LEICESTER TUPA KULE! NANI KUWA MWANAMUME WA EPL 2016-17?

LEICESTER TUPA KULE! NANI KUWA MWANAMUME WA EPL 2016-17?

646
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

MSIMU uliopita mpaka kufikia hatua hii, Leicester walikuwa kwenye nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England.

Msimu huu mambo yamegeuka, timu vigogo zimeonekana kujizatiti huku Leicester wakionekana hawana chao.

Hebu cheki hali ilivyo hadi sasa ambapo tayari timu vigogo zimeshajiweka kwenye mazingira ya kuchukua ubingwa zikiwa zimeshashuka dimbani mara 20.

  1. Chelsea

Wakali hao wa Stamford Bridge wameshajikusanyia pointi 49 na wameonekana kung’ang’ania kileleni mwa msimamo wa ligi.

Udhaifu wao

Mfumo wa sasa wa 3-4-3 anaotumia Kocha Antonio Conte, unaweza kuigharimu timu hiyo ikiwa washambuliaji wake wa pembeni watakuwa majeruhi.

Pia, Conte anatakiwa kuufanyia kazi uzembe wa kikosi hicho kuibuka na ushindi wa bao moja katika michezo mingi.

Vipi kocha waliyenaye?

Ujio wa Conte ndani ya Stamford Bridge umeonekana kuibadilisha Chelsea kwa kiasi kikubwa.

Mfumo wake wa 3-4-3 umekuwa chachu ya mafanikio ya klabu hiyo ya bilionea Roman Abramovich.

Mafanikio ya Conte alipokuwa Italia ambapo alinyakua mataji matatu ya Serie A, ni nguzo imara kwa Chelsea. Ni wazi Chelsea wanaweza  kutembelea mafanikio ya Conte.

Vipi kuhusu majeruhi?

Mpaka sasa, Chelsea ni moja kati ya timu mbili pekee za Ligi Kuu England ambazo hazina majeruhi.

Hiyo imekuwa ikimpa wakati mgumu Conte kuchagua kikosi cha kwanza.

Mastaa tegemeo

Ingawa msimu huu Chelsea wameonekana kucheza kitimu, ni wazi kuwa mchango wa Eden Hazard na Diego Costa utabaki kuwa muhimu kwa kikosi hicho.

Lakini pia, Chelsea inapaswa kuendelea kunufaika na ubora wa NG’olo Kante, katika eneo la kiungo.

Mechi zilizobaki

Tayari Chelsea imeshamalizana na Tottenham. Ni Arsenal, Liverpool, Man United na Man City zilizobaki.

Kushinda mechi hizo kutaifanya Chelsea kujenga hali ya kujiamini zaidi.

  1. Liverpool

Msimu huu Liverpool wamejipanga chini ya kocha Mjerumani, Jurgen Klopp. Mpaka sasa wameshaweka kibindoni pointi 44.

Udhaifu wao

Ukweli ni kwamba kama si uzembe wa walinda mlango basi Liver wangekuwa mbali msimu huu.

Kocha Klopp amejaribu kuwatumia Loris Karius na Simon Mignolet kwa nyakati tofauti, lakini hakuna aliyeweza kutibu tatizo.

Lakini pia, watahitaji uwepo wa Daniel Sturridge katika safu ya ushambuliaji.

Vipi kocha waliyenaye?

Klopp ni kocha mwenye mafanikio katika klabu zote alizopitia. Cha kushangaza zaidi ni utamaduni wake wa kutumia fedha kiduchu kujenga kikosi imara.

Mfano mzuri ni pale Borussia Dortmund  ambapo alikifanya kikosi hicho kuwa tishio barani Ulaya huku akiwa ametumia bajeti ndogo. Amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Liver na wachambuzi wa soka wanatabiri kuwa huenda akawa nembo ya klabu hiyo siku moja.

Vipi kuhusu majeruhi?

Mastaa Sturridge na James Milner waliumia wakati wa Sikukuu za Krismasi na mwaka mpya, lakini watarejea hivi karibuni.

Joel Matip na Philippe Coutinho wako mbioni kurejea kikosini. Ni Danny Ings pekee anayetarajiwa kuwa nje kwa muda mrefu.

Mastaa tegemeo

Huku Adam Lallana akionekana kushuka kiwango, Sadio Mane na Roberto Firmino, wamekuwa nguzo imara kwenye kikosi cha timu hiyo.

Lakini pia, ni ngumu kuusahau mchango wa Mbrazil, Philipe Coutinho, kwenye kikosi cha Liver msimu huu.

Kiwango chake cha juu kimesababisha saini yake kuwatoa udenda mabingwa wa La Liga, Barcelona.

Ratiba inawabeba au inawatupa?

Katika timu 10 za juu, Liver itacheza mechi sita ikiwa nyumbani Anfield.

  1. Tottenham

Vijana hao wa kocha Mauricio Pochettino, si wa kupuuzwa kwenye mbio za ubingwa. Wanakamata nafasi ya tatu wakiwa na pointi 42.

Mastaa tegemeo

Idadi kubwa ya wachezaji wa Totenham wameonekana kuwa kwenye ubora wa hali ya juu msimu huu.

Mlinda mlango, Hugo Lloris, mabeki  Toby Alderweireld, Kyle Walker na Danny Rose, wamekuwa siri ya mafanikio kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Dele Alli na Harry Kane, nao wamekuwa silaha muhimu kwenye safu ya ushambuliaji.

Udhaifu wao

Ni muda mrefu umepita tangu Spurs walipokuwa kwenye kinyang’anyiro cha kufukuzia ubingwa wa EPL.

Msimu uliopita, walimaliza mbio hizo wakiwa nafasi ya tatu huku taji likitua kwa Leicester City.

Kocha waliyenaye

Ni mmoja kati ya makocha walioibuka ghafla na kujijengea heshima kubwa England.

Jina la Muargentina huyo lilianza kuvuma akiwa na kikosi cha Southampton na kuanzia hapo amekuwa moto wa kuotea mbali mpaka alipotua White Hart Lane mwaka 2014.

Majeruhi

Mbali na Erik Lamela, kikosi cha Spurs kimeonekana kupitiwa mbali na balaa la majeruhi.

Ratiba inawabeba au inawaua?

Mpaka sasa Pochettino hajafungwa na mahasimu wao wa jijini London, Arsenal. Atakuwa na kibarua cha kurudiana na Gunners ifikapo Aprili mwaka huu.

  1. Man City

Matajiri hao wa jijini Manchester wanalingana pointi na Spurs na ni tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa tu inayowatofautisha katika nafasi ya msimamo.

Udhaifu

Wachambuzi wanaamini aina ya wachezaji waliopo Man City hawaendani na Pep Guardiola. Safu ya ulinzi ya timu hiyo ni kimeo hasa kile kilichotokea katika kichapo cha mabao 4-2 kutoka kwa Leicester.

Bado kipa Claudio Bravo, hajaonekana kuziba pengo la Joe Hart.

Kocha waliyenaye

Guardiola yuko kwenye wakati mgumu kwa sasa pale England, lakini ni ngumu kupingana na uwezo wake.

Katika misimu yake saba katika maisha ya soka, Mhispania huyo ameshinda makombe ya ligi kuu mara sita.

Majeruhi

Nahodha Vincent Kompany amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara. Ilkay Gunodgan, naye atakuwa nje kwa kipindi kirefu huku pia Man City ikiwakosa Leroy Sane na Fabian Delph wanaouguza majeraha.

Fernandinho anakabiliwa na adhabu ya kutocheza mechi baada ya kupewa kadi nyekundu mbili.

Mastaa tegemeo

Wakiwa na Sergio Aguero, Kevin De Bruyne na David Silva, Man City wanajivunia safu yao ya ushambuliaji.

  1. Arsenal

Mpaka sasa Washika bunduki hao wa Emirates wanashika nafasi ya tano wakiwa na pointi zao 41.

Udhaifu

Bado Arsenal wameonekana waoga kwenye mechi dhidi ya vigogo. Lakini pia, safu ya ulinzi ni tatizo. Kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana, Arsenal ilishindwa kuzuia nyavu zao kutikiswa katika michezo yote 12 waliyoshuka dimbani.

Kocha waliyenaye

Kumekuwa na mgawanyiko wa maoni kutoka kwa mashabiki wa Arsenal kuhusu kocha wao, Arsene Wenger. Wapo wanaoamini anatakiwa kubaki na kuna kundi lisilomhitaji.

Lakini ikiwa huu ni mwaka ambao mkataba wake utamalizika, ni mashabiki wachache wanaomhitaji.

Majeruhi

Santi Cazorla, Francis Coquelin, Theo Walcott, Mathieu Debuchy, Per Mertesacker, Danny Welbeck na Mesut Ozil, wako nje.

Mastaa tegemeo

Hakuna ubishi kuwa Arsenal wanamhitaji majeruhi Santi Cazorla kikosini.

Katika mechi ambazo Cazorla ameanza msimu huu, Arsenal walikuwa na wastani wa asilimia 86 kushinda. Bila Mhispania huyo, sasa Arsenal wanabaki na asilimia 46 ya kushinda.

Mbali na hao, pia Arsenal inawategemea Alexis Sanchez na Mesut Ozil.

Mechi zilizobaki

Arsenal watakuwa na kibarua kizito kuzifuata Chelsea, Liver na Spurs. Lakini itakuwa nyumbani Emirates kucheza na Man United na Man City.

  1. Man United

Wakali wa Old Trafford wana pointi 39 walizovuna katika michezo 20.

Udhaifu

Safu ya ulinzi imekuwa ikifanya makosa ya kizembe. Lakini pia, wamekuwa wakipoteza pointi katika michezo ya nyumbani ambayo mingi huwa wana uwezo wa kushinda.

Kocha waliyenaye

Hivi karibuni kocha, Jose Mourinho, alidai kufurahia kuifundisha Man United. Ni kocha mwenye mafanikio makubwa ikiwamo kunyakua mara mbili taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Majeruhi

Nahodha Wayne Rooney na Luke Shaw, wako nje huku orodha hiyo ikimjumuisha pia James Wilson.

Mastaa tegemeo

Zlatan Ibrahimovic, Paul Pogba wanaonekana kutokana na Juan Mata na Michael Carrick wanaonekana kuwa tegemeo pale Old Trafford ingawa Henrikh Mkhitaryan amefufuka.

Mechi zilizobaki

Katika mechi za mwisho wa ligi, Man United watavaana na Chelsea, Arsenal na Tottenham. Man United wanatakiwa kujiandaa kwa kuweka mazingira mazuri katika michezo ya sasa dhidi ya vibonde.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU