SIRI YA KIPIGO YAFICHUKA YANGA

SIRI YA KIPIGO YAFICHUKA YANGA

3672
0
KUSHIRIKI

NA HUSSEIN OMAR

YANGA wamemaliza wiki ya kwanza ya mwaka mpya kwa kupigwa kipigo cha aibu cha mabao 4-0 na Azam katika mchezo wa makundi wa Kombe la Mapinduzi uliochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar.

Kipigo hicho cha timu hiyo kimeibua siri iliyojificha, walioanza michuano hiyo kwa kumpiga mabao 6-0 Jamhuri ya Pemba, kisha mabao 2-0 dhidi ya Zimamoto ya Unguja, ambapo baadhi ya wachezaji wa Yanga, wamesema kilichangia kupoteza mchezo huo.

Wachezaji wa timu hiyo wamesema hawakuamini kilichotokea uwanjani, kwani walikuwa na uhakika wa kushinda si chini ya mabao 3-0 kutokana na udhaifu waliouona kwa Azam na kwamba wengi walionekana hata kupuuza maagizo ya makocha wao.

Mmoja wa watoa habari wetu kutoka ndani ya kambi ya Yanga, alisema kutokana na mwanzo Azam kusuasua na kucheza soka ambalo halikuwa la kutisha kwenye mechi mbili za awali, baadhi ya wachezaji walidharau mchezo huo.

“Kuna wakati ilikuwa ukiwaambia wachezaji juu ya mechi hiyo wanasema acha Azam watufunge kama wana uwezo, wengine walisema wazi kwamba hawana sababu ya kujichosha kwa timu kama Azam ambayo imejichokea, sasa hii ndiyo iliwaponza kwani Azam wao walijua kwamba tumewadharau wakaingia kwa kukamia ushindi na wakaupata tena mkubwa,” anasema mtoa habari wetu.

Kutokana na hali hiyo, BINGWA liliwatafuta baadhi ya wachezaji wa Yanga kutaka kujua nini kilitokea ambapo mshambuliaji wa timu hiyo, Amissi Tambwe, anasema wachezaji wote hawaamini kilichotokea kwani wengi walikuta wakiishiwa nguvu ya kupambana na wapinzani wao tangu dakika za mwanzo tu.

Tambwe alisema Azam waliwazidi ujanja, licha ya wao kujiandaa kwa lengo la kutaka kuendeleza wimbi la ushindi, lakini walichanganyikiwa zaidi baada ya kushindwa kubadilisha matokeo kufuatia John Bocco kufunga bao la mapema.

“Si kweli kwamba tulidharau sana Azam, lakini katika hali ya kawaida tulijua tumeshavuka na kwa jinsi yulivyowaona Azam tuliamini kwamba tungewafunga tu,” alisema Tambwe.

Alisema kadiri mchezo huo ulivyoendelea ndivyo walivyozidiwa kiwango na wapinzani wao na wao kujikuta wakipoteana na kuchoka zaidi. “Tulipofungwa mapema ilitushtua, tulijitahidi lakini wenzetu walikuwa wamejipanga sana, yaani walijua kucheza na Yanga hii, hawakutoa nafasi kwa mipango yetu kupangwa,” alisema mshambuliaji huyo.

Lakini pamoja na hayo, Tambwe alikwenda mbali zaidi na kusema hata kama wangefungwa lakini hawakutarajia kuwa kipigo cha mabao mengi ambacho kimewafedhehesha wao na mashabiki wa timu yao.

“Hata kama ni matokeo ya mpira, lakini hapana aisee, mabao manne ni mengi sana hatuamini kupigwa bao zote hizo, inauma lakini hatuna jinsi,” alisema  Tambwe.

Tambwe alisema mpira ni mchezo wa makosa, lakini matokeo ya juzi yamewaacha hoi kabisa kwani hawakutarajia kufungwa kwa idadi kubwa ya mabao.

Kwa upande wake, Simon Msuva, ameonekana kuwatuliza mashabiki wa timu hiyo, baada ya kusema kwamba hawana sababu ya kumsaka mchawi kutokana na matokeo hayo.

“Ndio matokeo ya mpira hatuna jinsi wenzetu wamefanikiwa kuzitumia nafasi tumefungwa, ni kipigo kizito sana kwa kweli lakini hatuna nadhani tuangalie mbele tuna mechi kubwa zaidi ya nusu fainali mbele yetu,” alisema Msuva.

Msuva amewataka wachezaji wenzake na benchi la ufundi la timu hiyo kusahau kipigo hicho na kuelekeza nguvu zao katika mchezo utakaofuata.

“Yaani kama tumetega mtego, yeyote atakayeingia na sisi katika hatua ya nusu fainali atakiona cha moto, kufungwa  kwetu na Azam isiwe sababu ya wachezaji kugawanyika na kuanza kumsaka mchawi,” alisema Msuva.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU