OMOG: SIMBA UBINGWA LAZIMA

OMOG: SIMBA UBINGWA LAZIMA

1506
0
KUSHIRIKI

ZAINAB IDDY NA SAADA SALIM, ZANZIBAR

BAADA ya kuitoa Yanga kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia sare tasa katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi uliochezwa juzi  usiku kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa, sasa umemsikia Kocha Mkuu wa Simba,  Joseph Omog, anachosema?  Sikiliza.

Omog amesema baada ya kutinga fainali  atahakikisha anaifunga Azam katika mchezo utakaochezwa kesho Ijumaa kwenye uwanja  huo na ubingwa  kutua Mtaa wa Msimbazi, Kariokoo jijini Dar es Salaam.

Alisema amefanikiwa kuvuka hatua hiyo hivyo ubingwa lazima utatua Simba,  kwani Azam ni wepesi  kwa kuwafunga kutokana na kwamba wanajua udhaifu wao, hasa baada ya kuwasoma walipocheza na Yanga katika makundi ya michuano hiyo wiki iliyopita.

Omog alisema licha ya Azam kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Yanga,  anaamini si timu ya kutisha kiasi cha kuwasumbua katika kuhakikisha  wanapata ushindi.

Alisema pamoja na kwamba Azam ina wachezaji wazuri, lakini atapata kikosi cha ushindi ili waweze kubeba kombe hilo.

Omog alisema soka waliloonyesha wachezaji wa Azam wakati walipocheza na Yanga, itakuwa ni rahisi kwake kupata ushindi katika mchezo huo wa fainali.

Katika hatua nyingine, Nahodha wa Azam, John Bocco, amesema ushindi wa mabao 4-0 walioupata  katika mchezo wa makundi dhidi ya Yanga  umewapa ujasiri mkubwa.

Bocco alisema ujasiri huo uliwawezesha kushinda mchezo uliofuata wa nusu fainali baada ya kuifunga bao 1-0 Taifa Jang’ombe na kutinga fainali ambayo watakutana na Simba.

Alisema anaiheshimu Simba kwa kuwa ni timu nzuri, lakini wao watapambana kuhakikisha wanapata ushindi  na baadaye kuondoka na kombe hilo.

“Hatukuanza vema katika hii michuano,  lakini baada ya ushindi wetu na Yanga ambao tulishinda mabao mengi, ulitupa ujasiri wa kujiamini, tutapambana kuhakikisha tunarejea nyumbani na kombe,” alisema.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU