HAWA NDIO WATABEBA TAJI LA AFCON 2017

HAWA NDIO WATABEBA TAJI LA AFCON 2017

546
0
KUSHIRIKI

Libreville, Gabon

MICHUANO ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2017) inatarajiwa kuanza Jumamosi hii nchini Gabon. Michuano hiyo ya 31, ilipangwa kufanyika nchini Libya, kabla ya Agosti 2014 kuhamishiwa Gabon kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Mataifa 16 yataumana na bingwa wa michuano hiyo atapata nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 moja kwa moja.

Mtandao wa Superspot.com umekaa chini na wachambuzi mashuhuri kwenye bara la Afrika na kutabiri ni nani atanyakua taji hilo la Afcon 2017, baada ya wiki tatu za michuano hiyo.

Ghana

Mmoja kati ya wachambuzi watatu ambao wametabiri timu itakayoibuka mabingwa wa Afcon 2017 ni George ‘The Predictor’ Akpayen.

Akpayen, ambaye ni mchambuzi maarufu nchini

Nigeria, ambao wataikosa michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo, ameandika kwenye mtandao wake kwamba Ghana ‘Black Stars’ wana wachezaji mchanganyiko ambao wana uzoefu na chipukizi. Kama Asamoah Gyan, Andre na mdogo wake, Jordan Ayew, Jonathan Mensah, Baba Rahman, Adam Kwarasey, Thomas Partey, Daniel Amarte, Christian Atsu na wengine wengi ambao watakuwa na mchango mkubwa kuisaidia Ghana kunyakua taji lao la tano la michuano hiyo ya Afrika.

Ingawa bado wana kocha wa Israel, Avram Grant, ambaye wengi hawampi nafasi kubwa kuisaidia Ghana, lakini anaweza akawashangaza wengi kwa kukwepa kushika nafasi ya pili kila mara katika timu anazofundisha na kuisaidia Black Stars kubeba taji.

Lakini yote itategemea na jinsi watakavyopambana kwenye kundi lao, kutokana na timu walizopangwa nazo kama Misri, Mali na Uganda.

Haitakuwa kazi rahisi kihivyo kwa Avram na vijana wake hata kama watafanikiwa kusonga mbele baada ya mechi za makundi, kwani kuna uwezekano wa kukutana na Ivory Coast, DR Congo au Morocco kwenye hatua ya mtoano.

Huenda ikawa safari ngumu kwa Ghana, lakini wana nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa kutokana na timu, mbinu zao na kuwa tayari kwa timu yao.

Wengi wanaamini hii ni nafasi nyingine ya Ghana tangu waliponyakua taji hilo kwa mara ya mwisho mwaka 1982.

Zimbabwe

Clyde Slyde Tlou, naye alitaja timu anayofikiria kwamba ina nafasi ya kunyakua taji hilo la Afcon kwa mwaka huu.

Ambapo kwa mtazamo wake anaona kwamba Zimbabwe wana nafasi ya kufanya maajabu baada ya timu na watu waliokuwa hawapewi nafasi kufanya maajabu.

Kwa mwaka 2016, anasema watu kama Donald Trump, ambaye hakuwa akipewa nafasi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Marekani, lakini alifanikiwa kuwa rais wa nchi hiyo. Mifano mingine ya Tiou ni klabu ya Leicester City, Cape Town City na Dr Phillip Chiyangwa, ambaye kwa sasa ni Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Kusini (Cosafa).

Hivyo ndio maana anaamini hata kwenye michuano ya Afcon, timu ya Zimbabwe, ambao wana vipaji vya kuwafanya wanyakue taji hilo japokuwa hawapewi nafasi. Walifanikiwa kutinga kwenye michuano hiyo huku wakiwa na mechi moja mkononi, ambapo uwepo wa nyota aliyeisaidia Mamelodi Sundowns kunyakua taji la Klabu Bingwa Afrika, Khama Billiat, kunaweza kuwa chachu hata kwenye kikosi hicho cha Zimbabwe.

Lakini pamoja na kuipa nafasi Zimbabwe, nao Ghana wanaweza wakanyakua taji hilo wakiwa na Avram. Black Stars wamekaa muda mrefu bila ya kubeba taji hilo, ambapo michuano iliyopita waliporwa tonge mdomoni na Ivory Coast, ambao nao walikaa muda mrefu bila ya taji hilo.

“Nafikiri Ghana wanaweza kufanya vizuri, ingawa hupaswi kuitosa Gabon, wanaoweza kutumia faida ya uenyeji kulibakiza taji hilo.”

Misri

Mchambuzi wa soka wa Zambia, Puncherello Chama, ameipa nafasi kubwa Misri, akisema Mafarao hao wamerejea kwenye zama zao kutokana na soka wanaoonyesha kwenye mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Mshambuliaji wa AS Roma, Mohammed Salah, amejizolea umaarufu kwenye kikosi hicho cha Misri, akiwa ametingisha nyavu mara saba akiwa na jezi za kikosi hicho, huku kinara wa ufungaji kwa nchi hiyo akiwa mabao 28 baada ya mechi 70.

Kiungo wa Arsenal, Mohammed Elneny na Ramadhan Sobhi wa Stoke City, wanaunda safu ya kiungo ambayo nchi nyingi watashindwa kuipenya, huku wakiwa na mlinda mlango, Essam El-Hadary, bila shaka Misri hii ina nafasi ya kunyakua taji hilo la Afcon.

Kwa mara ya mwisho Misri kushiriki michuano hiyo walifanikiwa kubeba taji, hivyo bila shaka wamerejea kubeba tena taji hilo.

Michuano hiyo ya Afcon 2017, itatimua vumbi kwa wenyeji Gabon na Guinea Bissau kucheza mechi ya kwanza.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU