ZUENA BINTI MSASAMBUKO (32)

ZUENA BINTI MSASAMBUKO (32)

399
0
KUSHIRIKI

ILIPOISHIA JANA…. Tukio la kwanza niliwahi kumkuta Judith akitoka katika duka la dawa analouza Isabella ingawa hakuniona kutokana na haraka zake, lakini nilijiuliza maswali ambayo sikuyapatia majibu ila nikahitimisha lile lilikuwa duka la dawa na yeyote angeweza kuingia….SASA ENDELEA

Baada ya ile hekaheka ya kukutana watatu nyumbani kwa Salehe,

likaja tukio la pili, la siku chache baadaye kumuona Judith akiwa kwenye gari lake akielekea kule kwenye duka la Isabella. Nikajipa kiulizo ambacho kiligeuka mshangao ulionifanya nigune tu na kushika hamsini zangu!

Nikakumbuka tukio hili la tatu la kumtuhumu Salehe kwa kuonana na Judith muda mfupi baada ya kuliona gari la Judith likielekea mtaa ule lilipo duka la Isabella na Salehe akanijibu ‘ana rafiki sijui ndugu sijui nani ana duka uko chini’ kwa muda ule nilipopokea hizi taarifa sikuisumbua akili yangu kujiuliza chochote wala kutaka kujua mengine! Nilichelea kuzalisha ugomvi bila kujua nilikuwa napulizia hewa ya moto ndani ya kopo lenye petroli!

Nikafanya makosa zaidi ya kumtuma Aisha kwenda kununua kifaa cha kupimia mimba kwa kumuandikia kwenye karatasi kifaa nilichohitaji toka duka la dawa, mazoea hujenga tabia, Aisha alishazoea kuvuka maduka yote ya dawa na kulifuata la Isabella. Najua alimhoji na najua Aisha alisema mimi ndio nilihitaji na taarifa zikamfikia Steve na Steve akamhoji Madobe kuhusu hili la mimi kuwa na mimba na ndio Madobe akili ikamkaa sawasawa! Binadamu tunavumilia tetesi si ushahidi!

Aliponipigia simu akihitaji pesa, Madobe alikuwa anajua Salehe anaoa na alikuwa anajua hamaniko nililonalo na kila kilichoendelea pale mtaani Madobe alikuwa anakijua ila maskini wa Mungu alikuwa anaumia ndani kwa ndani, akijaribu kila hali kupambana na habari zile akitamani zisiwe na ukweli. Akamtuma mjumbe afuate pesa lakini pia aje amjue Salehe vizuri na aje apate uhakika wa hiki na kile alichokuwa akiambiwa na mjumbe akarudisha taarifa kuwa ni kweli pengine akiziremba taarifa zake kwa madoido yote! Upambe kazi atakwambia kuna umati wa watu na utatoka ukute watu watatu.

Hivyo, nyodo zote nilizokuwa nikimfanyia alijua zilitoka wapi na zililetwa na nini na kabla hajaomboleza vya kutosha juu ya usaliti niliomfanyia, Matarishi wakamfikishia ujumbe Zuena wako ana mimba na hiyo mimba itakuwa ya Salehe Masoud! Yule mwanamume aliyewahi kumkuta hospitali mkaitana shemeji! Jiweke kwenye nafasi ya Madobe!

Ni Isabella huyu huyu ndiye hasa aliyempa taarifa Judith kuhusiana na mimi kuwa na Salehe na pamoja na Madobe! Nikakumbuka vizuri Salehe aliwahi kugombana na mimi kuhusiana na habari kuwa na mchumba. Nikamkana Madobe nikihitimisha tulikwisha achana siku nyingi. Nae akaniamini kwa vile kila alipokuja nyumbani hakuwahi kukuta nimelala nje na kila aliponitaka alinipata bila shaka!

Usimchezee mwanamke ukadhani unamjua alifu kwa ujiti! Mioyo yao ikifunguka leo hii unaweza kufa mdomo wazi kwa kujua mazito waliyobeba vifuani mwao! na ndio maana wapo wanaoamini kuwa shetani ni mwanamke!

********

Nilizinduka usingizini, nikihisi maumivu makali ya shingo. Nilisinzia nikiwa nimeketi, nikiegemeza kichwa upande. Salehe alikuwa amelala mapajani mwangu. Nikakumbuka usiku uliopita alikuwa na maumivu ya kichwa yaliyonihangaisha gizani. Nikamtazama na kutabasamu moyoni nikishusha pumzi na kuziparaza zile nywele zake laini zenye mawimbi. Akaamka!

Akaketi akiuma meno, bado alikuwa na maumivu makali ya kipigo alichopewa.  Akatikisa kichwa na kusonya… akatulia kidogo na kunitazama.

“Isabella ni nani?’ likawa swali lake la kwanza.

“Nadhani ndio yule rafiki wa Judith mwenye duka la dawa kibaha,”

‘kheeee!’ akauliza kwa mshangao akinitolea macho.

‘Ndio hivyo’ nikamjibu

‘okay!….Zuena nina mengi ya kukuuliza kuna vitu sivielewi hapa na nimepigwa sana jana na watu nisiowaelewa…lakini inaonekana kama….Judith ananiadhibu mimi na kuna mtu anakuadhibu wewe…okay Mado ni nani?’ akaongea kwa kuungaunga sentensi huku akipambana na maumivu ya hapa na pale. Sikulitarajia lile swali na sikulihitaji kwa wakati ule. Nikamtolea macho tu nikivangavanga!

Naye akanitolea macho, akingojea jibu. Nikashusha pumzi kwanza nikitafuta majibu ya haraka na nisipate hata moja la kuzugia. Tukatazamana tu mpaka tuliposikia mlango ukikorokocholewa ndipo tulipohamishia macho yetu kwenye kona ya kuelekea uko mlangoni, tukimsubiri kwa hamu huyo aliyefungua mlango

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU