SAVIO: HAKUNA WA KUTUNG’OA KILELENI RBA

SAVIO: HAKUNA WA KUTUNG’OA KILELENI RBA

431
0
KUSHIRIKI

NA SHARIFA MMASI

MICHUANO ya Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), mzunguko wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake, inatarajiwa kutimua vumbi Januari 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Lengo la ligi hiyo yenye msisimko wa hali ya juu, ni kuibua vipaji kwa wachezaji wa timu mbalimbali shiriki, pamoja na kumpata bingwa upande wa wanaume na wanawake atakayeshiriki michuano ya Taifa (NBL) hapo baadaye.

Tayari shamra shamra kuelekea RBA zimeanza kuonekana kwa baadhi ya timu zikiwamo za Donbosco upande wa wanaume ni Savio na wanawake Don Bosco Lioness.

BINGWA limekuwa likipiga kambi kwenye Uwanja wa Donbosco uliopo Upanga, jijini tangu siku ya kwanza walipoanza maandalizi kuelekea RBA.

Katika kambi hiyo, liliweza kufanya mahojiano na watu mbalimbali akiwamo nyota wa kikapu nchini, Muhammed Yusuph, ambaye pia ni kocha mkuu wa klabu ya wanawake ya Donbosco Lioness.

Lengo la mahojiano hayo lilikuwa ni kutaka kujua mipango yao kuelekea RBA na namna walivyojipanga kutetea taji la ubingwa msimu huu wa mwaka 2017.

BINGWA: Inakumbukwa ligi ya RBA iliyopita nyinyi ndio mabingwa watetezi, mmejipangaje kuhakikisha mnatetea taji lenu lisinyakuliwe na timu nyingine?

Muddy: Tunajipanga kikamilifu kuhakikisha kombe linabaki Don Bosco, ndio maana tulianza mazoezi mapema mno kujihakikishia ubingwa msimu huu.

BINGWA: Ni kweli mazoezi kwa wakati pekee ndiyo sababu itakayowafanya mng’ang’anie kiti cha uongozi RBA msimu huu?

Muddy: Hapana, sisi kama timu ya Savio tunahakikisha wachezaji wote wanafuata ratiba kama ilivyopangwa pamoja na nidhamu ndani na hata nje ya uwanja.

BINGWA: Je, unadhani kuna timu yoyote inayoshiriki RBA itawakosesha amani ya kuchukua kombe msimu huu?

Muddy: Mhhh kiukweli hakuna timu hata moja inayotutisha, sisi tunajiamini na tunajipanga kuendeleza umwamba zaidi na zaidi.

BINGWA: Timu gani inawapasua kichwa sana mnapokutana nayo kwenye michuano mbalimbali hususani hii ya RBA?

Muddy: Hofu yetu kubwa ipo kwa ndugu zetu JKT Mgulani, kwa sababu tuko nao karibu sana na wanazijua mbinu zetu tunazotumia katika mazoezi.

BINGWA: Nini matarajio yenu msimu huu katika ligi ya RBA?

Muddy: Matarajio yetu makubwa ni kuhakikisha hatutoi nafasi kwa timu yoyote kutufunga hatimaye tutetea taji letu la ubingwa.

Muddy: Tukirudi upande wa timu yako ya wanawake unayoifundisha ya Don Bosco Lioness, kipi kinawapa jeuri kuelekea RBA?

Muddy: Kwanza kabisa kikosi changu kipo imara, niseme tu mazoezi tunayoendelea nayo na viwango walivyonavyo wachezaji wangu ndio inatupa jeuri ya kuwanyang’anya Vijana Queens kombe mwaka huu.

BINGWA: Tangu kuanza mazoezi mpaka sasa ni wachezaji wangapi wamekumbana na majeraha?

Muddy: Tunamshukuru Mungu mpaka sasa hakuna mchezji yeyote aliyepata jeraha kubwa la kututia hofu kuelekea RBA, yaliyopo ni madogo madogo tu na ya kawaida.

BINGWA: Kitu gani hukuridhishwa nacho kwenye ligi msimu uliopita?

Kusiga: Kwanza kabisa Chama cha Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD) tayari wameshafanya uchaguzi na msimu huu RBA itaendeshwa na viongozi wapya, sitaki sana kulizungumzia hilo lakini tunatarajia uwapo wa maboresho ya aina yake.

BINGWA: Upi ushauri wako kiujumla?

Muddy: Kiujumla napenda kuwashauri viongozi mbalimbali wa timu kuhakikisha wanafuata sheria za kikapu, wachezeshaji kutenda haki bila kuwa na ubaguzi wa timu yoyote na mashabiki wajitokeze kwa wingi kwani mchezo wa kikapu unaelekea kurudi katika hali yake ya zamani.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU