BUSS BALL MCHEZO UNAOKUWA KWA KASI MORO

BUSS BALL MCHEZO UNAOKUWA KWA KASI MORO

345
0
KUSHIRIKI

NA NYEMO MALECELA, MOROGORO

ULISHAWAHI kusikia soka la mezani? Nadhani wengi wetu tumesikia lakini hatujui ni mchezo wa aina gani. Mchezo huu ni maarufu sana na unakuwa kwa kasi hivi sasa na unajulikana kwa jila la ‘Buss Ball’.

BINGWA limefanikiwa kukuletea uhondo wa soka hili baada ya kutembelea Gymkhana ya Morogoro wikiendi hii, ambako ndiko linakochezwa kwa wingi na watumiaji wa viwanja vya michezo vya Gymkhana.

Hili ni soka linalochezwa mezani, linatumia sheria 17 za soka sawa na soka la uwanjani. Tofauti yake soka hili linachezwa katika meza maalumu ambayo ina midoli 22 iliyochomekwa kwenye miti maalumu ya kuchezea. Midoli hii ni sawa na idadi ya wachezaji wa timu mbili za soka la uwanjani.

Yaani kila timu inakuwa na wachezaji 11 ndani ya uwanja (mezani), lakini tofauti yake na soka la uwanjani ni kwamba wachezaji hawa midoli hawawezi kucheza bila kuwepo wachezaji binadamu pembeni mwa meza.

Wachezaji hawa binadamu wanaweza kuwa wawili kwa kila timu au mmoja kwa kila timu. Endapo wachezaji binadamu atakuwa mmoja basi atahakikisha achezesha wachezaji wote wa timu yake kwa kushika miti iliyochomekwa wachezaji midoli wa uwanjani.

Lakini kama wachezaji hawa binadamu watakuwa wawili kwa kila timu basi mchezaji mmoja binadamu atacheza nafasi ya golikipa kwa kuhakikisha anamchezesha mdoli golikipa anazuia mpira usiingie langoni mwa timu yake.

Katika soka hili muda si kipengele muhimu badala yake ili mchezo uweze kumalizika inatakiwa timu moja itangulie kuifunga timu pinzani jumla ya mabao 10 na ndipo pointi zitahesabiwa kuwa ni 10-(…) jumla ya mabao yatakayokuwa yamefungwa na timu pinzani.

Mchezo huo hauna mwamuzi wala benchi la ufundi bali una mashabiki sawa na ilivyo soka la uwanjani. Ni mchezo ambao wachezaji wake wakishapangwa na kocha ambaye ndiye mtengeneza meza (uwanja) haubadilishwi mfumo wa uchezaji hadi meza hiyo iharibiwe na kutengenezwa upya.

Utamu wa mchezo huu ni kwamba, wachezaji binadamu ndio hujibatiza majina ya timu. Na kuhakikisha wanaziwezesha timu zao kufanya vema ili kuepuka zomeazomea za wapinzani.

Cha kufurahisha katika viwanja hivyo vya Gymkhana Morogoro, soka hili halichezwi na wageni pekee, kwani hata watoto wanaotoka mtaani katika mji wa Manispaa ya Morogoro tayari wameshajifunza jinsi ya kulicheza. Wamekuwa na upinzani mkali kama ilivyo kwa mashabiki wa soka la uwanjani.

Christopher Nikitasi ni Mwenyekiti wa klabu ya Gymkhana, anasema mchezo huu unawafanya wachezaji hasa watoto wanaotoka katika mitaa ya Manispaa ya Morogoro kutumia akili nyingi ya kuhesabu na umakini ili kuhakisha wachezaji 11 wa timu yake wanacheza kwa ufasaha uwanjani.

“Ni mchezo unaowafanya wawe na nidhamu na umakini zaidi ya wachezaji wa soka la uwanjani kwani wao wanacheza nafasi 11 uwanjani kwa wakati mmoja,” anaeleza.

Anasema awali mchezo huo waliuanzisha katika klabu hiyo kwa ajili ya wageni kutoka Ulaya, lakini wamejikuta ukichezwa sana na watumiaji wote wa viwanja hivyo ikiwemo watoto wa Morogoro.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU