OMOG AIBA UCHAWI AZAM, AANDAA ‘4G’ NYINGINE

OMOG AIBA UCHAWI AZAM, AANDAA ‘4G’ NYINGINE

1029
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR


KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog pamoja na msaidizi wake, Jackson Mayanja, wametamba kuishikisha adabu Yanga watakapokutana nao leo katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, huku wakiwa na matumaini tele ya kuwashushia watani wao hao wa jadi kipigo kitakatifu kama kile walichokipata kutoka kwa Azam Jumamosi iliyopita cha mabao 4-0 (four goals ‘4G’).

Simba watashuka uwanjani huku wakipewa nafasi kubwa ya ushindi baada ya kufanya vema katika hatua zilizopita, wakati wapinzani wao hao wakitoka kupata kipigo kikali kutoka kwa Azam katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi.

Kutokana na upepo ulivyo kwa Wekundu wa Msimbazi hao, Omog na mwenzake, Mayanja wanaonekana kuwa katika morali ya hali ya juu ya kushinda na tayari hesabu zao wamezielekeza kwenye idadi kubwa zaidi ya mabao.

Na silaha pekee ambayo Omog ataitumia, ni kufuata nyayo za Azam kwa kujaza viungo wengi ili kuwamaliza wale wa Yanga ambao wameonekana kutokuwa na kasi kubwa kwani wengi wana umri mkubwa tofauti na ilivyo kwa wenzao wa Msimbazi.

Viungo wa Simba wanaotarajiwa kuimaliza Yanga ni Jonas Mkude, Yassin Muzamiru, James Kotei, Jamal Myante, Said Ndemla na wengineo wengi, akiwamo kiungo mshambuliaji, Mohammed Ibrahim ‘Mo’ ambao ni wazi watapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza, iwe ni kwa kuanza au kuanzia benchi.

Mbali ya hayo, mshambuliaji raia wa Burundi, Laudit Mavugo, ametakiwa kuhakikisha anang’ara leo kama anataka kuendelea kuwapo Msimbazi baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye mechi kadhaa zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tayari wapenzi wa soka Tanzania Bara, wamepanda boti kwenda Zanzibar kushuhudia mtanange huo, japo wale wa Simba ndio wanaoonekana kujiamini zaidi.

Hata hivyo, kuna imani kuwa timu hizo mbili zinapopambana, ile inayoonekana dhaifu ndiyo siku zote inayotoka uwanjani na ushindi.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU