NIYONZIMA AMKABIDHI ‘MZIGO’ MWAMUZI

NIYONZIMA AMKABIDHI ‘MZIGO’ MWAMUZI

1661
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY


NAHODHA wa Yanga, Haruna Niyonzima amesema kuwa pamoja na ugumu wa mchezo wao dhidi ya Simba kutokana na kila timu kujiandaa vilivyo, lakini mwisho wa siku, mwamuzi atakayechezesha pambano baina yao leo, ndiye atakayeamua mechi iwe nzuri au la.

Akizungumza na BINGWA jana, Niyonzima alisema  wao wamejipanga  na wanaamini utakuwa mchezo mzuri iwapo mwamuzi atazitafsiri kikamilifu sheria zote 17 za mchezo wa soka.

“Sisi tumejiandaa vizuri na wapinzani wetu wamejianda pia na hiyo inatokana na ukweli kuwa mpira wa miguu ni maandalizi, hivyo sina shaka utakuwa mchezo wa kipekee na dakika 90 zitaamua.

“Lakini ili uwe na mvuto, lazima mwamuzi atimize majukumu yake ya kuhakikisha anatafsiri vizuri sheria za mchezo kwani yeye ndiye kila kitu tunapokuwa uwanjani,” alisema.

Niyozima alisema maneno mengi yamekuwa yakisemwa juu yake kwamba na mapenzi na Simba hivyo kucheza chini ya kiwango pindi mechi hiyo inapowadia na kusisitiza safari hii amepanga kuwakata kidomodomo wabaya wake.

“Ni mechi ambayo maneno mengi sana yanakuwa yanazungumzwa lakini kimsingi, tumejipanga vyema kuhakikisha tunashinda. Baada ya kupoteza pambano letu lililopita dhidi ya Azam, tumejipanga kufanya kweli,” alisema Niyonzima.

Pamoja na hayo, kiungo huyo alisema wachezaji wote ndani ya kikosi cha Yanga wamejiapiza kufanya kila linalowezekana kuwaziba midomo wenzao wa Simba.

“Sababu tunayo na nia tunayo. Wachezaji wote tuliitaka hii mechi. Sasa imekuja wakati mwafaka na hatuna budi kujipanga katika suala zima la kupata ushindi. Kila mmoja analifahamu hilo kwa uwazi kabisa,” alisisitiza Niyonzima.

Katika hatua nyingine, kiungo huyo alisema ushindi wa leo utawapa fursa nzuri ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ya Kombe la Mapinduzi.

“Unajua tangu nije hapa bongo sijawahi kulishika au kulipokea Kombe la Mapinduzi. Ukweli ni kwamba nalitaka hili kombe nilipokee mwenyewe. Makombe yote nimefanikiwa kuyashika, lakini hili la Mapinduzi bado,” aliongeza kiungo huyo.

Kuelekea katika pambano hilo la leo, nyota huyo wa kimataifa wa Rwanda amewataka wachezaji wenzake watakaokuwa sehemu ya kikosi cha kwanza leo kujituma ili kuweza kutimiza malengo yao ya mwaka huu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU