UCHUMI, SIASA NI MAJANGA KWA WENYEJI AFCON 2017

UCHUMI, SIASA NI MAJANGA KWA WENYEJI AFCON 2017

326
0
KUSHIRIKI

LIBREVILLE, Gabon

WIKI hii mashabiki wa soka ulimwenguni kote watakuwa bize kufuatilia kile kitakachokuwa kikiendelea nchini Gabon.

Nchi hiyo ndiyo inayotarajiwa kuandaa fainali za Mataifa Afrika kwa mwaka huu ambazo zinafahamika kwa jina la Afcon 2017.

Mbio za kuwania taji la mashindano hayo makubwa barani Afrika zitaanza kutimua vumbi Januari 14 na zitafikia tamati Februari 5.

Kwa upande wao, Gabon watakuwa na kibarua kizito cha kufukuzia ubingwa wao wa kwanza kwenye michuano hiyo huku wakikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa timu vigogo zitakazotua nchini humo.

Ghana, Misri, Algeria, ni chache tu miongoni mwa timu nyingi kubwa na zenye heshima kwenye soka la Afrika zitakazokuwa zikipigania taji hilo kwa mwaka huu.

Hata hivyo, Gabon wanaandaa michuano hiyo ya Afcon 2017 huku hali ya kiuchumi nchini humo ikiwa si ya kuridhisha.

Imeelezwa kuwa bado idadi kubwa ya wananchi wake wamekuwa wakiishi maisha magumu, jambo linalosababisha wengi wao kutoona umuhimu wa mashindano hayo.

Siku kadhaa zilizopita, wachezaji wa Gabon, akiwamo Pierre-Emerick Aubameyang, waliomba mashabiki wao kuwaunga mkono lakini bado hawaonekani kufanikiwa katika hilo.

Bado wananchi wa Gabon hawafurahii kudorora kwa hali ya kiuchumi nchini mwao huku pia kukiwa na shaka ya kuyumba kwa masuala ya kisiasa.

Licha ya matangazo mbalimbali ya Afcon katika mitaa mbalimbali, bado wananchi wameendelea kuwa bize na mambo yao.

Hali tete ya kiuchumi imesababishwa na kuporomoka kwa kasi kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Itakumbukwa kuwa uchumi wa Gabon inayotajwa kuwa na watu milioni 1.8, unategemea kwa kiasi kikubwa rasilimali ya mafuta.

“Watu wengi wameathirika kutokana na kuyumba kwa bei ya mafuta ulimwenguni. Wengi wamepoteza kazi katika viwanda vya mafuta,” alisema Rais wa nchi hiyo, Ali Bongo Ondimba.

Kuhusu mtikisiko wa kisiasa nao kwa kiasi kikubwa unatishia hali ya usalama katika siku za usoni.

Uchaguzi  uliomuweka madarakani rais wao Bongo, umeonekana kukosolewa na kutiliwa shaka na mahakama ya katiba nchini humo na hata  Umoja wa Ulaya (EU), hawaonekani kuridhishwa nao.

Kwa upande wake, Bongo amesisitiza kuwa uchaguzi wake haukua na shaka, hivyo ana haki zote za kuiongoza nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Ikiwa ni miezi sita imepita tangu Bongo alipotangazwa kuwa rais, aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi huo, Jean Ping, ameendelea kujitamba kuwa yeye ndiye mshindi huku akimtaja Bongo kuwa alitumia njia za panya kuingia ikulu.

Mpinzani huyo, Ping, ametamka wazi kuwa hayuko tayari na atapambana kuona nchi hiyo haibaki mikononi mwa ‘dikteta’ Bongo.

Mvutano huo nao umetajwa kuwaweka roho juu wananchi wa Gabon na kuwavuruga kiakili, hivyo suala la michuano ya Afcon kwao si kitu cha msingi sana.

Katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na tishio la migomo ambapo wafanyakazi wa Serikali wamekuwa wakishinikiza kuondoshwa kwa mgogoro huo wa kisiasa.

Lakini pia, magazeti yanayounga mkono vyama pinzani nayo yameendelea kuhimiza wananchi kugomea michuano ya Afcon hasa katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Guinea-Bissau utakaochezwa Januari 14.

Lakini pia, yamewataka wananchi wa Gabon kutumia mashindano hayo kupaza sauti ya kile kinachowamaliza wakiwa nchini kwao.

Wachambuzi wa soka wameanza kutilia shaka usalama katika michezo mbalimbali ya Afcon hasa ile itakayochezwa Port-Gentil na Oyem, miji ambayo imekuwa na machafuko ya mara kwa mara.

Hata hivyo, kinyume na mawazo ya wachambuzi hao, rais Bongo ameendelea kusisitiza kuwa anaamini mashindano hayo yatakuwa na mafanikio makubwa katika kurejesha hali ya utulivu nchini kwake.

Bongo amesema ni wakati wa Wagabon kufunga mijadala ya kisiasa kwa sasa na kuelekeza nguvu Afcon 2017, jambo ambalo limepingwa na hasimu wake Ping.

Mbali ya Aubameyang anayekipiga Borussia Dortmund, Gabon ina idadi kubwa ya mastaa wanaoweza kuipa mafanikio timu hiyo katika michuano ya Afcon 2017.

Mfano; Didier Ndong wa Sunderland, Mario Lemina (Juventus) Bruno Ecuele Manga (Cardiff City) na Malick Evouna (Tianjin Teda,  Ligi Kuu China).

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU