ETI ONYANGO AMECHUKUA TUZO, KASEJA, MAPUNDA WAMEZEEKA!

ETI ONYANGO AMECHUKUA TUZO, KASEJA, MAPUNDA WAMEZEEKA!

998
0
KUSHIRIKI

NA HUSSEIN OMAR

HATIMAYE ile hafla ya utoaji tuzo za Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) ilifanyika juzi jijini Abuja, Nigeria.

Staa wa Leicester City, Riyard Mahrez, ndiye aliyenyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika ambapo mshindi wake alikuwa akisubiriwa kwa hamu na idadi kubwa ya mashabiki wa kandanda.

Winga huyo wa Leicester alitwaa tuzo hiyo akiwapiku Pierre-Emerick Aubameyang na Sadio Mane.

Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilinyakua tuzo ya Klabu Bora Afrika huku mkuu wao wa benchi la ufundi akipewa ya Kocha Bora barani humu.

Binafsi nilifurahishwa zaidi na kitendo cha mlinda mlango Denis Onyango wa Uganda kuwa mmoja ya waliong’ara usiku huo.

Kwa ambao hawakupata muda wa kufuatilia, Onyango mwenye umri wa miaka 30, alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi za Ndani.

Mganda huyo alichukua tuzo hiyo baada ya kuwabwaga Khama Billiat anayecheza naye pale Mamelodi na Rainford Kalaba wa Zambia.

Baada ya kumalizika kwa hafla hiyo, nilibaki na maswali mengi sana hasa kila nilipoifikiria tuzo ya Onyango.

Fikira zangu zilitua moja kwa moja kwa walinda mlango mahiri Juma Kaseja na Ivo Mapunda.

Nilipojaribu kulinganisha umri wa watatu hao niligundua kuwa hawapishani sana.

Kwa msaada wa mitandao, nilibaini kuwa Onyango ana umri wa miaka 30, Ivo ana umri wa miaka 33 na Kaseja amezaliwa miaka 32 iliyopita. Kwa mantiki hiyo, walinda mlango hao hawapishani sana.

Kwa maana nyingine, Onyango ni mlinda mlango wa muda mrefu kama walivyo akina Kaseja na Ivo.

Lakini sasa, nini kinachosababisha Mganda huyo kuwa mbele yao usiku ule jijini Abuja?

Wakati Onyango ndiyo kwanza anaanza kuuza jina lake kwa tuzo ya Caf, tayari akina Kaseja wameshamaliza maisha yao ya soka.

Ndiyo, hakuna namna unayoweza kuamini kuwa kuna siku Kaseja au Ivo watarudi kwenye ubora waliowahi kuwa nao.

Kaseja amejiunga na Kagera Sugar ya Bukoba na mwenzake Ivo hana timu kwa sasa.

Itakumbukwa kuwa wakati Onyango alipokuwa akija hapa nchini akiwa na kikosi cha Sports Club Villa, alikuwa na tofauti gani na Kaseja au Ivo?

Onyango hakua na uwezo wa kutisha sana kuliko walinda mlango tuliokuwa nao na kama aliwazidi basi ni kwa kiwango kidogo mno.

Kwa kiwango ambacho Onyango alikuwa akimkuta nacho Kaseja pale Msimbazi miaka kadhaa iliyopita, leo hii tungezungumza mengine.

Hakuna ubishi kuwa Kaseja alikuwa moto wa kuotea mbali katika kuokoa michomo, lakini je, nini kilichofuata?

Ni kipindi kile ndipo alitakiwa kujiongeza na kutafuta njia ya kwenda kucheza soka nje ya nchi.

Lakini pia, Ivo aliwahi kuwa kwenye ubora wa hali ya juu miaka michache iliyopita leo hii hakuna shabiki wa soka anayemzungumzia. Amepotea.

Leo hii Onyango anakipiga Afrika Kusini na kuchukua tuzo hiyo ya Caf huku Kaseja akiicheza Kagera! Ni aibu kwa Kaseja na hata kwa soka letu.

Nini klilichosababisha tofauti kubwa kati ya Onyango na akina Kaseja?

Hakuna ubishi kuwa wachezaji wa hapa Tanzania huwa hawana utamaduni wa kujituma. Wengi huishi kimazoea na matokeo yake ndiyo hayo tuliyoyaona.

Kitu kingine mashabiki na makomandoo wa timu zetu za hapa Bongo wamekuwa na kasumba ya kuwatoa wachezaji mchezoni kwa madai wamezeeka.

Hii ni mbaya sana katika mustakabali wa soka letu kupiga hatua moja mbele, napenda kutoa rai kwa wachezaji ambao bado wana uwezo wa kucheza soka wajitume kama ilivyo kwa Onyango.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU