NGOMA ATAJWA USHINDI WA SIMBA

NGOMA ATAJWA USHINDI WA SIMBA

1771
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY, ZANZIBAR

KIPIGO cha changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia sare tasa ndani ya dakika 90 walichokipata Yanga kutoka kwa Simba katika nusu fainali ya michuano ya Mapinduzi juzi usiku, kimewafanya baadhi ya mashabiki wa Wanajangwani hao kutamka wazi kuwa kilitokana na kutokuwamo katika kikosi straika wao, Donald Ngoma.

Yanga walikubali kichapo hicho katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Amaan visiwani hapa, ambapo Simba watakutana na Azam kesho katika fainali.

Ngoma alikosekana katika mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi ambapo mashabiki wa Yanga wanadhani kuwa kama angekuwapo wangeibuka na ushindi kwa madai kuwa safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa dhaifu na washambuliaji wao wakiongozwa na Amissi Tambwe, walishindwa kuutumia mwanya huo.

Mbali na mchezo huo, pia Ngoma alikosekana dhidi ya Azam FC Yanga walipopewa kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 4-0 hatua ya makundi na kuwafanya kumaliza nafasi ya pili iliyowafanya kukutana na Simba waliomaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi lao katika nusu fainali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashabiki wa Yanga walioshuhudia mchezo huo, walisema kuwa safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa uchochoro, lakini Tambwe na wenzake wakashindwa kutumia vizuri nafasi hiyo kufunga na kama Ngoma angekuwapo ushindi ungepatikana mapema.

Shabiki maarufu wa Wanajangwani hao,  Ally Yanga, alisema laiti kama Ngoma angekuwapo shughuli ingeisha mapema na wangekwenda kulala usiku huo kwa furaha kwani safu ya ulinzi ya Simba iliyokuwa chini ya Abdi Banda na Method Mwanjale, isingeweza kumzuia.

“Mwili wa Ngoma na nguvu zake mara nyingi zimekuwa zikiwasumbua mabeki wa timu pinzani, nina uhakika Yanga ingepata ushindi ndani ya dakika 90.

“Zile beki za Simba zilikuwa dhaifu sana katika mchezo huo na washukuru Mungu kwamba Ngoma hakuwapo kwani angewaaibisha mno, sidhani kama Banda na Mwanjale wanaweza kumzuia yule jamaa asifunge.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU