VIPIGO VYAPASUA VICHWA COASTAL UNION

VIPIGO VYAPASUA VICHWA COASTAL UNION

491
0
KUSHIRIKI

NA OSCAR ASSENGA, TANGA

JINAMIZI la kufungwa mechi za nyumbani za Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, limeanza kuwapasua vichwa viongozi wa Coastal Union na sasa wanahaha kutafuta ufumbuzi.

Katika mchezo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijii hapa, Coastal Union iliendelea kufungwa  baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa  Kurugenzi ya Mufundi.

Akizungumza  na BINGWA jana, ofisa habari wa timu hiyo, Hafidh Kidoh,  alisema kutokana na hali hiyo wanakusudia kukutana ili kuona namna ya kufanya vizuri kwa mchezo utakaofuata.

Kidoh alisema lengo la kukutana haraka ni kutaka kuokoa timu hiyo ili iendelee kubaki kwenye ligi hiyo, kwani hawana uhakika wa kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao kutokana na matokeo mabaya wanayoendelea kupata kwa sasa.

Alisema licha ya juhudi kubwa walizozifanya kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri, lakini  wamekuwa wakipoteza mechi zao na kupoteza matumaini ya kujerea ligi kuu msimu ujao.

“Unajua sisi tulifanya kazi kubwa kuhakikisha timu yetu inafanya
vizuri, lakini mambo yamekuwa mabaya kutokana na mwenendo mbovu wa matokeo tulionao, tumeshindwa kutimiza ndoto zetu ila tutajipanga kuona namna ya kufanikisha msimu ujao.
“Kwa sasa tunaangalia namna ya kuipatia ufumbuzi changamoto
za kupoteza michezo yetu ya nyumbani, kwani hili ni tatizo kubwa ambalo tunahitaji kulitatua haraka,” alisema Kidoh.

Coastal Union imesaliwa na michezo minne dhidi ya JKT Mlale ya Songea, Mbeya Warriors, Njombe Mji na KMC ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, kiungo wa zamani wa African Sports, Raphael John, amesema ukata na kukosekana kwa ufadhili ni chanzo cha timu za mkoa huo kufanya vibaya kwenye ligi hiyo.

John alisema hakuna muujiza mwingine utakaowezesha timu za Coastal Union, African Sports na Mgambo Shooting kufanya vizuri kama wafadhili na wadau hawatajitokeza kuzisaidia timu hizo.

Alisema bila kushirikiana kwa pamoja wakazi wa Tanga wataendelea kuiona Ligi Kuu Bara kwenye runinga.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU