YANGA VS SIMBA, ILIKUWA MECHI YA MBINU NA MAELEKEZO

YANGA VS SIMBA, ILIKUWA MECHI YA MBINU NA MAELEKEZO

1137
0
KUSHIRIKI

NA AYOUB HINJO

MASHABIKI wengi kutoka Tanzania Bara walivuka maji kuelekea kisiwani Unguja kuangalia mchezo huo wa watani wa jadi. Inawezekana hata pale uwanjani walikuwa wengi kuliko hata wenyeji wenye uwanja wao. Ndivyo mchezo wa soka ulivyo. Ndivyo inavyodhihirisha Watanzania ni vichaa wa soka.

Mchezo huo wa nusu fainali ulitosha kudhihirisha nguvu ya timu hizi ilivyokuwa kubwa kutokana na mapenzi ya mashabiki wake kutoka sehemu mbalimbali nchini. Ni mchezo uliofuatiliwa na Watanzania wote na kwa ufupi unaweza kusema Tanzania ilisimama kwa dakika 90 za mchezo huo.

Ni mchezo ambao ulizikutanisha timu hizo kwa mara ya kwanza katika mwaka huu wa 2017 na ikiwa ni mara ya pili katika michuano ya Kombe la Mapinduzi na kwa bahati nzuri, Simba mara zote wanazokutana na Yanga kwenye michuano ya kombe hilo wanashinda.

Kabla ya mchezo, pengine kila mtu alisema ni ngumu kutabiri mechi ya Simba na Yanga. Ni kweli, kiufundi timu zote ziko vizuri sana na zina vikosi imara mno, lakini kwa upande mwingine, Simba walikuwa na matumaini ya ushindi hasa kutokana na mahasimu wao kutoka kupoteza mchezo wao na Azam kwa mabao 4-0.

Tukiuangalia mchezo huo kwa jinsi ulivyochezwa ndani ya dakika 90, kuna mengi yanaweza kuzungumza kiufundi kwa timu zote mbili. Achilia mbali penalti ambazo mara zote huwa hazina mwenyewe.

Ni mchezo uliojaa mbinu na maelekezo

Ilikuwa tofauti kwa timu zote mbili tangu zikutane kwenye Uwanja wa Amaan. Simba waliingia uwanjani wakiwa na mbinu ya kumiliki mchezo, lakini pia wachezaji wake walitakiwa kuzingatia sana maelekezo ya benchi la ufundi.

Omog alijaza viungo wengi ili kuifanya timu yake itengeneze nafasi za magoli, uwapo wa Jonas Mkude, James Kotes, Mzamiru Yasin, Mohammed Ibrahim, ilionyesha wazi kwamba kocha Joseph Omog alikuwa na mbinu ya kuwakata kabisa Yanga na viungo wawili wa kulinda ukuta na wawili wa kupandisha mashambulizi kwa kumlisha Juma Luizio. Lakini haikuwa hivyo, kwani hawakutengeneza nafasi nyingi sana lakini zile za wazi walishindwa kuzitumia.

Kwa upande wa Yanga ni kama ilivyokuwa kwa wapinzania wao, waliingia wakiwa na mbinu zao za kuwaadhibu Simba walijaza viungo pia, Thaaban Kamusoko, Said Juma Makapu walifanya kazi ya kulinda ukuta, Deus Kaseke na Haruna Niyonzima nao wakafanya kali ya kulisha safu ya ushambuliaji, mbinu za kocha George Lwandamina zikagongana na Omog na hivyo kuufanya mpira wa juzi usivutie kabisa kwa kuwa mafundi walifanya kazi kubwa ya kufuata maelekezo na si kuonyesha ufundi wao.

Lwandamina alifahamu Simba wataingia na staili gani, ndio maana akaamua kutumia mipira mirefu kwa wachezaji wake wa safu ya mbele na alijua wazi kwamba vita ya katikati ingekuwa kubwa sana ndiyo maana akaamua kupanga kikosi namna ile.

Hawa walitisha zaidi

Daniel Agyei, ingizo jipya la Simba kwenye usajili wa dirisha dogo. Kipa huyu amechukua nafasi ya Vincent Angban tangu apate nafasi kwenye kikosi cha Simba anaonekana kuwa na vitu vingi vya ziada.

Ufanisi wake wa kuokoa mikwaju ya penalti ulifanikiwa kuivusha Simba hatua ya nusu fainali kuelekea fainali.

James Kotei, mashabiki wa Simba wanamwita “mkata umeme wa kweli.” Kweli! Alidhihirisha hilo, alihakikisha mabeki wake hawapati madhara na bado muda mwingi alionekana kuisukuma timu kwenda mbele.

Kwa kazi aliyoifanya inaonyesha ni usajili makini wa Simba hadi sasa. Ndio alikuwa nyota wa mchezo kwenye mechi hiyo ya watani wa jadi.

Luizio alishindwa kuzitumia nafasi mbili za wazi alizozipata kuwaadhibu Yanga, lakini alionyesha yeye si mshambuliaji wa mchezo linapokuja suala la kuisaidia timu kutengeneza nafasi za magoli.

Ana kasi na pia ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira. Mara nyingi alikaa na mpira mguuni kuhakikisha anawavuta mabeki wa Yanga ili kutoa nafasi kwa wenzake kufunga, lakini mabeki wa Yanga walikuwa na nidhamu ya hali ya juu sana na hawakuruhusu hilo.

Said Juma Makapu tangu kuja kwa kocha mpya amekuwa akipata nafasi mara kwa mara ya kucheza. Ana uwezo wa kuwalinda mabeki wake kama alivyofanya kwenye baadhi ya michezo aliyocheza.

Kama lilivyo jina lake, “Makapu” alijitahidi kuzuia kiasi kikubwa cha mashambulizi yaliyojengwa na Simba kuelekea golini kwao, alicheza kwa kufuata maelekezo kuhakikisha Mo Ibrahim na Mzamiru hawaelewani na alifanikiwa.

Niyonzima, fundi huyu wa mpira, alijitahidi kufanya kila lililowezekana kufikisha mipira kwa Tambwe, lakini umakini wa mabeki wa Simba ulizuia pasi zake nyingi Kotei hakuwa na kazi kubwa sana na Niyonzima kwa sababu ni kama walijua wazi kwamba kumficha Msuva na Kaseke kuwa chini ya ulinzi kulipunguza madhara ya Niyonzima.

Alikuwa kiunganishi mzuri kutoka nyuma hadi mbele. Alipiga pasi ndefu na fupi kuhakikisha wanapata matokeo chanya lakini mwishowe haikuwa hivyo.

Kaseke huwa hasemwi sana na mashabiki wa Yanga, lakini ni moja ya watu waliopambana kweli kweli. Alishirikiana vizuri na Haji Mwinyi kuhakikisha mashambulizi hayapiti.

Kaseke alikuwa makini sana katika kushambulia na kuzuia. Kwa muda aliocheza hakumfanya kocha wake ajutie kwanini alimpa nafasi na alicheza sana kwa kufuata maekelezo kuliko ufundi wake ndiyo maana vita ya katikati ya uwanja ilikuwa kubwa.

Penalti gonjwa kwa Yanga

Wakati dakika 90 zinamalizika, asilimia kubwa ya mashabiki wa Yanga waliwapa ushindi Simba. Ndio walitamka Simba ameshavuka kwenda fainali.

Ni kama tatizo la saikolojia kwa Yanga linapokuja suala la penalti. Miaka ya karibuni wamekuwa wakishindwa kupata matokeo kabisa endapo wanafika kwenye penalti.

Si jambo la kukaa nalo tena vichwani na kuamini. Jibu pekee la tatizo lao ni kulifanyia mazoezi mara kwa mara ili kujenga hali ya kujiamini na ukomavu.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU