AFCON 2017 NI ZAMU YA AUBAMEYANG AU MAHREZ?

AFCON 2017 NI ZAMU YA AUBAMEYANG AU MAHREZ?

444
0
KUSHIRIKI

LIBREVILLE, Gabon


IVORY Coast wataweza kutetea ubingwa wao katika fainali za Mataifa Afrika za mwaka huu (Afcon 2017)?

Lakini je, wenyeji Gabon watavuna nini ikizingatiwa kuwa nchi yao imekuwa kwenye mtikisiko wa kisiasa na kiuchumi?

Vipi kuhusu Misri ambao wameikosa michuano mitatu iliyopita?

Bila shaka hayo ndiyo maswali yaliyobaki vichwani mwa mashabiki wa soka kuelekea Afcon 2017.

Mbio za kuliwania taji la michuano hiyo zitaanza kutimua vumbi Jumamosi, Januari 14.

Mbali na mastaa wengine, Pierre-Emerick Aubameyang na Riyard Mahrez watakuwa kivutio kikubwa kwenye mashindano hayo.

Aubameyang anayekipiga Borussia Dortmund atakuwa na kibarua cha kuibeba Gabon ambayo haipewi nafasi kubwa ya kung’ara kwenye michuano hiyo.

Kwa upande wake, Riyad Mahrez, amepania kuifikisha Algeria fainali ya michuano hiyo hapo Feburi 5.

Wakati Aubameyang akiwa moto wa kuotea mbali katika kupasia nyavu Bundesliga, Mahrez ndiye aliyetwaa tuzo ya Mchezaji Bora Afrika kwa mwaka jana.

Katika kinyang’anyiro hicho, Mahrez aliwabwaga Aubameyang na Sadio Mane.

“Kinachofuata baada ya tuzo hii ni Afcon. Timu yangu itajaribu kufanya vizuri,” alisema Mahrez ambaye alizaliwa Ufaransa.

Algeria watakuwa Kundi B pamoja na Senegal, Tunisia na Zimbabwe.

“Kundi letu ni gumu likiwa na timu kubwa Afrika. Lakini tumejiandaa na tuna timu nzuri.”

Kwa upande wao, Ivory Coast watamkosa mkongwe Yaya Toure ambaye alistaafu soka la kimataifa mwaka 2015.

Pia, watamkosa fowadi wao, Gervinho, ambaye ni majeruhi.

Ivory Coast wapo Kundi C ambapo watakuwa na Morocco inayonolewa na kocha wao wa zamani, Mfaransa Herve Renard.

Morocco wanapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele na kutinga hatua ya robo fainali na kuzipiku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Togo itakayokuwa na straika Emmanuel Adebayor.

“Nimepanga kufika robo fainali na tunaweza kufanya hivyo,” alisema Renard ambaye pia aliwahi kukiongoza kikosi cha Zambia kushinda fainali za Afcon 2012.

Hii ni mara ya kwanza kwa Misri kucheza michuano hiyo tangu mwaka 2010.

Matarajio yao yako kwa winga wa Roma, Mohamed Salah.

Ni moja kati ya timu vigogo zilizokosa nafasi ya kucheza michuano hiyo mwaka 2015.

Itakuwa Kundi D ambapo itavaana na Uganda, Mali na Ghana.

Pia, michuano ya mwaka huu ni ya kwanza kwa Guinea-Bissau ambapo watatoana jasho na wenyeji Gabon katika mchezo wa ufunguzi utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Stade de l’Amitie uliopo jijini Libreville.

Gabon iliyopo Afrika ya Kati ina watu milioni 1.8 na imezungukwa na Equatorial Guinea, Cameroon, Congo na Guinea.

Nchi hiyo ina ukubwa unaokaribia kilomita za mraba 270,000.

Gabon ilipata bahati ya kuandaa mashindano ya Afcon 2017 baada ya Libya kushindwa kutokana na machafuko ya kisiasa.

Hata hivyo, bado hali ya usalama pale Gabon haijaonekana kutulia hasa baada ya uchaguzi mkuu.

Kitendo cha Rais Ali Bongo kutangazwa kushinda uchaguzi wa Agosti mwaka jana, kimekosolewa vikali na wanaharakati wa masuala ya kisiasa wa ndani na nje ya nchi hiyo.

Mpinzani wake Jean Ping amedai kuwa alistahili kushinda lakini Bongo alifanya ‘figisu figisu’.

Wapinzani wa Bongo wamewataka wananchi kususia michuano hiyo ya Afcon 2017.

Hata hivyo, Bongo ameonekana kutotilia shaka hali ya usalama kwa kipindi chote cha mwezi mmoja wa mashindano.

Mwaka jana, alimwalika staa wa Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi, kuweka jiwe la msingi kabla ya ujenzi wa Uwanja wa Port-Gentil utakaotumika kuanzia wiki ijayo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU