ZUENA BINT MSASAMBUKO (10)

ZUENA BINT MSASAMBUKO (10)

598
0
KUSHIRIKI

ILIPOISHIA jana…. Mimi nilikuwa nimelala kiubavu upande wa subira, miguu yangu ikielekea kule kule mbele alipokuwa shangazi. Baada ya kujikandika henna na kuridhika akaanza kujichora miguuni. SASA ENDELEA…

‘Shangazi si utupake na sie kwanza, umekazania ngoko hizo ka’ kwato za punda Farida akamtania shangazi

‘Kwato? We unazo?….baba Hijja alinipendea hizi kwato mwenyewe akisema mwanamke mwenye vigimbi ndiye mwanamke shupavu na mwanamke mwenyewe ndio mimi,’ shangazi akatambia mguu wake hali  akipandisha dera lake na kutuonyesha mguu wake mkavu, akituachia kicheko na tukacheka hasa!

‘Haya basi tujadili hayo Maulidi maana hata sijui itakuwaje?’ Mama akakatiza kicheko na kuulizia suala la msingi juu ya kile kikao. Mtoto wa Shabani alikuwa anatimiza siku 40 tangu kuzaliwa hivyo alitudokeza kuwa angeweza kufanya sherehe ya Maulidi ya mtoto wake pale nyumbani.

‘Kwanza yule mkewe amekubali Maulidi isomewe hapa?…Sio tujichetushe kuita waitikiaji dua na maustadhi halafu tuje sikia Maulidi inasomwa Kiparang’anda huko…tukose pa kuweka nyuso zetu’ shangazi akatoa dukuduku lake lililotufanya tucheke tena. Ni kweli Nursati wifi yetu alikuwa na kijitabia cha kujisikia. Akijaribu kila hali kuuficha ukweli kuwa mumewe Shabani alikuwa Mzaramo wa Mzenga  na yeye alitokea Kiparang’anda. Hiyo elimu ya kidato cha sita iliyompatia kazi ilitosha kumfanya atuone kama watu duni tusiostahili kumkaribia. Ukitaka kujua tabia halisi ya mtu subiri akamate pesa za maana akuzidi kidogo kwa kipato! Utajua wazi ipi pikipiki na ipi guta

‘Yule mwanamke naye asitutie wazimu sasa kila kitu Nursati Nursati, shabani naye ubwege umemjaa ….mwanamume gani  unamkabidhi kila kitu mkeo…mpaka maamuzi yako binafsi,’ Farida akaingilia kati huku akinyanyuka toka pale mapajani mwa mama na kuketi wima

‘Hhahahaaaaaa kamuachia akili za kuvukia barabara tu mnaloo?’ Shangazi akashadadia akitufanya tucheke zaidi

‘Tulitoe waaaapi!’ tukaitikia kishabiki huku tukicheka na kugongesha viganja.

‘Hapa ni kushikamana tu akileta za kuleta tunamwitia Mwanahija amkong’ote mpaka tumbo la uzazi limnyooke’ Farida akazidi kuchochea akimkumbuka na Mwanahija. Tukazidi kucheka tukikumbushiana makeke ya Mwanahija. Nikamkumbuka dada yangu kweli. Nikampigia simu!

‘….tupo hapa na shangazi Mama Hijja….subira…Farida na mama, tumekukumbuka mpaka basi’ nikaongea kwenye simu wengine wote wakinitazama kwa bashasha wakisikiliza majibu ya Mwanahija kupitia kiwambo cha sauti nilichoweka hewani.  Nikamsogezea mama simu baada ya Mwanahija kuomba kusikia sauti ya mama. Mama akazungumza naye

‘….maulidi ya mtoto wa Shabani mwanangu…..nakwambia hatuna a wala be….shabani mwenyewe hajatoa tamko lolote….haya Laaziz, usikose mwanangu….maulidi shurti shangazi na shangazi mwenyewe ndio wewe….uje bwana…haya’ nikakata simu uku tukicheka maana majibu yake yalikuwa yanatosha kukufanya ucheke mpaka ujikojolee. Mama akarudisha mada.

‘Tatizo baba yenu naye hana hata kauli juu ya shabani, angalau angemshauri afanyie maulidi hapa lakini ndio hivyo….kaka yako naye kichwa kile kama nazi tu’ mama safari hii akamnanga baba akimweleza shangazi ambaye alicheka kwanza kisha akamgeukia mama.

‘Wifi nawe vituko! Yule nazi hukuwaona wenye mapapai kichwani ukaolewa nao?’  tukacheka, safari nikinyanyuka kidogo nakumimina uji kwenye kikombe nilichokuwa natumia. Nilitaka kupunguza kasi ya kucheka.

‘….Tuyaache ya maulidi, haya kuna hili la huyu bi mdogo’ mama akabadili mada akinisonta na kidole cha shahada kilichobeba dole gumba na kuchanusha vile vitatu vilivyobaki.

‘Mimba tena?’ shangazi akadakia akitutolea macho na kututazama kwa awamu

‘bora ingekuwa mimba, kuna chotara mtoto wa Mzee Masoud njia panda hapo…wifi hatuli tukashiba hatulali tukaota’ mama akayasema yote akisimulia ayajuayo. Tukatazama na Subira aliyekuwa kimya akicheka tu kwa yale yaliyopo.

‘Makubwa! Kwanza Mzee Masoud yupi kwanza… yule mranda mbao kule kwenye kona pale au yule Masoud mwenye mtoto mwehu mwehu hivi ….’ Shangazi akauliza uku akikatishwa na Farida na kupewa jibu

‘mbali kote uko wapi shangazi! Mzee Masoud Abdilatif!’

‘Mtume Simama!….yule chotara anayeitwa nani sijui Selemani sijui sele nani sijui’

‘Salehe jamani ….’ Nikamsahihisha shangazi asizidi kuniharibia jina la chotara wangu

‘haya huyo huyo…. ila sasa ukisikia kubeba gunia la sukari na kulitosa baharini ukitegema bahari iwe tamu  ndiko hivi…wewe na yule mbona mbuzi na kuku….hamfanani kwa umbo wala ladha seuze bei?’ Shangazi akaninanga bila huruma. Wakati wengine wakicheka mimi nilitulia kimya nikilitazama dari.

‘Nimempenda shangazi’ nikajitetea nikijilaza mapajani mwa Subira.

‘Si umchukue sasa unangoja nini?’ Anamshushua

‘Anamdengulia kweli, juzi hapa kamtolea nje ndani ya gari, alipokuja kumuona bombani kampita kama hamjui vile’ Subira akasimulia baada mimi kumsimulia tukio zima baada ya lile tukio la bombani.

‘Sasa mnatakaje, nijifunge vitenge nikamgonge hodi nizungumze nae au? Shangazi akahoji akiivuta chupa ya uji na kujimiminia uji.

‘Ikiwezekana msaidie tufanye yale mambo yetu yale…tum…..’ Farida akaongea akishindwa kumaliza neno lake kwa mdomo na kulimalizia kwa kitendo cha kupuliza kiganja chake akianzia mwishoni mwa kiganja mpaka vidoleni.

‘Faridaaa!’ Mama akaita akimchoma kwa vidole vyake mapajani.

‘Eeh mama wanaume hawashikiki hawa bila dawa….watu kibao wanahangaika hivi hivi ndoa hakuna tutazaliana hapa kama panya,’ Farida kajitetea akiungwa mkono na shangazi.

Itaendelea Alhamisi

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU