MOROCCO KUMKOSA BOUFAL AFCON

MOROCCO KUMKOSA BOUFAL AFCON

328
0
KUSHIRIKI

RABAT, Morocco


TIMU ya Taifa ya Morocco itamkosa kiungo wake mahiri, Sofiane Boufal, baada ya kujitoa katika kikosi hicho kutokana na majeraha yanayomkabili.

Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa staa huyo wa timu ya Southampton, alijitoa kwenye kikosi hicho juzi baada ya kuumia wakati timu hiyo ikiwa mazoezini katika nchi za Falme za Kiarabu ikijiandaa na mechi yao ya kirafiki iliyotarajiwa kupigwa jana dhidi ya Finland na hivyo ataungana na mwenzake, Younes Belhanda  ambaye naye tayari yuko nje ya uwanja.

“Sofiane Boufal ameondoka kambini  iliyopo Al-Ain leo asubuhi (juzi), baada ya kuthibitishwa majeraha yake na hivyo hawezi kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika,” ilieleza taarifa kutoka Shirikisho la Soka nchini humo bila kutoa maelezo zaidi kuhusu majeraha yanayomkabili  nyota huyo.

“Nafasi yake itajazwa na mchezaji mwingine ambaye jina lake lilitatajwa baadaye,” iliongeza taarifa hiyo.

Boufal ambaye alijiunga na  Southampton akitokea Lille ya Ufaransa, wakati wa usajili wa majira ya joto yaliyopita alikuwa akionekana kuwa tegemeo katika kikosi hicho cha Morocco, baada ya Belhanda kuvunjika kidole siku chache kabla ya Sikukuu ya Krismas ambacho kitamfanya akae nje ya uwanja kwa muda wa wiki zaidi ya sita.

Katika fainali hizo zitakazofanyika nchini Gabon kuanzia Januari 14, Morocco ambayo kwa mara ya mwisho kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ilikuwa mwaka 1976, imepangwa Kundi C na itazianza kwa kukutana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)  mechi itakayopigwa Januari 16 kabla ya kuzivaa Togo na Ivory Coast.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU