MISRI ITARUDIA UBABE WAO CHINI YA HECTOR CUPER?

MISRI ITARUDIA UBABE WAO CHINI YA HECTOR CUPER?

344
0
KUSHIRIKI

LIBREVILLE, Gabon

TUKIO la mwisho kubwa lililowahi kufanywa na kikosi cha Misri katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), ni bao tamu la straika wao aliyesifika kwa kufunga mabao akitokea benchi, Mohamed Nagy ‘Gedo’.

Kwa kasi akitokea wingi ya kushoto, Gedo alikokota mpira kabla ya kupigiana ‘one two’ na Mohamed Zidan, alipoingia tu kwenye  boksi la Ghana na kukaribiana na mlinda mlango, Richard Kingson, hakufanya ajizi akautumbukiza mpira kimiani na kuandika bao pekee la ushindi kwenye fainali ya michuano hiyo.

Bao la dakika ya 85 liliwasaidia Misri kuvunja rekodi kwa kutwaa taji la tatu mfululizo la michuano hiyo iliyopigwa nchini Angola mwaka 2010. Kikosi hicho kilionekana kuwa kitatishia vigogo kama Cameroon na Ivory Coast.

Tangu mwaka huo, Misri ilipata shida mno kufuzu kushiriki michuano hiyo na hata ule ubabe wao ukafifia. Ushindi wao katika michezo ya kufuzu kwenye michuano ya nyuma baada ya 2010, ulipatikana katikati mwa matatizo mbalimbali yakiwemo maanguko ya kiuchumi kwa klabu za nchini humo na migogoro ya kisiasa.

Katika michuano ya 2012, Misri haikufanya vizuri sana ndani ya mechi mbili za awali na ilijikuta ikichapwa tena kwenye mechi nyingine za awali kuelekea fainali za 2013 na timu vibonde kama Jamhuri ya Afrika ya Kati iliyokuwa ikinolewa na kocha aliyetimuliwa Swansea City inayoshiriki Ligi Kuu England hivi karibuni, Bob Bradley.

Fainali za mwaka 2015 walifanya vibaya tena kwa kumaliza nafasi ya tatu kwenye kundi lao lakini baada ya michuano mitatu kuwapitia vibaya, Mafarao hao wamerudi tena mwaka huu huku tumaini lao pekee likiwa ni kocha Hector Cuper.

Kama kuna taifa la Afrika lina kocha mzuri, basi Misri ina kocha bora ambaye ni Muargentina, Cuper.

Cuper anakumbukwa kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuifikisha klabu ya Valencia fainali mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2000 na 2001, kuwanoa moja ya miamba ya soka Italia, Inter Milan pamoja na timu ya taifa ya Georgia.

Misri ni taifa lililobahatika kuwa naye, hasa katika kipindi hiki ambacho wana njaa ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia tangu walipoonekana mara ya mwisho mwaka 1990 kwenye michuano iliyopigwa Italia.

Kocha huyo pia anaiheshimu mno dhamira hiyo, ambapo anahakikisha kwamba taifa hilo linakwenda nchini Urusi mwaka 2018 kushiriki michuano hiyo na kweli lengo lao litaweza kutimia iwapo wataendelea kufanya vizuri zaidi ya hivi sasa ambapo wanaongoza kundi lao baada ya kushinda michezo miwili.

Lakini pia, wameonesha dhamira nyingine ya kutoidharau michuano ya Afcon kulingana na kiwango cha hali ya juu kilichowasaidia kuichapa Nigeria kwenye mchezo wa kufuzu, Cuper na kikosi chake wameonesha wazi kuwa watafanya makubwa mwaka huu.

Makocha kutoka Amerika Kusini wanaokuja kuzinoa timu za Afrika huwa hawatokei mara kwa mara, lakini waliowahi kuwepo walifanya mambo mazuri.

Kocha wa Guinea ya Ikweta, Muargentina Esteban Becker, aliwahi kuifikisha timu hiyo nusu fainali katika michuano iliyopita lakini ni mara moja tu ilitokea kocha wa Amerika kuipa taji timu ya Afrika ambaye ni Otto Gloria.

Mbrazil huyo aliyezaliwa Januari 9, 1917, anakumbukwa kwa mengi enzi zake kama vile kuinoa vilivyo klabu ya Benfica iliyofanya makubwa miaka ya 1950 na kurudi tena mwaka 1968 alipoifikisha kwenye fainali ya Kombe la Ulaya.

Timu yake ya mwisho kuifundisha ilikuwa ni Nigeria ambayo alifanikiwa kuipa taji la Afrika mwaka 1980, huku wao wakiwa wenyeji. Kikosi chao kiliundwa na wakali kama Christian Chukwu, Alloysius Atuegbu, Muda Lawal na Segun Odegbami ambao waliishi na Otto kama ndugu yao kabisa kutoka Nigeria.

Cuper anafanana na Otto katika suala la kuishi kindugu na wachezaji, hilo likiwa ni jambo muhimu ili ufanikiwe katika soka la Afrika ambapo yeye ameamua kupanga kikosi chenye uwiano sawa kati ya wachezaji wanaokipiga nje na wanaotoka timu za nyumbani kama Al Ahly na Zamalek.

Je, ataisaidia Misri kunyakua taji lingine tangu walipofanya hivyo 2010? Tusubiri tuone.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU