KUONGEZWA TIMU 48 FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA 2026…...

KUONGEZWA TIMU 48 FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA 2026… KUTAINUFAISHA AFRIKA?

350
0
KUSHIRIKI

ZURICH, Uswisi

WAJUMBE wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wamepigia kura pendekezo la kuongeza timu kwenye fainali za Kombe la Dunia kutoka 32 hadi 48, lakini mabadiliko hayo yatafanyaje kazi na Bara la Afrika litanufaika vipi?

Pendekezo la Rais wa shirikisho hilo la soka, Gianni Infantino, lilipitishwa juzi Jumanne, ambapo fainali za michuano hiyo za mwaka 2026 zitakuwa na makundi 16 na kila kundi likiwa na timu tatu.

Hii ni mara ya kwanza tangu mwaka 1998 yalipofanyika mabadiliko ya kuongeza timu nyingine nane na kuwa 32, lakini swali kubwa ni jinsi michuano hiyo itakavyofanyika baada ya kuongezwa kwa timu hizo.

Mfumo huo mpya utafanyaje kazi?

Wajumbe walipigia kura mapendekezo manne tofauti ya kuongeza timu za kushiriki fainali za Kombe la Dunia, likiwemo pendekezo la timu 40 huku kundi moja liwe na timu nne au tano, wengi walilipitisha pendekezo la Infantino lililokuwa na timu 48 yenye makundi 16 na kila kundi timu tatu kukifuatiwa na hatua ya mtoano kwa timu 32 zinazosonga mbele.

Pendekezo hilo lililopigiwa kura litaongeza mechi na kutoka 64 hadi 80, lakini fainali hizo zitatumia simu 32 kumalizika.

Kwanini Fifa wametaka mabadiliko?

Infantino aliweka wazi lengo lake la kuongeza timu ni kuyapa mataifa mengine nafasi ya kufurahia fainali za Kombe la Dunia, kuinua, kukuza na kuendeleza soko la soka kimataifa.

Ingawa kumekuwa na ukosoaji kwamba pendekezo la kuongeza timu limetokana na tamaa ya fedha, Fifa wamesema kwamba mapato yataongezeka hadi bilioni 5.3 kutoka 4.5 zinazotarajiwa kupatikana kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Pia pendekezo hilo ni jaribio la kwanza kwa utawala wa Infantino aliyerithi mikoba ya Sepp Blatter.

Afrika inanufaikaje na mpango huu?

Haijawekwa wazi jinsi ambavyo timu 16 zilizoongezwa zitakavyojumuishwa katika fainali hizo za Kombe la Dunia mwaka 2026, lakini moja ya mipango yao ni kuongeza timu tatu kutoka Bara la Ulaya.

Afrika inaweza ikapata faida kubwa kwa kuongezeka timu nyingine nne, ukiacha zile tano za mwanzo na sita zitaongezwa kutoka bara la Amerika Kusini. Upande wa Oceania watakuwa na uhakika wa kupata nchi ya kucheza kwenye fainali hizo, wakati Shirikisho la Soka la Kaskazini, Amerika ya Kati na Chama cha Soka cha Caribbean (CONCACAF) na bara la Asia zitakutana timu mbili kusaka nafasi moja.

Mashujaa wa Euro 2016, Iceland pamoja na Uzbekistan, Burkina Faso na Venezuela, ambao wote walikaribia kutinga fainali hizo, wanaweza wakapata nafasi mwaka 2026, lakini taswira nzima ya mchakato utakavyokuwa na timu zitakavyoongezwa, utajulikana baada ya kikao kijacho cha Baraza la Fifa nchini Bahrain, Mei mwaka huu. Jambo moja kubwa ni kwamba kutakuwa na upinzani mkubwa sana katika kusaka nafasi hizo zilizoongezwa.

Pendekezo hilo linaungwa mkono?

Kuna baadhi ya watu ambao wako kinyume na Fifa, tayari wameshaanza kukosoa mpango huo, ambapo wanadai upo kwa ajili ya kupata fedha.

“Haitasaidia kuendeleza soka au kuongeza ushindani kwa mataifa yaliyo chini kwenye ubora,” yalisema baadhi ya maelezo ya wanaopinga pendekezo hilo.

“Badala yake, italeta kejeli katika kufuzu kwa shirikisho lote, imelenga kupata fedha na kupata nguvu ya kutawala.

Muungano wa klabu za Ulaya, ambapo Manchester United na Liverpool ni wanachama, nao ulitoa kauli yao ikisema uamuzi huo ni wa ‘kisiasa kuliko kisoka.”

Ujerumani nao wamekosoa muundo huo mpya wa timu za Kombe la Dunia, lakini nchi nyingi za Ulaya zimeunga mkono mipango hiyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Scotland (FA), Stewart Regan, amezipokea habari hizo kwa kusema: “Tunaamini hii ni habari njema, hasa kwa mataifa madogo, itasaidia mashabiki mbalimbali duniani kujumuika kuzishangilia klabu zao kwenye fainali hizo za Komnela Dunia. Hilo pia litasaidia mataifa hayo kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya kisoka na kuendeleza soka la vijana, ambapo inaweza kusaidia jamii.”

Mambo ambayo bado hayajaamuliwa

Pamoja na mipango hiyo, Infantino amependekeza kuwemo kwa penalti kwenye mechi zote ambazo zinaishia kwa sare, ili kukwepa uwezekano wa kupanga matokeo katika mechi za mwisho za michuano hiyo.

Maamuzi mengine ya kujua nani ataandaa fainali hizo za 2026, haijajulikana mpango mwaka 2020 huku kukiwa na ofa kutoka Marekani, kama watafanya wenyewe au kushirikiana kati ya Canada na Mexico, ambao wote wana uwezekano wa kupewa nafasi hiyo

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU