DANISE UMEZAA KIPENZI CHA WENGI MILTON KEYNEYS

DANISE UMEZAA KIPENZI CHA WENGI MILTON KEYNEYS

588
0
KUSHIRIKI

NA HALID MTUMBUKA

MATATIZO yaliyotokana na unywaji wa pombe yaliitesa sana afya ya mwanamama wa Kiingereza, Danise.

Licha ya raha zote zilizopo katika mitaa ya Jiji la Milton Keynes, sifikiri kwamba baada ya matatizo hayo aliifurahia Milton Keynes kama alivyokuwa na kipenzi chake Kenny kutoka nchini Nigeria.

Wakati wakiwa wapenzi hakuwahi kuwaza kama ipo siku atakuja kuteseka kiasi alichoteseka, fimbo ya maisha haina huruma!

Huyu ndiye aliyebeba kiumbe ndani ya tumbo lake na baada ya miezi tisa kiumbe kilizaliwa na kupewa jina la Bamidele Jarmaine Alli, sisi tunamfahamu zaidi kama Dele Alli.

Hali ya mama yake ilimlazimu kutengana naye na kwenda kulelewa nje ya familia yake. Hiyo ilikuwa ni Jiji la Milton Keynes nchini Uingereza.

Hakuwa na baba wala mama kipindi hicho. Aliifikiria sana siku ya Aprili 11, 1996, siku aliyozaliwa na alitamani pia kuwa na kipenzi chake, mama yake Danise pengine na baba yake lakini dunia iliwatenganisha.

Kitu pekee kilichosalia kwenye maisha yake ni kipaji chake. Aliamua kuwekeza huko baada ya kujiunga na timu ya Milton Keynes Don hatimaye jicho la Tottenham Hotspur likamuona mwaka 2015. Hawakutaka kujiuliza juu ya maamuzi yao, walimsajili kwa uhamisho wa awali pauni milioni 5, historia ya waliyofanikiwa haifurahishi machoni wala masikioni.

Miezi 18 baada ya kusajiliwa na Spurs anafunga mabao mawili kwenye usiku muhimu sana kwa timu yake na ushindi muhimu mno kwao ndani ya uwanja wao wa nyumbani, White Hart Lane.

Wakati huu ndiyo unaweza kuyakumbuka majina ya watu kama, Matt Le Tissier. Usiku ule nikiwa nimejikunyata nakiangalia kichwa chake kilichokaza hasa mishipa ya nyuma ya shingo yake na kufunga mabao mawili, nililikumbuka jina hilo.

Historia ya Matt Le Tissier kwenye mchezo kati ya Southampton dhidi ya Liverpool, mwaka 1993 ilinijia usiku ule kwani Dele Alli alikuwa anafikisha idadi ya mabao 20 baada ya kucheza michezo 52 akitumia miezi 18 tangu aweke saini za kucheza White Hart Lane, hili ni tukio kubwa mno kwangu usiku ule kwa kijana huyu mwenye umri wa miaka 20.

Hakika Danise alikizaa kipenzi cha wengi si tu kwenye mitaa ya Milton Keynes, bali Uingereza na dunia nzima ya wapenda mchezo wa soka, alimfanya hata Mauricio Pochettino aufurahie ule mfumo wake wa usiku ule, 3-4-2-1 huyu jamaa huwa anafanya vitu vya ajabu sana anapopambana na mpinzani wake.

Miaka yake 20 tayari Dele Alli anatajwa kule Santiago Bernabeu kwa rais mwenye usia na urafiki wa kudumu dhidi ya yeyote anayeshindwa kuyatimiza majukumu yake ipasavyo, Florentino Perez. Wenyewe wameiweka imani yao kwake na kwa sababu zao maalumu.

Wamepania, wanachokisubiri ni kile kipindi watakapomaliza adhabu yao ya kutosajili na itamalizika msimu ujao. Uhakika wa kumpata Dele Alli unakuja baada ya kuwa na mahusiano mazuri ya kibiashara kati ya wawili hao, yaani Spurs na Real Madrid.

Real Madrid ilimsajili, Luka Modric kutoka Spurs tukasema dili limekamilika, baadaye wakamsajili Gareth Bale na pia tukatamka hivyo hivyo, ni kitu kimoja tu kitakachotuzuia tusitamke hivyo nacho ni uhitaji wa Real Madrid kwa Dele Alli vinginevyo kwa uwezo wa huyu mtoto wa Danise, hakuna zaidi ya hicho kitakachotuzuia kutamka dili limekamilika.

Wakati sisi tukitamka hivyo, ile mitaa yote ya Jiji la Milton Keynes huenda wakamtungia wimbo huyu, Bamidele ‘Dele’ Jarmaine Alli.

Ni hicho tu ninachowadai watu wa Milton Keynes kwa kijana huyu, ni hicho tu ninachowadai wanakwaya wa The Church of Christ the Cornerstone.

Kwanini nisiwadai wakati yeye ameweza kufikisha idadi ya mabao 20 kwenye Premier League ndani ya michezo 52 pekee?

Paul Scholes alifikisha idadi hiyo ya mabao akiwa amecheza michezo 74, David Beckham alifikisha idadi hiyo ya mabao baada ya kucheza michezo 90 na hata yule Frank Lampard alifikisha idadi hiyo baada ya kucheza michezo 140.

Hata rafiki yake kipenzi na wa siku nyingi, Eric Dier, hawezi kupinga kwamba Dele Alli yupo kwenye kiwango cha juu hivi sasa. Namba hazidanganyi! Unahitaji kusimuliwa nini tena kwa Dele Alli? Kiungo mwenye kila sifa ya kuwaniwa na Real Madrid.

Si tu kwa kuwazuia Chelsea kufikisha idadi ya kushinda michezo 14 mfululizo kwenye Premier League kwa kufunga mabao mawili, lakini alipiga mashuti matatu siku ile, mawili yalilenga lango na moja halikulenga lango.

Alipiga pasi 27 kati ya hizo 19 zilifika kwa walengwa ambazo ni sawa na asilimia 70 ya pasi zilizopigwa na miguu yake.

Kwanini Florentino Perez macho yasimtoke? Aliishi kama alivyotaka Pochettino usiku ule, aliamua kubadilisha kidogo tu kutoka 3-4-3 na kuweka 3-4-2-1 akiamini kwamba wapo watu watakaomfanyia kazi yake na kazi ilifanyika.

Dele kama ‘forward’ wa kulia alifanya majukumu yake ipasavyo hasa kwenye kushambulia na ndiyo maana aliibuka kama nyota wa mchezo siku ile.

Dele Alli anaweza kuwa staa mpya wa Real Madrid.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU