PLUIJM ATUMA UJUMBE MZITO ZENJI

PLUIJM ATUMA UJUMBE MZITO ZENJI

1635
0
KUSHIRIKI

NA HUSSEIN OMAR


MKURUGENZI wa Ufundi wa Yanga, Hans van der Pluijm, amewatakia kila la kheri vijana wake hao wa Jangwani katika mchezo wao wa hatua ya nusu fainali michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba, utakaopigwa leo usiku kwenye Uwanja wa Amaan, akiwataka kuhakikisha wanacheza kwa uwezo wao wote ili kumwangamiza ‘Mnyama’.

Akizungumza na BINGWA jana, Pluijm alisema hatakuwepo uwanjani kushuhudia pambano hilo leo, lakini amewataka vijana wake kupigana kufa kupona kuiletea ushindi timu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Jangwani na Twiga, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

“Nipo Dar, sijaambatana na timu kwenye mashindano. Nina masuala yangu binafsi ila nawatakia kila la kheri vijana wangu. Namwomba Mungu awape wepesi waibuke na ushindi leo,” alisema Pluijm.

Katika hatua nyingine, Mholanzi huyo alisisitiza nidhamu ya mchezo kwa wachezaji wa timu hiyo kuelekea katika pambano hilo la leo ambalo linavuta hisia za mashabiki wengi hapa nchini na wale wa nchi za jirani.

“Kama unavyojua, mchezo wa Simba na Yanga ni presha tupu. Nawaomba wachezaji kuzingatia nidhamu ya mchezo kuepuka kupata kadi zisizo na ulazima, nipo pamoja nao nawaunga mkono,” aliongeza Mholanzi huyo.

Simba na Yanga zinakutana kwa mara ya kwanza tangu kuanza mwaka huu na watakutana tena katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara msimu wa 2016/17.

Mahasimu hao wawili wanakutana ikiwa ni baada ya juzi Simba kufanikiwa kuongoza Kundi A kwa kufikisha pointi 10, ikishinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja. Mahasimu wao Yanga wameshika nafasi ya pili katika Kundi B, baada ya kujikusanyia pointi sita, wakishinda michezo miwili na kufungwa mmoja.

Hata hivyo, timu hizo zimekutana mapema kabla ya mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopangwa utakaopigwa Februari 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo umekuja kumaliza ubishi baina ya mahasimu hao ambao katika mechi yao ya Oktoba mosi mwaka jana walitoka sare ya bao 1-1 na kuibua vurumai kubwa zilizosababisha uharibifu wa miundombinu ya Uwanja wa Taifa.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU