona na Uhuru, jijini Dar es Salaam.

“Niseme tu haya mapumziko ya wiki mbili kutokana na michuano ya Kombe la Mapinduzi, kwangu imekuwa ahueni  kupata nafasi nzuri ya kufanyia kazi  upungufu uliojitokeza  kwa kujenga kikosi bora,” alisema Mawazo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU